Kitaifa
Latra yatangaza nauli treni ya SGR
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra),imetangaza nauli za abiria wa usafiri wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kuwa Sh 31,000 kwa watu wazima na watoto wa kuanzia umri wa miaka 12 kushuka chini wakilipa nusu gharama.
Hata hivyo, kiwango cha nauli kwa usafiri huo ni pungufu kidogo kulinganisha na kinachotozwa na usafiri wa mabasi yanayotoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, kwani mengi yanatoza Sh29,000 hadi Sh35,000 kulingana na aina ya daraja.
Pia taarifa hiyo imetaja nauli kutoka Dodoma hadi Makutupora kwa mtu mzima atalipa Sh37,000 na watoto wenye umri chini ya miaka 12 kushuka chini watalipa Sh18,500.
Nauli hizo zinatangazwa ikiwa ni siku chache zimebaki kabla ya treni hiyo kuanza safari zake rasmi Julai mwaka huu kama ilivyotangazwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Latra iliyotolewa leo Jumatatu Juni 10, 2024 inaeleza nauli hizo zimepitshwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Latra kwa kuzingatia umbali kwa kilomita.
“Nauli hizi ni baada ya kufanyia kazi maombi yaliyoletwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) na wadau wengine,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza masharti mengine ya kuzingatia kabla ya kuanza kutumika kwa nauli hizo ni mtoa huduma (TRC) kuwa na leseni ya usafirishaji.
“Kuwa na ithibati ya usalama wa miundombinu ya reli na mabehewa, kutumia mfumo wa utoaji wa tiketi za kielekroniki, kuunganisha mfumo wa tiketi za kieletroniki na mifumo ya LATRA,” imesema
“Nauli itakayolipwa na mtu mzima na mtoto mwenye umri zaidi ya miaka 12 ni Sh 9.51 kwa kilomita, na mtoto kuanzia kuanzia miaka 4 hadi 12 atalipia Sh34.76 kwa kilomita. Aidha mtoto mwenye umri chini ya miaka minne (4) hatalipa nauli,” imesema