Kitaifa
Mabasi mapya 100 kupoza makali mwendokasi
Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam kwa sasa liko ‘bize’ kiasi cha kama ni mgeni unaweza kudhani linajengwa upya. Maeneo mengi vumbi linatimka kutokana na ujenzi wa barabara.
Barabara kadhaa, zikiwamo za Nyerere, Uhuru, Sam Nujoma, Bibi Titi na Kawawa watumiaji wanapita kwa shida, lakini hawalalamiki kwa kuwa kinachoendelea kitakuja kuwa na manufaa kwa Taifa.
Ni kazi inayoendelea ya ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mabasi ya yaendayo haraka maarufu mwendokasi.
Awali usafiri huo ulipoanza katika awamu yake ya kwanza, Watanzania waliamini ungemaliza changamoto ya usafiri wa umma katika jiji hilo ambalo ni kitovu cha biashara.
Hata hivyo, kinachoendelea kwa sasa katika utoaji huduma ni tofauti na matarajio ya wengi. Mradi umegubikwa na changamoto nyingi, hautoi huduma zenye kuridhisha abiria.
Malalamiko ya wengi ni huduma mbovu zisizo na viwango, abiria kusubiri mabasi muda mrefu, huku wakiwa wamerundikana vituoni ambako hakuna huduma za kijamii.
Sababu inayotajwa mradi huo kugubikwa na changamoto, ni uchache wa mabasi ambao haukidhi mahitaji ya abiria.
Mradi wa usafiri wa mabasi ya mwendokasi ulizinduliwa Januari, 2017 na Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli.
Uko chini ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) unaomiliki miundombinu na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) iliyotoka ubavuni mwa Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA) inayomiliki mabasi.
Awali, UDART ilikuwa uwekezaji wa sekta binafsi, lakini kwa sasa unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 85, lakini bado umeshindwa kuonyesha ufanisi na kupunguza changamoto kwenye usafiri wa umma nchini.
Msajili Hazina aingilia kati
Kutokana na yanayoendelea kwenye mradi huo, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeingilia kati, kuhakikisha unaendeshwa kwa ufanisi na kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali na wadau.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo Julai 15, 2024, msajili huyo, Nehemia Mchechu amesema ofisi yake imeendesha vikao na wadau, kuhakikisha mradi huo unajiendesha kwa ufanisi na kutoa huduma bora.
Kutokana na hilo, Mchechu amesema mabasi 100 yanatarajiwa kununuliwa na kuingizwa kutoa huduma kwenye njia kuu za awamu ya kwanza ya mradi, akieleza mchakato umekwishaanza kwa kushirikiana na Benki ya NMB ambayo itafadhili kwa kutoa mkopo.
“Kesho (Julai 16) nitakuwa na kikao na NMB kwa ajili ya ununuzi wa mabasi 100, hivyo tutatatua changamoto ya uchache wa mabasi,” amesema Mchechu.
Kwa mujibu wa Mchechu, mabasi hayo 100 yatakuwa yamefika ndani ya miezi sita kuanzia sasa, huku njia zingine za mlisho ambazo ujenzi wake unaendelea zikisubiri utaratibu mwingine.
“Nimefanya mikutano na watu wa Dart na Udart pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) na sasa tumeshafikia ukingoni,” amesema.
Hata hivyo, amesema changamoto za mradi huo ni nyingi na zimechochewa zaidi na mwanzo wa safari yake na kwamba, Serikali imeendelea kuzitatua. Miongoni mwa changamoto hizo ni madeni na mabasi mengi kuharibika.
“Tunafahamu umiliki wa kampuni inayosimamia mradi huu, ilianza ikiwa sekta binafsi na sasa Serikali inamiliki asilimia 85, lakini kulikuwa na mambo mengi ambayo tumeendelea kuyatatua taratibu. Ila mwanzo wa safari ya huu mradi imekuwa changamoto,” amesema Mchechu bila kuingia ndani zaidi, akiahidi Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi wa Dart, watapata fursa ya kuja kueleza mikakati inayoendelea.
Kampuni zaidi kuendesha mwendokasi
Kutokana na kusuasua kwa utoaji huduma kwenye njia za mradi wa awamu ya kwanza, Mchechu amesema zitahitajika kampuni zaidi ya nne kuwekeza kuuendesha ili kuongeza ufanisi.
“Sitaki kuwa na kampuni moja ili siku wakikwama au wakigoma basi mji mzima usimame, lakini tukiwa na mwekezaji zaidi ya mmoja itasaidia kujua nani anatoa huduma nzuri. Hapa tutahitaji kuwa na kampuni tatu hadi nne kwa ajili ya kutoa huduma,” amesema.
Katika awamu ya kwanza ya mradi huo (inayofanya kazi sasa) mabasi 210 yalinunuliwa ili kuhudumia njia za Kimara -Kivukoni, Kimara –Gerezani, Kivukoni –Kimara, Gerezani – Kimara, Mbezi Luis–Kivukoni, Mbezi Luis –Gerezani, Kivukoni –Mbezi luis, Gerezani –Mbezi Luis, Mbezi Luis–Hospitali ya Muhimbili, Hospitali ya Muhimbili –Mbezi Luis, Kibaha –Gerezani na Kibaha –Gerezani.
Matokeo ya usanifu ya Agosti, 2019 yanaonyesha mtandao wa barabara ulihitaji kilomita 154.4. Matokeo pia yanaonyesha mahitaji ya watumiaji wa usafiri wa umma yataongeza hadi kufikia abiria 2,590,000 kwa siku ifikapo mwaka 2025 kwa mahitaji ya mabasi 1,975 katika njia 80.
Kwa mujibu wa utafiti wa Dart, ifikapo mwaka 2030 watumiaji watafikia 3,050,000 kwa siku kwa mahitaji ya mabasi 3,290 katika njia zipatazo 129. Idadi hiyo itakuwa ni zaidi ya robo ya wakazi wa jiji hilo linalokadiriwa kufikia wakazi milioni 10 ifikapo mwaka 2030.
Awamu ya kwanza inayotoa huduma ilijenga kilomita 20.9 kwa thamani ya Dola 260 milioni. Awamu ya pili inatarajiwa kujenga kilomita 20.3 kwa Dola 141.7 milioni, awamu ya tatu kilomita 24.3 kwa Dola 148.2 milioni na awamu ya nne kilomita 30.1 kwa Dola 97.9 milioni.
Awamu ya tano Euro 178 milioni (Sh500 bilioni) na awamu ya sita Dola 261 milioni. Kwa sasa, awamu ya pili ya mradi huo kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu kilomita 20.3 inatarajiwa kuanza wakati wowote baada ya mzabuni wa ununuzi wa mabasi kupatikana.
Hata hivyo, wakati Mchechu akizungumzia uwepo wa zaidi wa kampuni moja kwenye uendeshaji wa mwendokasi, Machi 26, 2024, Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athuman Kihamia alisema zaidi ya kampuni 30 zimejitokeza kuwania zabuni kuwekeza kwenye uendeshaji wa mwendokasi.
Kauli ya Dk Kihamia ilitokana na Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa kutaka sekta binafsi ishirikishwe kwenye uendeshaji wa mradi huo.
“Zaidi ya kampuni 30 zimejitokeza, lakini mpaka sasa hakuna iliyoshinda zabuni, Dart bado inaendelea na mchakato,” alijibu Dk Kihamia bila kutaja majina ya kampuni hizo zaidi ya kueleza mbili zinatoka Dubai, Asia, Uingereza na zingine barani Afrika.
Wakati Dk Kihamia akigusia uwepo wa kampuni hizo, siku chache nyuma Kamishna wa Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila alinukuliwa na kituo cha Azam TV akisema kampuni ya uendeshaji ya Dubai imekwishapatikana na kinachoendelea ni mazungumzo ya kimkataba baina yake na Dart.
Alipoulizwa ni wangapi wamejitokeza kuwekeza kwenye mfumo wa PPP, Kafulila alisema: “Kwa sasa tuko kwenye hatua ya majadiliano na mwekezaji ili kufunga mkataba na bila shaka pengine ndani ya mwezi ujao, mkataba kati ya mwekezaji na Serikali utakuwa umepatikana.”
Mifumo ya mapato tatizo
Licha ya changamoto zilizopo kwa sasa, Mchechu pia ameilekeza Dart kukamilisha ufungaji wa mfumo wa malipo ya nauli kwa njia ya kielektroniki.
“Kama kuna wizi mkubwa unafanyika ni katika malipo ya fedha kwa mkono na tayari tumekubaliana hadi Agosti, 2024 Dart waachane na mfumo wa malipo ya fedha taslimu,” amesema.
Mashirika zaidi kufumuliwa
Katika kuhakikisha mashirika ya umma yanajiendesha kwa ufanisi, Mchechu amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuwafyeka watendaji watakaoshindwa kuyaendesha kwa ufanisi.
Amesema kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyoagiza ni lazima mashirika ya umma na yale ambayo Serikali inamiliki hisa yatoe gawio.
“Katika hilo, tutalisimamia kikamilifu, ni lazima Serikali ipate gawio kinyume chake kama mtendaji umepewa kila kitu kisha shirika halijiendeshi kwa ufanisi, tunakuondoa tu,” amesema.
Mchechu amesema ofisi yake inaendelea na mikakati ya kuboresha na kupanga mikakati na watendaji wa mashirika ya umma likiwemo Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Pia, amewataka wenyeviti wa bodi za taasisi na mashirika ya umma nchini, kuandaa mpango wa kuwa na warithi kwenye nafasi za juu za uongozi.
Majina ya warithi hao kwa mujibu wa Mchechu, yatokane miongoni mwa watendaji katika taasisi hizo, ili wanaporithi nafasi za uongozi wawe na uzoefu wa utendaji wa taasisi husika.
Amesema kuanzia mwaka huu, bodi hizo zinatakiwa angalau kuwa na majina matatu ya warithi watakaotokana miongoni mwa watumishi ndani ya taasisi husika.
Kikao kazi
Katika hatua nyingine, amesema wiki ya mwisho ya Agosti mwaka huu, kutafanyika kikaokazi cha wakuu wa taasisi za umma mkoani Arusha.
Pamoja na mambo mengine, watajadili kuhusu maazimio ya kikao kazi cha mwaka 2023.