Kitaifa

Waziri Nape aja na bajeti ya mapinduzi ya kidijitali

Dodoma. Wakati Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetangaza kuleta mapinduzi ya kidijitali, pia imesema itawasilisha bungeni muswada wa sheria ya kuwalinda watoto na mitandao.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ambaye leo Alhamisi, Mei 16, 2024 alipowasilisha bungeni taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025.

Bunge limeidhinisha maombi ya fedha ya wizara hiyo ya Sh180.9 bilioni, kati ya fedha hizo Sh142 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Fedha hizo ni pungufu kwa asilimia 21.95 ukilinganisha na Bajeti iliyotengwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ya Sh212.4 bilioni.

Akifanya majumuisho ya hoja mbalimbali za wabunge, Nape amesema anakubaliana na ushauri wa Mbunge wa wa Buchosa, Eric Shigongo ambaye alishauri umuhimu wa kuwalinda watoto na mitandao kwa lengo la kuwajengea maadili mema.

“Ninakubaliana na hoja ya Eric Shigongo na mimi nimekuwa nikisema mara kwa mara Watanzania, wazazi wa Kitanzania msiwaachie watoto wenu walelewe na mitandao sio salama, tunaharibu kizazi chetu.

“Ndio maana hapa nimesema mwaka huu wa fedha tutakwenda kufanya mapitio ya sheria ya usalama mtandaoni kurekebisha mambo mawili makubwa.

“Moja kuwalinda watoto na mitandao na nitawaomba wabunge, kila mmoja hapa ni mzazi tushirikiane tuwalinde watoto wetu. Hata huko walikoanza wameanza kuzuia watoto wasiingie kwenye mitandao kwa sababu hawako salama,” amesema

Nape amesema: “Jambo la pili tutakalolileta kwenye hiyo sheria ni namna ambavyo mtandao unaweza kutumika kwenye masuala ya ugaidi ili tuilinde nchi yetu. kwa hiyo mabo mawili, usalama wa watoto mtandaoni na ugaidi.”

Awali, Shigongo akichangia mjadala kwenye wizara hiyo alisema waanzilishi wa maendeleo ya teknolojia dunia, Bill Gates na Steve Jobs hawakuruhusu watoto wao kutumia teknolojia kama ya simu, iPad na iPhone.

Shigongo amesema Bill Gates aliwekwa wazi kwamba watoto wake hawalkuruhusiwa kutumia simu hadi watakapofika umri wa miaka 14.

“Nimesimama kuzungumza haya maneno kuwakumbusha wabunge wenzangu juu jukumu tulilonalo la kuwalinda watoto wetu na kizazi kitakachofuata, sisi tulio ndani ya Bunge hili na wengine ni matunda ya wazazi wetu waliwekeza kwetu ndio sisi leo ni Watanzania bora.

“Nasema haya kwa sababu tumewaacha watoto wetu kwenye teknolojia, wanaachwa watoto muda wote wanatumia simu, muda wote wanatumia ipad na wanatengeza uraibu wa vyombo hivi,” amesema.

Shigongo amesema amesoma utafiti unaonyesha uraibu wa kokeni na uraibu wa teknolojia ni vitu vinavyofanana, vyote vinadhibitiwa na homoni ya ‘dopamine.’

Mbunge huyo amewataka wazazi nchini wawajibike kwenye malezi ya watoto wao na kwamba wasiachwe watumie sana sayansi na teknolojia.

“Waruhusu watoto wako watumie sayansi na teknolojia wakati wa kufanya kazi za shule, mama au baba adhibiti simu siyo kila mtoto akilalamika kidogo tu mtoto kanunuliwa iphone 14 unadhani kwamba ni sifa, tunaharibu watoto wetu hatutakuwa na Watanzania bora  siku za kesho,” amesema.

 

Mapidunzi ya kidijitali

Nape akizungumzia mapinduzi ya kidijitali amesema yanaweka msingi wa kulipeleka Taifa kwenye uchumi wa kidijitali unaowezeshwa na kuendeshwa na Tehama.

“Ili kuharakisha Tanzania kuelekea katika uchumi wa kidijitali, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanza kutumika kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na kanuni zake pamoja na uanzishwaji wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi,” amesema

Nape amesema pia Serikali imepitisha mkakati wa kitaifa wa uchumi wa kidijitali 2024-2034 utakaosaidia kuongeza matumizi ya kidijitali kwa huduma zinazotolewa na Serikali pamoja na sekta binafsi.

Amesema pia kutakuwa na mfumo wa Jamii Namba, ambao utatumika kufanya utambuzi wa kipekee wa kila mwananchi kuanzia anapozaliwa ambapo atakuwa na akaunti ya kidijitali itakayomwezesha kupata huduma zote za kijamii.

“Mfumo wa Jamii Malipo, ambao utawezesha wananchi kutumia Jamii Namba kupokea fedha na kurahisisha kufanya malipo kidijitali.

“Mfumo huu pia utasaidia ujumuishi katika huduma za kifedha na kuongeza wigo wa mapato ya Serikali; na Mfumo wa Jamii Data Shirikishi, ambao unamwezesha mwananchi kumiliki taarifa zake katika kupokea huduma mbalimbali nchini,” alisema.

Pia, Nape alisema katika kuhakikisha Tanzania inapiga hatua zaidi katika uchumi wa Kidijitali, Wizara kwa kushirikiana na wadau muhimu inaendelea kuandaa mfumo jumuishi unaojumuisha mifumo mitatu.

Mifumo hiyo ni mwongozo wa kitaifa wa ujumuishaji wa makundi anuai katika huduma za kidijitali ili kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi anaeachwa nyuma katika matumizi ya Tehama.

Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu,  imesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 bajeti ya matumizi ya maendeleo imepungua kwa asilimia 21.95.

Akisoma maoni ya kamati Ally Jumbe ambaye ni mbunge wa Kyela na mjumbe wa kamati, amesema wanaishauri Serikali iwekeze fedha za kutosha katika miradi na kuhakikisha fedha zilizotengwa na Bunge zinafika kwa wakati ili kuwezesha Wizara na taasisi zake kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Amesema kamati imeishauri Serikali kuwa wabunifu wa namna bora ya utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha kuwa, fedha zilizotengwa zitumike kwa malengo yaliyowekwa.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi