Kitaifa

Matumaini kwa watumiaji mafuta, bei ikiendelea kushuka

Dar es Salaam. Bei ya mafuta inatarajiwa kuendelea kushuka zaidi katika mwezi ujao kutokana na mwenendo wa soko la dunia, Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac) kimeeleza.

Mbali na matarajio ya bei kushuka, lakini bado uhaba wa Dola umeendelea kuwaumiza waagizaji hao, wakiamua kutumia Euro katika uagizaji.

Kauli hiyo ya matumaini imetolewa baada ya Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya ambayo inaonyesha kushuka ikilinganishwa na zile zilizotumika mwezi uliopita.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taomac, Raphael Mgaya alisema mafuta yatakayoingia sokoni Julai bei itakuwa chini.Amesema hilo linatokana na wao kuyanunua kwa bei nafuu katika soko la dunia ikilinganishwa na bei zilizotumika kununua yanayotumika sasa.

“Hata hivyo, bei za mafuta zinazotumika mwezi huu ambazo zimeshuka hazikuakisi hali halisi ya gharama za uingizaji mafuta zilizotumiwa na kampuni. Gharama za ubadilishaji fedha zilizotumiwa na Ewura hazikua sahihi zinampa nafuu mlaji lakini zinamuumiza mwagizaji,” alisema Mgaya.

Wakati mgaya akisema hayo, ripoti ya Ewura inaonyesha bei ya rejareja ya petroli iliyoingia kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa Sh52.72 hadi Sh3,261 kwa lita moja ikilinganishwa na bei ya mwezi uliopita.

Dizeli imeshuka hadi Sh3,112 kutoka Sh3,196 iliyokuwa inatumika mwezi uliopita.

Hata hivyo, pamoja na kushuka bei ya petroli bado kunaifanya kuwa ya juu zaidi katika kipindi cha miezi mitano kati ya Desemba 2023 na Machi 2024.

Ewura imeeleza kupungua bei za mafuta kumetokana na kupungua kwa bei ya mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FBO) kwa wastani wa asilimia 11.82 kwa petroli na asilimia 7.77 kwa dizeli.

“Mabadiliko ya bei yamechangiwa na kupungua kwa gharama za kuagiza mafuta kwa wastani wa asilimia 2.26 kwa petroli na asilimia 8.51 kwa dizeli kwa Bandari ya Dar es Salaam,” ilisema taarifa ya Ewura iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Dk James Mwainyekule.

Taarifa imesema kulikuwa na kupungua kwa wastani wa asilimia 7.07 kwa petroli na asilimia 25.24 kwa dizeli  inayoingia kupitia Bandari ya Tanga na kupungua wastani wa asilimia 12.64 kwa petroli na asilimia 12.61 kwa dizeli kwa Bandari ya Mtwara.

Kwa mujibu wa mtandao wa Treading Economics bei ya mafuta ghafi kwenye soko la dunia katika miezi miwili iliyopita imepungua kwa asilimia 15 hadi Dola za Marekani 73.89 (Sh184,725) Juni 4, ikilinganishwa na Dola 86.63 (Sh216,575) iliyorekodiwa Aprili 5. mwaka huu.

Hata hivyo, wakati bei ya mafuta ikishuka, Mgaya aliliambia gazeti dada la The Citizen kuwa walilazimika kutumia Euro katika kuagiza mafuta badala ya Dola ya Marekani kutokana na upatikanaji wake kuwa wa tabu.

“Zaidi ya theluthi moja ya bidhaa za petroli zilizoagizwa nchini Juni mwaka huu ziliagizwa kutoka nje kwa kutumia Euro. Hili kwa kiasi fulani linaathiri bei ya mafuta nchini,” alisema Mgaya na kuongeza:

“Dola sasa zinapatikana kwa urahisi katika soko lisilo rasmi lakini kwa viwango ambavyo ni ghali zaidi kuliko vilivyo rasmi.”

Akijibu hoja ya Dola, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba,  amesema mfumuko wa bei wa Marekani haujashuka vya kutosha, hivyo riba zao bado ziko juu jambo linaloathiri nchi nyingine, ikiwemo Tanzania.

Hata hivyo, amesema ni vigumu kujua ni fedha gani za kigeni zinazotumiwa na wananchi,  kwa sasa kwa sababu fedha zote zilikuwa kwenye mzunguko ikiwemo Euro na Pauni.

Amewatoa hofu watumiaji wa Dola akisema hali itarejea katika hali ya kawaida hivi karibuni, akieleza kuwa msimu wa mauzo ya nje ya mazao ya asili unatarajiwa kuanza.

Mbali na hilo, amesema  kufunguliwa kwa baadhi ya migodi baada ya mvua kunyesha na kuanza kwa msimu wa utalii ni sababu nyingine za kuanza kupatikana kwa Dola.

“Tunakaribia msimu ambao watalii wengi watawasili nchini, migodi mingi itafunguliwa baada ya mvua na uuzaji wa kahawa na chai nje ya nchi, pamoja na mengine, utaongeza upatikanaji wa Dola nchini,” amesema Tutuba.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi