Connect with us

Kitaifa

Goba wamlalamikia Waziri Aweso ukosefu wa maji, awaomba radhi

Dar es Salaam. Wakazi wa Kata ya Goba, Halmashauri ya Ubungo, jijini Dar es Salaam wamemlalamikia Waziri wa Maji, Jumaa Aweso uhaba wa maji unawakosesha furaha ya kuishi, huku wakimtaka kuuondoa uongozi wa kimkoa wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Makongo na kuweka wengine watakaokuwa tayari kuwapatia huduma hiyo.

Wamesema licha ya kufikiwa na miundombinu, kuzungukwa na matenki ya maji, ikiwemo lile la Chuo Kikuu cha Ardhi na Mshikamano, wana miezi mitatu sasa hawapati huduma hiyo.

 

Wananchi hao wamefunguka hayo kwenye mkutano uliofanyika Mtaa wa Kibululu Kata ya Goba, leo Jumanne, Julai 2, 2024 ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara ya Waziri Aweso kutembelea maeneo yanayohudumiwa na Dawasa ambayo mara kadhaa yamekuwa yakilalamikiwa.

Waziri Aweso anafanya ziara hiyo takribani wiki moja imepita tangu Mwananchi Digital liripoti hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam.

Habari hiyo ya uchunguzi iliangazia jinsi baadhi ya wakazi za jiji hilo wanavyopata adha ya upatikanaji wa huduma hiyo. Mathalani eneo la Msumi, Kata ya Mbezi wanadiriki kutumia saruji kuyasafisha, ili kuwawezesha kutumia.

Kadhia hiyo ilimfanya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew kufanya ziara Machi 20, 2024 maeneo mbalimbali kujionea hali halisi ya upatikanaji wa maji akieleza, ameagizwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Mwanzo wa ziara ya Aweso ndani ya Dawasa ilikuwa Jumapili ya Juni 30, 2024 alipotembelea maeneo ya tenki la Chuo Kikuu cha Ardhi, Luguruni, Mshikamano na Tegeta A na kukuta hayana maji.

Kutokana na hilo, Waziri Aweso aliiomba Bodi ya Dawasa inayoongozwa na Mwenyekiti, Jenerali mstaafu, David Mwamunyange kuridhia uamuzi wa kumsimamisha kazi Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Kiula Kingu na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji wa Dawasa, Shaban Mkwanywe.

Alichukua uamuzi huo, ili kupisha uchunguzi wa utendaji usioridhisha na kusababisha kutopatikana kwa huduma ya maji katika eneo wanalolisimamia.

Jana Jumatatu Julia mosi, 2024, alimsimamisha kazi Meneja wa Dawasa Kinyerezi, Burton Mwalupaso kutokana na kushindwa kumudu majukumu yake. Ziara hizo ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri.

Leo Jumanne Julai 2, 2024, akiendelea kupita maeneo mbalimbali ya Ubungo, Mkazi wa Mtaa Mpya, Kata ya Makongo, Bernad Mapalala amesema kwa sasa hawafanyi maendeleo kwa sababu wanatumia fedha nyingi kununua maji kwenye maboza baada ya kukosa huduma ya Dawasa.

“Tunajua ni hujuma zinaendelea, tumepitiwa na miundombinu ya maji, lakini hayatoki. Waziri kuna watu wanatuuzia huduma hii kwa bei ghali, boza moja la lita 1,000 ni Sh 12,000 hadi Sh13,000 kwa ajili ya matumizi nyumbani,” amesema.

Mapalala aliyeonekana mwenye hasira, amesema wanachoamini wanafanyiwa hujuma na viongozi wa Dawasa kwa kukubaliana na wauza maboza wafanye biashara.

“Tunashauri kiongozi wetu safisha viongozi hawa, tuletee wengine watu tupate huduma,” amesema.

Kwa upande wake, Anna Kajigili amesema katika mtaa wao wa River View wana miezi mitatu sasa hawana maji ya Dawasa, lakini wanashangaa kila mwezi wanatumiwa bili.

“Waziri inakuwaje hatupati maji, lakini tunaletewa bili za maji kila mwezi zinatoka wapi hizi bili wakati siku hizi tunajinunulia katika maboza. Hii changamoto inatukosesha furaha ya kuishi, tunaomba majibu kabla hujaondoka,” amesema.

Kwa upande wake, Diwani wa Makongo, Ether Ndowa amesema licha ya changamoto hizo, Dawasa wana shida ya kutunza nyaraka za watu wanaomba kuunganishiwa huduma.

“Wameomba wananchi wengi kuunganishiwa maji, lakini hakuna kinachoendelea, wakifuatilia hawana taarifa wanaanza mchakato upya, wakati mwingine wanajibu hawana vifaa inakuwa shida,” amesema.

Amesema kata hiyo imezungukwa na matenki matatu ya maji, ikiwemo Chuo Kikuu cha Ardhi, Mshikamano na Kibamba, lakini huduma hiyo wanaisikia kwa majirani.

Maswali na Majibu

Baada ya wananchi hao kueleza kero zao, Waziri Aweso alimuuliza Meneja wa Dawasa mkoa wa kihuduma Makongo, Mkashida Kavishe inakuwaje watu hawapati huduma.

Kavishe alisema:”Tunashindwa kuwapatia maji wananchi kwa sababu matenki tunayotegemea hayana maji.”

Waziri Aweso: Inakuwaje watu wanaomba kuunganishiwa maji na wengine wamelipia kabisa shida nini meneja, sheria inasemaje?

Kavishe:Mheshimiwa Waziri, sheria inatutaka tuwaunganishie siku saba baada ya kulipia, lakini tatizo lilopo hatuna vifaa, tulishawaandikia bajeti makao makuu tangu mwaka wa fedha uliopita hatujaletewa vifaa.

Baada hapo, Waziri Aweso aliwaomba msamaha wananchi hao na kuwaeleza wameshaanza kuchukua hatua, ikiwemo za kinidhamu kwa baadhi ya watendaji tangu juzi Jumapili.

“Tuna mpango wa kusafisha Dawasa yote, tubaki na watendaji walio tayari kufanya kazi kwa kuwajibika. Hatutaki watendaji wanaoshinda ofisini wakati watu hawapati huduma, tunataka watoke,” amesema.

Amesema wakati wakiendelea kuchukua hatua kuhusu kukosekana maji kwenye matenki, kuna taratibu wanazichukua na muda si mrefu wananchi hao wataanza kuona mabadiliko.

“Wananchi ambao hamjaunganishiwa maji, kesho viongozi njooni muwaunganishie mtajua kwa kutoa vifaa, ila nataka wananchi  waunganishiwe huduma,” amesema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi