Makala

Namna ya kuongeza matumizi ya intaneti nchini kwa tija

Dar es Salaam. Hali ya mipango miji na viwango vya kodi vinavyotozwa katika baadhi ya huduma za mtandao vimetajwa kuwa vinapunguza kasi ya ufikishaji na utumiaji wa mtandao wa intaneti kwa Watanzania wengi.

Mpaka Machi 2024, idadi ya laini za simu zinazotumika zilikuwa zimefikia milioni 72.5 (upenyaji wa asilimia 111), ikiongezeka kutoka milioni 47.7 (upenyaji wa asilimia 78) kipindi kama hicho miaka mitano iliyopita.

Watumiaji wa intaneti nchini hivi sasa wamefikia milioni 36.8 na intaneti ya simu ndiyo njia maarufu zaidi ya kupata Intaneti, ikiwa na laini milioni 24.4. Teknolojia ya 2G bado ina matumizi makubwa, ikiwa na laini milioni 12.25. Teknolojia za faiba nyumbani ni 49.163 na faiba ofisini ni laini 5,126.

Kulingana na ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), idadi ya laini zinazotumia intaneti imeongezeka kwa zaidi ya milioni 5.1, sawa na wastani wa ongezeko la laini zaidi ya milioni 1 kila mwaka.

Mpaka Machi, 2024 asilimia 88 ya idadi ya Watanzania ilikuwa imefikiwa na intaneti ya kasi (walau 3G, 4G na 5G), hata hivyo asilimia 72 tu ya eneo la nchi lilikuwa limefikiwa na mtandao huo.

Kuhusu suala la usambazaji wa mtandao mkuu wa ufundi wa kampuni ya mawasiliano ya Tigo, Emmanuel Mallya anasema watoa huduma wengi wamewekeza kuhakikisha miundombinu ya mtandao inapatikana na sasa changamoto iliyobakia ni upande wa matumizi.

“Mfano sisi tumesambaza miundombinu ya 4G kwa asilimia 94 na ina uwezo wa kuhudumia wateja wengi zaidi ya tunaowahudumia sasa, lakini shida ni kuwa matumizi yanahitaji watumiaji nao wawe na vifaa vya kuwawezesha kutumia huduma hiyo inayokuwa imewekwa,” anasema Mallya.

Mallya anasema kama Tanzania inataka kuwa ya kidijitali, haina budi kupunguza gharama za kuwekeza na kutumia huduma za mtandao kama yalivyo mataifa mengine ambayo yanapiga hatua kwa kasi katika eneo hilo.

“Tuna importy duty (ushuru wa forodha) ya asilimia 20 hadi 28 kwa vifaa vya kidijitali, hii inapaswa kupunguzwa tukiangalia mbele zaidi. Kama tunataka kufaidi matunda ya dijitali hatuna budi kupunguza au kuondoa kabisa tozo ya kupitisha Mkongo wa mawasiliano ardhini, hapo tu Rwanda hiyo tozo haipo,” anasema.

Hata hivyo, Mallya anasema hatua ya Serikali kuiondoa tozo hiyo katika bajeti iliyopita ilileta nafuu kubwa ambayo anaweza kuihusianisha na urahisi wa huduma mpya ya Fiber majumbani na ofisini iliyoanzishwa na mtandao huu Aprili mwaka huu.

“Punguzo la tozo hiyo kutoka Dola za Marekani 1,000 kwa kilomita hadi Dola 100 limeleta nafuu kubwa pengine ndiyo maana hata nasi tumeweza kutoa huduma hii ambayo tunatarajia tutaitoa kwenye miji yote mikubwa, tukianza na majiji kwa kuwa hayo yana uhitaji mkubwa,” anasema.

Mallya anasema changamoto nyingine katika usambazaji wa faiba ni maeneo ya kupitisha nyaya hizo, kwani maeneo mengi ya miji hayajapangiliwa vizuri, lakini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine usambazaji wao ulianzia Mbweni, jijini Dar es Salaam.

“Kama ilivyo kawaida yetu tunazingatia zaidi ustahimilivu kuhakikisha huduma zetu zinakuwa za uhakika muda wote. Nafikiri mliona hata wakati wa changamoto ya intaneti baada ya kukatika kwa mkongo wa baharini majini sisi hatukutetereka,” anasema Mallya.

Akizungumzia huduma ya Tigo ya faiba majumbani na ofisini, Ofisa Mkuu wa Biashara, Isack Nchunda anasema lengo ni kuendelea kuwajumuisha watu wengi zaidi katika ulimwengu wa kidijitali katika zama ambazo matumizi ya teknolojia hiyo yanakua kwa kasi.

“Huduma zetu sasa zimekuwa zaidi ya kupiga simu na kutumia ujumbe, tofauti na tulivyoanza karibu miongo mitatu iliyopita. Mambo mengi yamebadilika kuanzia teknolojia na hata watu wanahitaji zaidi mtandao wa intaneti wenye kasi ili kufanya shughuli zao,” anasema Nchunda.

Anasema ndiyo maana pamoja na kuwekeza kwenye tekinolojia za 5G na 4G wameanzisha na huduma ya faiba ambayo inatoa uhakika wa kasi zaidi, huku ikiwaunganisha watu wote wanaokuwa kwenye nyumba au ofisi hiyo bila kikomo.

“Lengo ni kuwaunganisha kwenye mtandao watu wote wa mjini ndani ya miaka mitatu, hata wale wasio na uwezo wa kununua simu za kisasa, ndiyo maana Tigo ina mpaka utaratibu wa kukopesa simu na mtumiaji akalipa kidogokidogo,” anasema Nchunda na kuongeza kuwa hilo linaenda sambamba na kuweka unafuu wa bei katika huduma.

Nchunda anaongeza kuwa licha ya mtandao huo kuongoza kwa kasi ya intaneti, uwekezaji na uboreshaji unaendelea kila siku, ili kuwa na utayari wa kuwahudumia wateja kadiri ya mahitaji yao.

“Katika nyakati za matumizi ya akili bandia (AI) na roboti mambo yanabadilika sana, ndiyo maana hata kuitabiri miaka 10 ijayo inakuwa si rahisi, lakini sisi tunataka muda wowote wanapohitaji huduma kwetu wakute tupo tayari,” anasema Nchunda.

Ofisa mkuu wa Tigo Business, John Sicilima anasema lengo la idara anayoisimamia ni kuunganisha kila mtu na kila biashara katika uchumi wa kidijitali na hilo anaona linawezekana kama Serikali itapunguza kodi katika vifaa vya kielektroniki, ili kuwawezesha watu kuvinunua kwa wingi.

“Tigo Business ipo kwa ajili ya kusaidia ukuaji wa biashara na kuhakikisha faida inapatikana, ndiyo maana tunakuwa na huduma zinazofaa makundi yote, ikiwemo wajasiriamali wachanga, wadogo, wa kati na wakubwa,” anasema.

Anasema mbali na faiba, kuna huduma za uhifadhi wa data (Data centers), huduma ya kutumia ujumbe kwa wingi, kwa watu wengi (Bulk SMS) lakini pia huduma za miamala ya simu, maarufu kama Tigo Pesa.

Kuhusu mazingira ya uwekezaji nchini, Sicilima anasema Uchumi wa Tanzania na taarifa za kidemografia ni kivutio kikubwa cha kuwekeza katika huduma za kidijitali na kukawa na uhakika wa kupata faida.

“Kasi ya ukuaji wa uchumi ni nzuri, idadi ya watu walio katika umri wa kufanya kazi nayo inavutia, lakini pia kuna amani, ndiyo maana kumekuwa hata na ukuaji mzuri wa kampuni zinazotoa huduma mbalimbali hapa,” anasema Sicilima.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi