Makala

Utafiti wafichua sababu mwanamke kulala zaidi ya mwanaume

Dar es Salaam. Kutokana na mwanamke kutumia ubongo wake zaidi, tafiti zimeonyesha anahitaji muda mwingi zaidi wa kupata usingizi ikilinganishwa na mwanaume, huku daktari akitaja sababu chanzo wanawake kuwa na vitambi kuliko wanaume.

Mwanamke ametajwa kufanya kazi nyingi na huzifanya kwa mara moja, kwa sababu hutumia zaidi ubongo wake halisi, hivyo huhitaji dakika ishirini zaidi za kulala kwa wastani wa saa 6 hadi 8 kwa siku kuliko wanaume wanavyohitaji.

Watafiti kutoka kituo cha utafiti wa usingizi cha Chuo Kikuu cha Loughborough nchini Uingereza, mapema wiki hii wamechapisha utafiti wao wakisema wanawake wanahitaji muda mwingi zaidi wa kupata usingizi kwa sababu wanatumia zaidi akili zao kuliko wanaume.

Kiongozi wa utafiti huo, Profesa Jim Horne kutoka chuo hicho amenukuliwa akisema akili za wanawake zimeunganishwa kwa njia tofauti, hivyo hitaji lao la kulala huwa kubwa zaidi.

“Wanawake huwa na kazi nyingi kuliko wanaume, hufanya maamuzi mara moja na wanaweza kubadilika hivyo hutumia zaidi ubongo wao halisi, lakini hata homoni zao zinaweza kuwa sababu nyingine ya kutofautiana kwa mahitaji ya usingizi kati ya mwanaume na mwanamke,” amesema Profesa Jim.

Amesema mzunguko wa kulala kwa wanawake unatawaliwa na homoni na kwamba homoni hizo huathiri wanawake na kuhisi uchovu na wakati mwingine wanahisi njaa.

Profesa Jim amesema pamoja na kwamba utafiti unaonyesha wanawake wanahitaji kulala zaidi kuliko wanaume, lakini pia tafiti zinaonyesha wana usingizi mrefu kidogo kuliko wanaume, wakilala kwa zaidi ya dakika 11 mbele.

Utafiti huo unaungwa mkono la Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige anayesema mwanamke anaweza kufanya vitu vingi zaidi kwa wakati mmoja kuliko mwanaume.

“Ana mtoto mgongoni palepale anafua, lakini anaweza kupika ana mmtoto mgongoni lakini anaweza kutumia mikono yake miwili katika kufanya kazi,” amesema.

Amefafanua kuwa katika masuala ya makuzi, mwanamke anakua haraka zaidi kuliko mwanaume kwani  binti wa miaka 14 atapaswa kuwa na kilo 49 na kijana wa kiume wa miaka 14 atakuwa na kilo 48.

Dk Mzige anafafanua kuwa hali hiyo hutokana na homoni anazokuwa nazo na akipevuka huongezeka uzito kuliko mtoto wa kiume na hiyo ndiyo sababu anakuwa na maumbile tofauti na mwanaume.

“Muda sahihi wa kulala ni saa 6 mpaka 8 lakini mwanamke bado anaweza kuamka usiku mara kadhaa kunyonyesha mtoto. Pia anaweza kutumia mikono yake miwili kwa wakati mmoja kufanya vitu tofauti huku akifikiria na kukumbuka vitu kwa haraka zaidi na anapevuka mapema zaidi kuliko mwanaume,” amesema Dk Mzige.

Amesema, “Muda sahihi wa kutosha unakuja wakati akiwa mjamzito lakini akishanyonyesha hakuna muda mzuri wa kupumzika kwa sababu anapaswa kunyonyesha mara 10 mpaka 14 kwa saa 24.”

 “Suala la usingizi ni kweli lakini ajue atakapokuwa mjamzito anapaswa kupumzika. Hii ndiyo sababu mwanaume anaambiwa msaidie kazi mama atakapokuwa mjamzito,” amefafanua.

Vilevile ameeleza kwamba katika maumbile na kukua mwanamke kutokana na chakula anachokula, mwingine hupevuka mapema kuliko bibi zao miaka ya nyuma kutokana na vyakula wanavyokula hivi sasa.

Amesema “Wengine wanapenda tabia bwete kuliko ilivyokuwa hapo kabla. Hata uzito wanawake wanakuwa na uzito mkubwa kuliko wanaume na wanawake wengi wana vitambi kuliko wanaume na wanaongoza pia watu wa Magharibi Unguja na Kilimanjaro, Tukuyu mkoani Mbeya na huko kusini wanaongoza kwa unene uliokithiri.”

 “Sijajua wametumia kigezo gani katika utafiti wao na majibu yao yalikuwaje na kulinganisha na tafiti zingine,” amehoji.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi