Connect with us

Kitaifa

SADC yazindua kanzidata ya dawa SMD

Dar es Salaam. Kanzi data ya dawa kwa ajili ya nchi wanachama wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC), Med Database SMD imeanzishwa ili kusaidia kila nchi kupata taarifa ya bei ya bidhaa za afya wakati wa kufanya ununuzi.

Hatua hiyo imefuata baada ya mawaziri wa afya wa SADC, kuridhia taarifa ya mshauri mwelekezi juu ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa pamoja wa bidhaa za afya Novemba 29, 2023 nchini Angola.

Kanzidata hiyo iliyozinduliwa leo Jumanne, Mei 14, 2024 na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Dk John Jingu imeelezwa kuwa ni muhimu kwa nchi wanachama kwa ajili ya kubadilishana taarifa muhimu zinazohusu ununuzi wa bidhaa za afya kwa pamoja (SPPS).

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amesema ununuzi huo wa pamoja utaongeza ufanisi.

Amesema uzinduzi huo ulitanguliwa na mafunzo ya matumizi kanzi data hiyo kwa wakurugenzi wa Bohari za Dawa na wakurugenzi wanaoshughulika na uhifadhi na takwimu za ununuzi wa bidhaa za afya kutoka nchi wanachama ili kuweza kuelewa namna kanzi data hiyo inavyofanya kazi.

Mavere amesema kanzidata hiyo itaweza kutunza taarifa ya bidhaa za afya kwa nchi za SADC na kila nchi itakuwa na taarifa zake zinazohusiana na bidhaa inayohusika na bei ilivyo katika mfumo huo wa ununuzi wa pamoja.

“Tulipewa jukumu na SADC, katika utekelezaji wake kulikuwa na vitu vingi. Mfumo ulikuwa haujakaa sawa kwani uliotumika awali haukuweka mazingatio makubwa kwenye maeneo muhimu ikiwamo sheria za ununuzi, fedha, kudhibiti ubora, usajili wa bidhaa katika nchi husika na mfumo wa malipo kati ya mnunuaji na muuzaji.

“Pia, kulikuwa na masuala masuala ya kikodi, unapokuwa na vitu kama hivyo ambavyo bado havijakaa sawa tuliamua kufanya mapitio na kuja kanzidata hii,” amesema.

Amesema kufuatia hilo walikuja na mambo matano ikiwamo namna ya kubadilisha kitengo cha ununuzi wa SADC kijitegemee na kwamba ifikapo Julai mpaka Agosti wanatarajia kupata vibali ili kuanza hatua za utekelezaji.

“Mfumo umeanza, lakini oda ya kwanza itakuwa lini ni mpaka tupate kibali,” amesema Mavere.

Awali, akizindua mfumo huo, Dk Jingu amesema katika mfumo huo mhusika ataweza kuona ni vifaa vipi vinavyopatikana wapi, muda wake wa kuishi ni upi na kama ana uhitaji ni nyenzo muhimu kuitumia katika kulinda afya za watu.

Dk Jingu amesema hiyo ni hatua moja muhimu katika kuhakikisha mashirikiano yanakuzwa katika nchi za SADC lakini kutekeleza kile viongozi wa nchi hizo walikubaliana kuwa na manunuzi ya pamoja.

“Tukienda kununua kwa pamoja tutapata kwa bei nzuri zaidi  na kuvutia hata wawekezaji kwenye viwanda vya dawa na vifaa tiba,” amesema.

Ameongeza kuwa viwanda vya ndani pia vitanufaika kwa kuwa soko la bidhaa wanazozalisha litakuwa rahisi.

“Tanzania kama mmoja wa nchi za SADC tumekua vinara kuhimiza ushirikiano hasa ununuzi wa pomoja, huduma hii itapatikana mitandaoni kwenye simu na kompyuta na wafanyabiashara wa viwanda watanufaika,” amesema Dk Jingu.

Ofisa mwandamizi wa sekretariet ya SADC kitengo cha ugavi, Malicious Tutalife amesema kanda ya SADC imeweka mkazo katika uanzishaji wa viwanda na ushirikiano wa kikanda.

Amesema katikati ya mwaka 2019, sektarieti ya SADC na Umoja wa Ulaya walitia saini makubaliano ya uchangiaji ili kuanza utekelezaji wa program inayoitwa ‘Mpango wa Msaada wa Maendeleo ya Viwanda na Sekta za Uzalishaji’, unaojulikana pia kama SIP.

Kwa mujibu wa Tutalife, mpango wa SIP ulibuniwa kusaidia mafanikio ya ajenda ya kikanda ya uanzishaji viwanda na utengamano, kwa kuzingatia kuboresha utendaji.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi