Kimataifa
Traore kuongeza miaka mitano madarakani
Burkina Faso. Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso inayoongozwa na Kapteni Ibrahim Traoré, imetangaza kuwa itaongeza muda wa utawala wa kijeshi kwa miaka mingine mitano.
Traore ataruhusiwa kugombea katika uchaguzi ujao wa urais, kulingana na shirika la utangazaji linalomilikiwa na Serikali.
Alipoingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 2022, Kapteni Traoré aliahidi kurejesha Serikali ya kiraia kufikia Julai mosi mwaka huu.
Lakini sasa Burkina Faso imejiunga na nchi jirani ya Mali katika kuongeza utawala wa kijeshi.
Hatua hiyo ilitangazwa Jumamosi, baada ya mkutano wa kitaifa wa mashauriano, uliofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Ouagadougou.
Hati iliyorekebishwa, iliyosainiwa na Kapteni Traoré, inasema kwamba kipindi kipya cha mpito cha miezi 60 kitaanza Julai 2, mwaka huu.
“Uchaguzi utakaoashiria mwisho wa mpito unaweza kuandaliwa kabla ya muda huu kuisha, ikiwa hali ya usalama itaruhusu,” shirika la habari la Reuters lilinukuu hati hiyo ikisema.
Burkina Faso imekuwa ikitawaliwa kijeshi tangu Januari 2022, wakati Luteni Kanali Paul-Henri Damiba alipomng’oa madarakani Rais Roch Kaboré.
Kanali Damiba alitetea mapinduzi hayo akisema kuwa Serikali iliyotangulia ilishindwa kukabiliana na ongezeko la vurugu za Waislamu wenye itikadi kali.
Tangu mwaka 2015, waasi wa jihadi wanaohusishwa na Al-Qaeda na kundi la Islamic State walikuwa wakiendesha uasi uliochukua muda mrefu, ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kupoteza mamilioni ya makazi.
Mnamo Septemba 2022, Kapteni Traoré alimng’oa madarakani Kanali Damiba, akisema mapinduzi ya pili yalihitajika kwa sababu kiongozi huyo alishindwa kukabiliana na uasi huo.
Kapteni Traoré aliahidi kuboresha hali mbaya ya usalama wa nchi hiyo ndani ya miezi miwili hadi mitatu, kisha kurejesha utawala wa kiraia ndani ya miezi 21.
Lakini licha ya ahadi hiyo, Kapteni Traoré ameonya kuwa uchaguzi si kipaumbele, utasubiri hadi maeneo yatakaporejeshwa kutoka kwa vikosi vya jihadi ili raia wote wa nchi hiyo waweze kupiga kura.
Chini ya hati mpya, hakutakuwepo utaratibu wa kugawa viti katika Bunge kwa wanachama wa vyama vya jadi, badala yake, uzalendo utakuwa kigezo pekee cha kuchagua wabunge.
Uamuzi wa kuongezwa muda wakati wa mashauriano ya kitaifa ulifanyika haraka na ripoti za vyombo vya habari vya ndani zilionyesha kuwa vyama vya kisiasa havikuwepo mwanzoni mwa mkutano huo.
Nchi hiyo imekuwa ikishutumiwa na mashirika ya utetezi wa haki za binadamu kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika mapambano yake dhidi ya Waislamu wenye itikadi kali, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela na kutoweka kwa nguvu kwa raia kadhaa.
Nchi hiyo iliyokuwa koloni la zamani la Ufaransa, ilipata uhuru mwaka 1960 ikijulikana kama Upper Volta.
Licha ya utaajiri wake wa madini ya dhahabu, nchi hiyo imejikuta kwenye vita na mapinduzi wa kijeshi mara kwa mara, ambayo yamesababisha kusimamishwa uanachama kwenye Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas).
Mwaka 2023, ilifukuza kikosi kidogo cha Ufaransa, ikikata mahusiano ya kijeshi na koloni lake hilo la zamani, ikitaka kuanzisha uhusiano na Russia.