Kitaifa
Dk Nchimbi ataka kibano kwa watumishi wazembe
Moshi. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameitaka Serikali kuendelea kupambana na kuwachukulia hatua watumishi wa umma wanaotanguliza maslahi yao binafsi badala ya wananchi.
Dk Nchimbi amesema kila mmoja kwenye eneo lake anapaswa kula kiapo cha uaminifu cha kuitumikia nchi kwa uzalendo na hivyo kuchochea maendeleo kwa Taifa.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumatano, Juni 5, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi Kuu ya Mabasi, Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Amesema kazi kubwa imefanyika katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ulioingia madarakani Machi 19, 2021.
“Yapo maeneo machache hatujafanikiwa ambayo yanasababishwa na baadhi ya watumishi wa umma ambao si waaminifu wasiojali maslahi ya wananchi. Serikali iendelee kupambana na watumishi wasiokuwa waaminifu na kila mmoja awe tayari kupambana kwa ajili ya nchi yake,” amesema Dk Nchimbi.
Katika kusisitiza hilo, Dk Nchimbi amesema: “Kila Mtanzania ahisi ana wajibu wa kipekee kuijenga nchi yake na kila mtu mahali alipo aahidi kuitumikia nchi kwa weledi mkubwa.”
Mtendaji mkuu huyo wa CCM, amesema katika siku za karibuni kumekuwa na majaribio ya viongozi, kila chama kinasema kinaweza kuongoza:
“Lakini nasema lazima tuendelee kukubaliana kwamba kwa sasa hakuna chama kinachoweza kuongoza zaidi ya CCM.
“Kuna baadhi ya vyama wanatuhumiana wao kwa wao, hapa (Moshi) mmekaa miaka zaidi ya 20 upinzani, lakini huko mnasikia wanatukanana na kutokana na hilo na wao bado hawajakomaa basi tuendelee kuwatizama na tuwaache wakomae kwanza lakini kwa sasa CCM kiendelee kupewa dhamana ya kuongoza,” amesema.
Dk Nchimbi amesema kila uchaguzi wa miaka mitano nusu yao wanakuwa wapya, wengine wanatoka na kuingia. Anayepata anapata, anayekosa anakosa.
“Kutokuwa kiongozi hakukuondolei wajibu wa kutumikia Watanzania wetu na kila mwananchi kwenye eneo lake atumikie wajibu wake hapo alipo,” amesema Dk Nchimbi.
Walichokisema Rabia, Gavu na Makalla
Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdallah amesema wao kama CCM wamefika kusikiliza kero ili na wao wazipeleke serikalini kwa ajili ya utekelezaji.
Rabia ambaye ni mlezi wa mkoa huo wa Kilimanjaro amesema jana Jumanne, Dk Nchimbi alitoa maelekezo kwa Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda juu ya mikopo kutoka na hilo tayari limeanza kutekelezwa.
“Na hii sasa ndio Serikali inayosikiliza na kutatua kero za wananchi.”
Katika hatua nyingine, Rabia amewaomba Watanzania kwa pamoja kuendelea kumwombea na kumuunga mkono Rais Samia kutokana na jitihada mbalimbali anazozifanya ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha maisha bora yanakuwapo.
“Ziara za Rais kwa mtu mwenye nia safi ya kufuatilia, huwa anakwenda kutafuta fedha za miradi ya maendeleo na ndio maana usiku na mchana anakwenda ili changamoto zinazomkabili Mtanzania yeyote na kwa miaka mitatu hii amegusa maisha ya kila Mtanzania na kwa anayoyafanya sisi CCM tuendelee kumuunga mkono na kumwombea,” amesema Rabia.
Naye Katibu wa Idara ya Oganaizesheni, Issa Ussi Gavu amesema uhai wa chama kuanzia ngazi chini hadi juu ni wanachama na wao hawana shaka katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu watafanya vyema.
“Niwaombe tushikamane, tupendane na maslahi yetu muda wote yawe ya chama na si mtu binafsi,” amesema Gavu.
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amewataka wana Kilimanjaro kuendelea kuwaunga mkono akisema:
“Sumu huwa haionjwi, tulifanya hivyo mwaka 2015 na mwaka 2020 tukarudi kwenye mstari, kwa hiyo tusirudie makosa.”
Awali akimkaribisha Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafii amesema:
“Kwa miaka 25 iliyopita, tulikuwa kama yatima. Lakini sasa mambo yanakwenda vizuri na tunawaomba muendelee kutuunga mkono na kuichagua CCM katika chaguzi zijazo.”
Naye Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo amesema mambo yaliyofanyika ni mengi ikiwemo wiki iliyopita ambapo waliahidi kuangalia eneo la utalii.
Tarimo amesema walikuwa na vipaumbele 10 na kati ya hivyo tisa viko kwenye utekelezaji .
‘’Lakini moja ni kuongeza eneo letu la mipaka ili kulifanya kuwa jiji, ngazi zote zimekwisha kufanyika na tunasubiri kutangazwa tu,’’ amesema na kuongeza:
“Tunaomba Katibu Mkuu hili suala mlibebe. Kwa sababu hata maeneo ya kuzikia yamejaa. Huu ufinyu wa eneo hata Serikali inakutana nao.’’