Connect with us

Kitaifa

Sh486 milioni kujenga daraja Mto Isenga

Songwe. Hatimaye daraja la Mto Isenga lililopo wilayani Ileje Mkoa wa Songwe limeanza kujengwa kwa gharama ya Sh486 milioni, huku likitarajiwa kurahisisha usafiri kwa wananchi katika vijiji 71 zilivyomo wilayani humo.

Akizungumzia ujenzi huo leo Alhamisi Julai 25, 2024, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) wilayani humo, Asamisye Pakibanja amesema ujenzi huo utawaondolea adha wananchi, hasa wakati wa mvua na kwamba Serikali imeshatoa fedha za ujenzi.

Mbali na daraja hilo, Mhandisi Pakibanja amesema Serikali imetoa Sh2.8 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa daraja linalotenganisha vijiji vya Ilanga na Namwangwa, wilayani Mbozi na kutenga Sh50 milioni kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa daraja la Mto Mafumbo katika Kijiji cha Ibezya Kata ya Ndola.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Ileje, Godfrey Kasekenya amesema katika kuimarisha miundombinu ya barabara, Serikali imetenga Sh74 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami barabara yenye urefu kwa kilomita 51 Isongole- Isoko, huku ikitarajia kutafuta fedha kukamilisha kipande cha Ndembo- Kasumulu.

Kasekenya amesema wamefanyia ukarabati kwa kuweka zege kwenye maeneo yaliyoharibika katika barabara ya Kafwafwa- Ibungu ambayo yalikuwa hayapitiki msimu wa mvua na kusababisha wananchi wa Tarafa ya Bundali kutopata huduma za kijamii.

“Serikali kupitia Tanroads Mkoa wa Songwe inatarajia kufanya upembuzi yakinifu wa barabara ya kutoka Isongole – Itumba Shigamba – Ibaba Katengele, ili ijengwe kwa kiwango cha lami na ikikamilika Wilaya ya Ileje itakuwa imefunguka,” amesema Kasekenya.

Kutokana na ujenzi huo, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Chitete waliozungumza na Mwananchi wameishukuru Serikali, huku wakisema ujenzi wa madaraja kwenye Mto Isenga utawapunguzia adha ya usafiri nyakati za mvua za masika.

Lucas Mgode, amesema msimu wa masika wananchi wa kjijiji hicho walikuwa wakiishi kama wapo kisiwani, kwani walikosa huduma za kijamii, zikiwemo za afya na elimu kwa upande wa wanafunzi wa sekondari ya Kakoma.

“Tunaishukuru Serikali kwa kusikia kilio cha wananchi kutenga fedha kwa aajili ya ujenzi wa madaraja hayo ambayo wamehangaika kwa miaka mitatu, lakini sasa tunaamini msimu ujao wa mvua tutaondokana na adha hiyo ukilinganaisha na miaka ya nyuma,” amesema Mgode.

Naye Eneliko Mtambo, amesema kwa miaka ya hivi karibuni wamepoteza ndugu zao waliotumbukia Mto Isenga linapojengwa daraja hilo, wakiamini ujenzi huo utakuwa suluhu kwa wanafunzi kutokosa masomo msimu wa masika.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi