Kitaifa
Samia ataja changamoto upatikanaji nishati safi Afrika
“Inasemwa kuwa nishati safi ya kupikia kidunia inapatikana kwa asilimia sita kusini na kati ya Asia na zaidi ya asilimia 14 kwa Amerika ya Kusini na Caribbean.
“Kinyume chake kwa Afrika ambayo ni bara lenye idadi kubwa ya watu na lenye rasilimali zote muhimu, ina kiwango cha chini cha kuwa na nishati hiyo,” amesema Rais Samia.
Amesema zaidi ya Waafrika 900 wanategemea nishati chafu, suala linalochangia uharibifu wa mazingira na upotevu bioanuai.
“Familia nyingi zinapambana kupata nishati safi ya kupikia kutokana na gharama kubwa, kutopatikana kwake na ugavi ulio wa chini.
“Sababu ya pili ni ulimwengu kutotoa kipambele katika utoaji wa fedha za kutosha na kutojali kuwepo kwa fursa za kiuchumi katika uzalishaji wa nishati safi ya kupikia,” amesema Rais Samia.
Ametaja sababu ya tatu kuwa ni kukosekana kwa ushirikishwaji ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya kupikia kwa wote.
Katika kupambana na changamoto hizo, Rais Samia amesema Tanzania imeanzisha programu ya miaka 10 wa nishati safi ya kupikia, inayolenga kuhakikisha asiliamia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Kuhusu mzigo walionao wanawake katika kutafuta nishati safi, amesema Tanzania inahamasisha wanawake, sio tu kutatua changamoto za mazingira na magonjwa, bali pia kuwawezesha kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii.
Ameendelea kutaja mikakati mingine kuwa ni kuendelea kulinda mazingira kwa kuhakikisha mpango ya maendeleo inahusisha vijana kufikia nishati safi ya kupikia.
“Kuongezeka kwa fursa kutawawezesha wanawake kuwapa fursa za uzalishaji kiuchumi na kupambana na vichocheo vya umasikini na kutokuwa na usawa.
“Kwa upande mwingine, kupunguza matumizi ya kuni kama nishati inayotoa moshi wenye sumu kutaokoa maisha na tunaamini hilo litafanikiwa,” amesema Rais Samia.
Amesema Tanzania inajifunza kwa nchi za Brazil, India na Indonesia na Ghana zilizoweka mikakati ya kupata nishati safi.
Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Store amesema mkutano huo ni fursa ya kuokoa vifo vya mamilioni ya watu, kupunguza upotevu wa viumbe hai, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ukuaji wa uchumi.
“Ninapotazama picha ya Afrika, naona baada ya kazi ya hatari ya kupika na kupata moshi, ni kazi ya mwanamke kumlinda mtoto aliyembeba mgongoni ili asipate moshi,” amesema Gahr Store.
Amezitaka nchi wahisani, mashirika na asasi za kiraia kuungana kuchangia upatikanaji wa nishati safi.
“Tuliungana ili kupata chanjo miaka 25 iliyopita na tulisaidia kupunguza vifo vya wanawake na watoto waliokuwa wakifa kwa magonjwa, hivyo sasa tunapaswa kutumia mkakati kama huo,” amesema Gahr Store.
Amesema wamekuwa wakisaidia miradi ya nishati nchi za Uganda, Tanzania, Ethiopia na Msumbji kupitia Benki ya Dunia, AFDB na asasi za kiraia.
“Ninayofuraha kutangaza leo kwamba Norway itawekeza Dola 50 milioni (Sh125.25 bilioni) katika mpango huu. Tuko tayari kuendelea kusaidia mipango huu,” amesema Gahr Store.
Rais wa AfDB, Akinwumi Adesina amesema kuna wanawake bilioni mbili duniani ambao hawapati nishati safi ya kupikia wakitegemea kuni na mkaa kupikia.
“Hawa wanawake hufanya kazi ngumu ya kupika huku wasichana wakikusanya kuni wakitembea kilometa nyingi ili kuhakikisha wanatayarisha chakula cha familia.
“Afrika inapoteza wanawake na watoto 600,000 kila mwaka kutokana na moto wa kuni na mkaa. Kama hatutabadilika watapotea wanawake na watoto milioni sita kwa miaka 10, hili halikubaliki,” amesema Adesina.
Amesema iwapo nishati safi itapatikana itawezesha kuokoa angalau hekta 200 milioni za misitu duniani kote ikiwamo Afrika.
Amezitaka nchi za Afrika kutenga angalau asilimia 5 ya Dola 7 bilioni (Sh17.53 trilioni) zinazowekezwa kila mwaka kwa ajili ya upatikanaji wa nishati safi barani humo.
“Hivyo ninayo furaha kutangaza kuwa AfDB itatoa Dola 2 bilioni (Sh5.01 trilioni) kwa ajili ya nishati safi ya kupikia kwa miaka 10 ijayo,” amesema Adesina.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), Tedros Ghebreyesus amesema wanakadiria kila mwaka watu milioni 3.2 wanakufa kutokana na moto wa moshi nyambani unaozalishwa na moto wa kupikia.
“Pia, robo ya idadi ya watu duniani inayoathiriwa na moshi wa mkaa, kuni na mabaki ya mazao kama vyanzo vya nishati. Wanawake na watoto katika jamii masikini ndio waathirika wakubwa,” amesema Adesina.
Mkutano huo umehudhuriwa na baadhi ya marais wa Afrika, mawaziri na watendaji wa Serikali mbaimbali duniani.