Kitaifa

Trafiki 168 wafukuzwa, wahamishwa kwa makosa ya kinidhamu

Dodoma. Askari wa usalama wa barabarani  168 wamechukuliwa hatua zikiwamo kushtakiwa kijeshi, kuhamishwa vitengo na kufukuzwa kazi, kutokana na makosa ya kinidhamu ikiwemo rushwa katika kipindi cha kuanzia Juni 2023  hadi Juni 2024.

Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani, Deus Sokoni ameeleza hayo wakati wa uzinduzi wa wiki ya usalama wa barabarani, inayoambatana na sherehe za miaka 50 tangu kuanzisha kwa Baraza la Usalama wa Barabarani.

Sokoni ameyasema hayo baada ya kuulizwa maswali na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango wakati akikagua mabanda yaliyopo katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Dk Mpango alihoji ni askari wangapi na hatua gani wamechukua.Akijibu swali hilo, Sokoni amesema wamewakamata askari 168 ambao wameondolewa katika utumishi wa  usalama wa barabarani, huku wengine wakichukuliwa hatua za kushtakiwa kijeshi na wengine kufutwa kazi.

Amesema askari wanane kati ya hao walifukuzwa kazi, 84 walionywa huku waliobakia wakihamishiwa katika vitengo vingine.

Dk Mpango amesema baadhi ya magari ya Serikali yanakimbia sana barabarani na wamekuwa hawaangaliwi mwendo  unaotakiwa wala wakati gani wa kupita gari jingine.

Amehoji madereva wangapi wa Serikali walikamatwa kwa kuendesha kwa mwendo kasi na hatua walizochukuliwa.

Akijibu swali hilo, Sokoni amesema madereva wa Serikali 253 walikamatwa mwaka jana, huku katika kipindi cha miezi sita cha mwaka huu, wakiwafutia leseni madereva 33.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Dk Mpango ameagiza udhibiti kwa magari yanayobeba wanafunzi ambayo alisema mengi yana hali mbaya, hali inayotishia usalama wa wanafunzi na madereva.

“Baadhi ya madereva wa magari hayo wanaonekana kukosa weledi, unaosababisha madhara mbalimbali ikiwemo ajali mbaya. Lakini pia yapo magari yanayobeba wanafunzi wengi kuliko uwezo wake, hali inayofanya watoto kusongamana na kukanyagana,” amesema.

Pia ameagiza Wizara ya Mambo Ndani iharakishe kukamilisha mapitio ya Sheria ya Usalama wa Barabarani, ikiwemo adhabu kwa makosa mbalimbali ya barabarani.

Aidha, Dk Mpango amesema ajali za pikipiki nchini zinazidi kuongezeka kila mwaka ambapo katika kipindi cha kati ya Januari hadi Desemba mwaka jana jumla ya ajali 435 zilitokea.

Amesema kati ya ajali hizo vifo 376 vilitokea ukilinganishwa na vifo 332 vilivyojitokeza mwaka 2022.

“Katika kundi hili la ajali za pikipiki hatuna budi kuendelea kusimamia sheria hususan katika uvaaji wa kofia ngumu, kutobeba abiria wengi kwenye pikipiki moja na umiliki halali wa leseni ya udereva pamoja na bima ya chombo cha moto,” alisema.

 

Mkakati kupunguza ajali

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema wapo katika utekelezaji wa mikakati inayolenga kupunguza ajali za barabarani.

Ametaja mikakati hiyo ni pamoja na mradi  wa miji salama, ukaguzi wa magari wa lazima na wa ufuatiliaji ambapo kutafungwa mifumo ya kisasa ya Tehama.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani, Daniel Sillo amesema kwa kuwa makosa ya kibinadamu ndio yanayoongoza kwa kuchangia ajali za barabarani, wameandaa mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na ajali za barabarani.

“Mkakati umelenga katika udhibiti wa madereva walevi na wanaoendesha kwa uzembe, udhibiti wa mwendo kasi, kuwashirikisha wamiliki wa vyombo vya moto katika dhana ya uwajibikaji, kudhibiti uendeshaji wa magari bila sifa na kutokuwa na bima,” aliyataja baadhi ya malengo ya mkakati huo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP) Camillus Wambura  amesema hivi karibuni wanatarajia kuzindua mfumo wa kielektroniki wa usajili wa wanafunzi wa shule za udereva ili makao makuu ya usalama wa barabarani waweze kufuatilia taarifa za kila mwanafunzi aliyesajiliwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, Vita Kawawa amesema kamati hiyo itaweka msukumo katika kuishauri Serikali kuongeza adhabu kwa makosa ya usalama wa barabarani baada ya kuona haziendani na athari zinazojitokeza.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi