Kitaifa

Polisi latahadharisha matumizi ya fedha taslimu ukaguzi wa magari

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema katika ukaguzi wa vyombo vya moto unaoendelea mikoa yote nchini, hakuna fedha taslimu itakayopokewa mkononi bali malipo yote yatafanyika kwa mfumo wa malipo ya Serikali kwa kutumia namba ya kumbukumbu ya malipo ‘control number’.

Kauli hiyo kwa umma imetolewa leo Julai 21, 2024 na Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime zikiwa siku 12 zimepita tangu kuanza kwa ukaguzi Julai 9, 2024, ikiwa ni katika kuadhimisha Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani inayolenga kukumbusha watu kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama.

“Jeshi la Polisi lingependa kusisitiza katika ukaguzi unaoendelea hakuna fedha taslimu itakayopokelewa mkononi ama na askari, ofisa wa Polisi au wanaojifanya vishoka. Fedha yoyote kwa ajili ya ukaguzi wa chombo cha moto ilipwe kupitia mfumo wa malipo ya Serikali (control number)” imesema taarifa hiyo.

Polisi limesema ukaguzi  unaofanyika mwaka huu, mmiliki wa chombo cha moto atalipa ada ya ukaguzi kupitia namba ya malipo atakayopewa au atakayopakua kutoka katika mfumo ndipo chombo chake kitakaguliwa na kupatiwa stika.

“Wamiliki wa vyombo vya moto mnasisitizwa kufuata utaratibu huu kwani atakayebainika kutoa malipo ya fedha ya ukaguzi wa chombo cha moto mkononi (cash) au atakayepokea malipo hayo mkononi awe mmiliki, askari, kishoka au yeyote yule atakamatwa na kufikishwa mahakamani,” imeeleza taarifa hiyo.

Misime katika taarifa hiyo amesema kila mwaka huwa wanaadhimisha siku hiyo ili kuzuia ajali zinazosababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na miundombinu.

“Huwa tunafanya ukaguzi wa vyombo vya moto (pikipiki, bajaji na magari) ili vile visivyofaa (vibovu) kwa matumizi ya barabarani wamiliki tunawaelekeza kurekebisha kasoro zilizobainika,” amesema.

Amesema yote yanafanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani zinavyoelekeza.

“Mwaka huu maandalizi ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani tayari yameshaanza ikiwepo ukaguzi wa vyombo vya moto ulioanza tangu Julai 9, 2024 katika mikoa yote,” amesema katika taarifa hiyo.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi