Kitaifa
Serikali ya Rais Samia na mafanikio ya uwekezaji nchini
Moja ya kati ya maeneo ambayo Serikali ya awamu ya sita imeyapa kipaumbele katika kipindi cha uongozi wake ni kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Wakati akihutubia Bungue kwa mara ya kwanza Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali yake itachukua hatua mahsusi katika kukuza uwekezaji ambazo ni pamoja na kufanya marekebisho kadhaa katika sera, sheria na kanuni kwa kuondoa vifungu vitakavyobainika kusababisha vikwazo katika kukuza uwekezaji.
Mikakati hiyo imezaa matunda kwani ndani ya kipindi cha uongozi wake kumekuwa na mazingira rafiki ya uwekezaji na ajira kwa Watanzania hali iliyoleta mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda na biashara.
Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imefanikiwa kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuweka mazingira bora ikiwemo kuondoa vikwazo vilivyokuwa vinawakabili wawekezaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri anasema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024, Serikali imefanya mabadiliko makubwa ya kisera na kanuni ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Mabadiliko haya yanadhihirisha azma ya Tanzania ya kujenga mazingira bora na rahisi kwa ajili ya uwekezaji.
“Katika kipindi cha mwaka wa fedha Julai 2023 hadi Juni 2024, TIC imesajili miradi 707 ukilinganisha na miradi 369 iliyosajiliwa mwaka wa fedha 2022-2023 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 6.561 ukilinganisha na Dola za Marekani bilioni 5.394 mwaka wa fedha 2022-2023 na kutarajia kuzalisha ajira 226,585 ukilinganisha na ajira 53,871 mwaka wa fedha 2022-2023.
Kati ya miradi hiyo, asilimia 38.19 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 42.86 ni ya wageni na asilimia 19.38 ni ya ubia kati ya Watanzania na wageni,” anasema Teri.
Anasema katika kipindi hicho kumekuwa na ongezeko la asilimia 91.60 katika usajili wa miradi ikilinganishwa na kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024 ambapo miradi 707 ilisajiliwa ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2022-2023 ambapo miradi iliyosajiliwa ilikuwa 369 tu. Ajira zinazotarajiwa zimeongezeka kwa asilimia 320.61 kutoka 53,871 hadi 226,585.
“Thamani ya mitaji ya miradi iliyosajiliwa imeongezeka kwa asilimia 21.6 kutoka Dola za Marekani 5,394.83 milioni hadi Dola za Marekani 6,561.09 milioni,” anasema Teri.
Anasema sekta ya uzalishaji viwandani inaongoza kwa kuwa na miradi 313 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 2.462 ikifuatiwa na miradi ya usafirishaji 128 yenye thamani ya Dola za Marekani 1.035 bilioni, ya tatu ni ujenzi wa majengo ya biashara miradi 76 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.079, ya nne ni utalii yenye miradi 75 yenye thamani ya Dola za Marekani 349.40 na ya tano ni kilimo yenye miradi 56 yenye thamani ya Dola za Marekani 710.02 milioni.
Serikali imeendelea kuboresha Kituo cha Utoaji Huduma Pamoja kilichoko TIC kwa kuanzisha mfumo wa kusajili miradi ya uwekezaji kwa njia ya mtandao. Mfumo huu unaruhusu wawekezaji kusajili miradi yao mahali popote duniani ndani ya siku moja hadi tatu.
Kituo hiki kimesaidia katika kuharakisha mchakato wa usajili wa miradi. Kwa mfano, ongezeko la miradi iliyosajiliwa, kutoka 369 hadi 707 katika mwaka wa fedha 2023/24 ni ushahidi wa mapinduzi yaliyotokana na kituo hicho.
Pia kituo kimeanzisha huduma za haraka kupitia Premier Service Centre ambapo mwekezaji anaweza kusaidiwa kupata vibali na usajili kwa haraka zaidi ndani ya masaa 24. Kituo hicho cha huduma za pamoja kimeiwezesha TIC kushirikiana kwa karibu na taasisi 14 ambazo zina jukumu la kutoa vibali na leseni kwa wawekezaji.
TIC imeanzisha mfumo wa Kieletroniki unaofahamika kwa “Tanzania Electronic Investment Window (TeIW)”, ambao umekuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha wawekezaji na kuruhusu usajili wa miradi na maombi kutoka popote duniani.
Kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani
TIC imeanzisha kampeni mbalimbali za uhamasishaji uwekezaji, ikiwemo kampeni maalumu ya kitaifa kuhamasisha uwekezaji wa ndani iliyoanza Augusti 2023 ikihamasisha wawekezaji wa ndani kusajili miradi yao TIC na kutoa elimu ya uwekazaji kwa Watanzania. Kampeni hiyo ilizinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Septemba 25, 2023.
Awamu ya kwanza ya kampeni iliyofanyika mwanzoni mwa mwaka 2024 ilijumuisha mikoa 17 ya Tanzania ambayo ni; Mwanza, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Morogoro, Dodoma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Mtwara, awamu ya pili inayoendelea iliyoanza Julai 2024 imelenga kufikia mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara, Simiyu, Lindi, Ruvuma, Rukwa, Katavi na Kigoma .
Malengo ya kampeni hii ni kubadili fikra na mtazamo wa watanzania kuwa uwekezaji ni mahususi kwa raia wa kigeni na sio kwa Watanzania kwa kutoa elimu ya uwekezaji hususan taratibu za kusajili miradi mbalimbali ya uwekezaji kwa makundi mbalimbali katika jamii kwa lengo la kujenga uelewa na hamasa ya kusajili miradi na kunufaika na vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi.
Kampeni inahusisha kufanya semina kwa mikoa lengwa kwa wafanyabiashara, wajasiriamali, waandishi wa habari na wawekezaji kwa kushirikiana na uongozi wa mikoa na wilaya kwa lengo la kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani na kuwawezesha kunufaika na vivutio kwa lengo la kukuza uchumi.
Shughuli nyingine zinazotekelezwa ni pamoja na kutembelea baadhi ya miradi ya uwekezaji inayotekelezwa na wawekezaji wa ndani kwa kuambatana na vyombo vya habari kwa lengo la kuonesha utekelezaji wa miradi na kutoa shuhuda mbalimbali kutoka kwa wawekezaji Watanzania walionufaika na vivutio katika kufanikisha utekelezaji wa miradi yao.
Kampeni hiyo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020, inalenga pia kutekeleza azma ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufungua nchi kwa kuhamasisha na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi.
Katika kutekeleza kampeni hiyo, TIC imeamua kuufanya mwaka 2024 kuwa mwaka wa kitaifa wa uwekezaji kwa kuendesha awamu ya pili ya kampeni iliyoanza Julai 15 hadi Septemba 3, 2024, kwa kushirikiana na wakuu wa mikoa, wilaya na vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhamasisha uwekezaji.
Uwekezaji nchini unalenga kutatua changamoto mbalimbali katika jamii kwa kuleta ufanisi na faida mbalimbali zinazochagiza na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Kuvutia mitaji ya uwekezaji, kuleta teknolojia mpya na za kisasa kwa Watanzania, kuongeza fursa za ajira mpya kwa vijana, kuongeza mapato yatokanayo na kodi na yasiyo ya kikodi, kuendeleza ujuzi wa rasilimali watu nchini, kuongeza uzalishaji bidhaa nchini na kukuza uchumi na kuokoa fedha za kigeni zionazotumika kuagiza bidhaa mbalimbali nje ya nchi.
Teri anahitimisha kuwa, mikakati ya TIC ni kusajili miradi 1,000 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5 kwa mitaji ya kigeni na Dola za Marekani bilioni 3.5 kwa mitaji ya ndani. Pia inalenga kuhakikisha asilimia 10 ya miradi inachangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.