Connect with us

Kitaifa

Kuwatapeli waumini ni jinai kama unyang’anyi

Dar es Salaam, Utotoni tulikuwa na kawaida ya kuketi kwenye nyumba ya mmoja wetu kuangalia mikanda mipya ya video.

Ilikuwa hivyo kwani tulikuwa tukicheza pamoja, siku za mapumziko ya mwisho wa juma tukatafuta mkanda mkali na kuchagua pa kuuangalia siku hiyo. Wazazi walikuwa aidha wameenda kufanya kazi kwa masaa ya ziada au pengine nao walitoka kwenda matembezini.

Nakumbuka siku tuliyokwenda kwa mwenzetu ambaye mzee wake alikuwa mkali kama pilipili kichaa. Pale tulikwenda kwa nadra sana maana mzee angewakuta, angewakung’uta jicho hadi mkasambaratika bila kuagana. Lakini mwenzetu alitutamanisha kuwa baba yake alinunua mkanda wa Bruce Lee na akatuhakikishia kwamba angerudi usiku.

Basi dogo akawasha mtambo na kuucheza mkanda uliokuwamo kwenye deki. Tukaanza kuona picha ikikimbia katika hali isiyo ya kawaida. Kumbe siku ile ilikuwa ya bahati mbaya kwetu kwani mkanda ulikuwa na kasoro. Tulikuja kushtuka nusu yake ikiwa imemezwa ndani ya deki. Tukazima haraka na kushirikiana kuuchomoa. Ghafla tukasikia muungurumo wa gari kuashiria bingwa karudi!

Kila mmoja wetu aliruka na kutulia kwenye kiti. Tofauti na siku zote, mzee alinyoosha moja kwa moja kwenye deki, akabonyeza kitufe na akauwasha mtemba wake huku akijitupa kwenye kochi. Safari hii hakukuwa na picha bali ujumbe wa tatizo kwenye deki. Mzee akainuka kwenda kuichokonoa lakini alichokutana nacho kilimrusha hatua kadhaa nyuma.

Mzee alichanganyikiwa, akaipiga teke deki yake. Alipotugeukia sote tukala kona. Lakini kwa mujibu wa kijana mwenzetu, msala ulihamia kwa yule aliyemuuzia mkanda. Anasema mzee aliingia chumbani kwa ghadhabu kuu, sijui alichukua kitu gani na dakika hiyo akatoka kama nyumbu aliyejeruhiwa. Akawasha gari na kutimua vumbi kuelekea kusikojulikana.

Hapo ndiyo utajua ubaya wa bidhaa feki. Mwenyewe alitoa fedha kununua mkanda aliousikilizia kwa hamu kubwa, akawahi kurudi ili atoe msongo kwa muvi hiyo mpya lakini akakutana na maudhi. Kwa jinsi tunavyomfahamu mzee wetu, bila shaka muuzaji alikiona cha moto. Si tu kwamba alirudisha fedha, bali alishikishwa adabu maana kwa tafsiri nyepesi alimchukulia mzee wetu kuwa zuzu.

Miaka ya hivi karibuni kumezuka kundi la viongozi wa dini. Hawa wanatumia visaidizi vya maombi kama maji ya upako, mafuta ya upako, udongo, chumvi, leso, keki za upako na vingine vingi kwa kuwatoza waumini gharama kubwa za visaidizi hivyo. Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa waumini ambao hawakufanikiwa kupata kile walichohitaji ama kuahidiwa na viongozi wa dini.

Mimi sitaki kuingilia imani za watu, lakini nikivaa viatu vya waumini naona wazi kwamba kuna kasoro mahala fulani. Wakati ule wa mfumuko wa waganga wa asili watu wengi waliteseka badala ya kupata ahueni.

Ni wazi kuwa Mungu anapowaleta Mitume, shetani hakosi kuingilia kati. Hivi sasa katika mfumuko wa wanaojiita mitume na manabii, matapeli hawachezi mbali kuwatesa wahitaji. Sisemi kuwa wote lakini kwenye msafara wa mamba kenge hawakosekani.

Niliwahi kuona video kwenye mitandao ya kijamii ikimwonesha Mchungaji maarufu hapa nchini akikemea vitendo vya baadhi ya manabii wa kisasa. Alisema yeye alishakutana na ishu ya “kukumbatia jasho la nabii” kwa malipo. Ati ukifanya hivyo nyota yako inasafishwa na matatizo yanakuacha. Haishangazi kuona waumini wakigombania jasho, kwani wapo waliouziwa ploti za mbinguni huko Mexico.

Dunia ya sasa inashangaza sana. Mtu ataona tangazo barabarani: “Jiunge na Freemason kwa kupiga namba hizi…” Atazipiga hizo namba na kuambiwa “Tuma Shilingi laki moja kwa usaili” naye atatuma. Akigundua amepigwa ndipo atakapoanza kulalamika. Mwingine ataambiwa kuna mikopo rahisi bila riba, lakini kwanza awekeze kiasi fulani.

Waswahili walisema “Hakuna raha bila jasho.” Iwapo ni kweli manabii hawa wanawatakia mema waumini wao, wangewakumbusha maandiko ya “Asiyefanya kazi na asile”.

Ingelikuwa mambo ni rahisi kama wanavyohubiri, basi hata wao wangelala tu nyumbani na kuomba fedha ziteremke. Haina tofauti na mganga wa fedha za majini anayelala kwenye kibanda cha maboksi.

Kuna ukweli kwa watu kuwa na shida mpaka wakarukwa na akili. Wakati mtu anapotetea uhai wake huwa tayari kwa jambo lolote. Atakuwa tayari kuuza kila alicho nacho katika kujitibu, atatekeleza kila sharti hata ikiwa kwenda mtupu kuvunja nazi makaburini. Hapa ndipo waganga feki wanapojiokotea fursa na kumfanya mgonjwa huyo kuwa mtaji wao.

Viongozi wetu wa kiimani wanaongozwa na utu na huruma. Kwa kuwa nyakati hizi tunawaona wakitembelea misafara ya magari ya kifahari, tungetegemea wampe mgonjwa uponyaji wa bure kama muasisi wao alivyokuwa akifanya. Tena basi kwa kuwa wengine hupita wakigawa fedha barabarani, basi mgonjwa angeweza kupewa nauli na hela ya kula.

Lakini mgonjwa atakutana na ada ya kumwona nabii, fedha ya maji ya upako, mafuta, leso, udongo, chumvi na mambo mengine kemkem. Kwa gharama hizi wagonjwa wanaumia badala ya kupona. Nadhani hili ndilo lililofanya Baraza la Muungano wa Makanisa ya Pentekoste kuwakana manabii hawa kwani wanawaunguzia picha.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi