Makala
Wanandoa watofautishe kupendana na kutaka
Kila mtu humpenda mwingine. Vivyo hivyo, anaweza kumtaka au kutakiwa na mwingine. Hakuna asiyejua kupenda ingawa si wote wanaopenda ifaavyo na inavyotakiwa. Muhimu ni kujua kupenda na kutaka ni vitu viwili tofauti. Mfano, unaweza kumpenda mtu kiasi cha kujisikia vibaya usipomuona. Pia, unaweza kumtaka mtu ukadhani unampenda.
Hata hivyo, kupenda kwa namna hii kunaweza kuwa kwa muda au kusikothaminika ikilinganishwa na kupenda mtu kwa kutegemea naye akupende na wote muelewe mnachofanya na kuwa tayari kukigharimia hata kwa maumivu, japo lengo kuu ni amani, furaha na starehe kati ya mengi.
Watu wengi huchukulia kutaka kuwa ni kupenda kwa vile wanachotarajia ni mapenzi yawe na kuwa pamoja au kujihusisha katika ngono. Kupenda kunakolengwa katika ndoa ni kule ambako kuna makusudi maalumu ambapo wahusika hujua wanachofanya kwa malengo fulani, mengi yakiwa ni yale yanayotarajiwa au kuzoeleka kijamii.
Kupenda ni kujitoa muhanga (risk) kwa ajili ya umpendaye. Mfano, wawili wanapopendana na kuamua kufunga ndoa, kwanza, wanatarajia kuishi na kuwa pamoja si kwa muda mfupi, bali wa kudumu.
Pili, kuanzisha familia ambayo huhusisha kutengeneza na kuzaa watoto. Tatu, hulenga katika kuunganisha familia za pande mbili. Katika upendo huu, wahusika hukubaliana kupendana kama walivyo kwa faida sawa ya wote wawili. Hii ni tofauti na kumtaka mtu ukadhani unampenda.
Wengi wanaowataka wawatakao, wakishawapata huwachoka haraka kwa vile walikuwa wakiwataka na siyo kuwapenda.Katika kupenda na kutaka, kutokana na mfumo dume uliotawala duniani, mwanamke anapaswa kuwa makini sana.
Hii ni kwa sababu, asipotofautisha kupendwa na kutakwa, ataishia kujihusisha katika ngono, jambo ambalo linaweza kusababisha mimba, magonjwa ya zinaa, hata kupoteza sifa, hasa uhusiano huu unapojulikana. Wanaume huwa hawapati mimba.
Hivyo, katika uhusiano uhusishao kutaka, na si kupenda, mwanamke anakabiliwa na hatari kubwa ya kuharibikiwa ikilinganishwa na mwanamume. Kwenye ndoa tunaongelea kupendana na siyo kutakana kunakoweza kutafsiriwa vibaya kama kupenda.
Nguzo ya ndoa ni jinsia mbili tofauti kupendana kwelikweli na kwa matendo. Katika kupenda, wawili hujitoa kwa wenzao bila kikwazo wala masharti wakishafunga ndoa. Lugha itumikayo ni kufunga ndoa ikimaanisha, kupoteza haki na uhuru wa kuwapenda wengine. Japo siku hizi wanadamu wameoza kufikia kuongeza aina haramu ya ndoa baina ya watu wa jinsia moja, bado ukweli unabaki palepale kwa maana yake halisi kuwa ndoa ni baina ya mwanamke na mwanamume.
Hii ndiyo siri ya kukithiri kwa mauaji na migogoro hatarishi baina ya wanandoa hata watoto, mfano inapotokea mmoja wa wanandoa akaamua kukatisha uhusiano na maisha yake, ya mwenzake, hata ya watoto.
Hii, mara nyingi, hutokana na kutaka kulipiza kisasi baada ya wahusika kukataa au kushindwa kukubali ukweli kuwa mahusiano yao sasa ni hatarishi na hayawezi kuendelea. Hata hivyo, upendo ukiwa wa kweli na kufanikisha lengo la ndoa, ni kinyume. Wahusika wataridhika, watafurahi, watafanikiwa, wataongeza upendo, na hata kuishi maisha marefu ikilinganishwa na walioharibikiwa au kushinda katika ndoa.
Usawa
Usishangae kukuta mzee wa miaka 50 na kijana wa miaka 30, wakiishi kwa usawa na kuaminiana na kupendana, tofauti hata baina ya wahusika na wazazi wao au wawili wanaolingana kiumri. Hata hivyo, mara nyingi, ni wanaume ambao umri wao huwa hauleti maswali wanapooa wanawake vijana kuliko wao.
Inapotokea mwanamke mzee akaolewa na mwanamume kijana, kunaibuka maswali. Hii ni kutokana na mazoea ya mfumo dume ambao unampendelea mwanamume na kumnyonya mwanamke.
Pia, katika mfumo dume, kuna baadhi ya jamii huwageuza wanawake wanasesere wa wanaume kumilki, kuchezea na kutweza watakavyo.
Hapa ndipo ilipojikita dhana ya wanawake hugeuzwa vitu sawa na vitu vingine.
Huu ni ujinga na ukatili wa kijinsia ambao jamii inapaswa kuuepuka na kuupiga vita. Binadamu wote ni sawa, japo wana majukumu na uwezo tofauti kutokana na maumbile yao. Mfano, mwanamume hawezi kubeba mimba, kunyonyesha wala kuzaa.
Kadhalika, mwanamke hawezi kutungisha mimba. Hivyo, udhalilishaji na unyonyaji wa kijinsia ni matokeo ya ujinga hata ukatili. Ni matokeo ya madaraka yasiyo ya haki, kwa kimombo unfair power dynamics. Kwetu sisi, kutokana na uzoefu wetu, ndoa ni uwanja wa kutendeana haki kwa usawa.
Usipomtendea mwenzako haki, usitegemee akutendee haki, hapa kuna kanuni ya ujibizano (rule of reciprocity).
Katika ndoa sawa na maisha mengine, ni nipe nikupe, ninyime nikunyime, nipende nikupende, nichukie nikuchukie. Huwezi kumpiga mwenzako ukategemea afurahie mateso na maumivu haya.