Kitaifa
Chanjo ya R21 kuleta mabadiliko vita dhidi ya Malaria Kusini mwa Jangwa la Sahara
Tunapoadhimisha Siku ya Malaria Duniani, sekta ya afya duniani inashuhudia maendeleo makubwa katika vita dhidi ya ugonjwa huo, hasa katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara eneo ambalo linabeba mzigo mkubwa zaidi wa ugonjwa huu hatari.
Kiini cha maendeleo haya ni kugunduliwa kwa chanjo ya R21/Matrix-M™, iliyotengenezwa kwa juhudi za ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Oxford na Taasisi ya Serum ya India, ikiwa ni uboreshaji kutoka kampuni ya Novavax’s Matrix-M™.
Chanjo hii ni zana yenye nguvu, inayoongeza kwa kiasi kikubwa mwitikio wa kinga mwilini na kuonyesha ufanisi mkubwa, katika maeneo yanayokabiliwa na maambukizi makali ya malaria.
Ubunifu kupitia ushirikiano
Uundaji wa chanjo ya R21/Matrix-M™ unawakilisha kilele cha ushirikiano wa kimataifa na mafanikio ya kisayansi. Ushirikiano huo ulichanganya utaalamu wa kina wa Chuo Kikuu cha Oxford katika utafiti wa chanjo na Taasisi ya Serum, inayoongoza kwa uzalishaji wa chanjo India. Novavax ilichangia teknolojia yake ya ubunifu ya adjuvant ambayo ni muhimu katika kuimarisha mwitikio wa kinga.
Muungano huu umetoa chanjo ambayo sio tu kwamba inakidhi viwango vya ufanisi na usalama, lakini pia inatoa ahadi ya kupatikana kwa bei nafuu katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Ufanisi na matokeo
Dk Ally Olotu, Mchunguzi Mkuu na Mkurugenzi wa Sayansi katika Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), akizungumzia matokeo ya chanjo hiyo amesema;
“Kufikia kiwango cha ufanisi cha asilimia 77 katika majaribio ya awamu ya pili, chanjo ya R21/Matrix-M™ imeonyesha uboreshaji mkubwa katika chanjo ya awali ya RTS,S/AS01 ambayo ilionyesha ufanisi wa takriban asilimia 56 hapo awali, hii inatoa matumaini mapya na ulinzi kwa makundi yaliyo hatarini zaidi katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.”
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeidhinisha chanjo ya R21/Matrix-M™ kwa ajili ya kuzuia Malaria kwa watoto wanaoishi katika maeneo yenye maambukizi makubwa.
Uamuzi huu ulifuatia matokeo ya majaribio yaliyoonyesha ufanisi wa asilimia 75 katika maeneo yenye maambukizi makubwa na asilimia 68 katika mikoa yenye uwepo wa malaria kwa muda mrefu. Wasifu wa usalama wa chanjo wenye athari ndogo, unasisitiza uwezekano wake wa kutumika kwa kiwango kikubwa.
Maoni ya wataalamu wa afya
Huku dunia ikisherehekea maendeleo ya karibuni katika vita dhidi ya Malaria, sauti za watu muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu hatari, zinatoa matumaini juu ya matokeo ya ugunduzi huu. Dk Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, alielezea faida kubwa za chanjo ya R21/Matrix-M™, akisema, “Kuidhinishwa kwa chanjo ya R21/Matrix-M™ kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa pengo kati ya mahitaji na usambazaji, kuimarisha mikakati yetu ya kuzuia malaria na uwezekano wa kuokoa mamia na maelfu ya maisha ya vijana barani Afrika.”
Akitoa maoni yake wakati wa mahojiano maalumu, Dk Olotu alieleza juu ya uidhinishaji wa chanjo uliofanywa na WHO. “Uidhinishaji wa WHO ni hatua muhimu katika afya ya umma. Uwezo wa chanjo hii kupunguza kasi ya viwango vya Malaria unaweza kubadilisha hali ya kuzuia malaria, sio tu Tanzania, bali kimataifa.” Mapendekezo haya yanasisitiza uwezo wa chanjo ya R21 kubadilisha mbinu ya kuzuia malaria na kutoa mwanga wa matumaini kwa maeneo yaliyoathirika zaidi na ugonjwa huo.
Aidha, Machi 26, 2024, Taasisi ya Afya Ifakara ilishiriki katika kikao cha tatu cha Baraza la End Malaria jijini Dar es Salaam, ambapo Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alitoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za kukabiliana na Malaria nchini. Kikwete alisifu nafasi ya Taasisi ya Ifakara katika utengenezaji wa chanjo na kusisitiza umuhimu mkubwa wa chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano ambao wako katika hatari zaidi.
Chanjo ya R21, imeonyesha ufanisi wa kutegemewa katika majaribio ya kliniki, ikiimarisha zaidi mapambano dhidi ya Malaria kwa kuongeza zana zaidi katika orodha ya afua zilipo ikiwemo vyandarua.
Kuongeza kiwango cha usambazaji ulimwenguni
Taasisi ya Serum ya India imejitolea kuzalisha hadi dozi milioni 200 kila mwaka, kuhakikisha upatikanaji wa chanjo hiyo ili kukidhi mahitaji ya kimataifa. Kiwango hiki cha uzalishaji ni muhimu kwa ajili ya kushughulikia mahitaji ya dharura ya maeneo yenye malaria. GAVI, ina jukumu muhimu katika juhudi hii kwa kuwezesha ufadhili na usambazaji wa chanjo katika nchi za kipato cha chini na kuhakikisha upatikanaji sawa. Dk Olotu anasisitiza uharaka wa utoaji wa chanjo hiyo kwa kusema kuwa “Tuna matumaini kwamba mchakato huu utahitimishwa haraka ili kutoa ufikiaji wa chanjo hii ya kuokoa maisha kwa watoto ambao wako katika hatari zaidi.”
Taasisi ya Afya Ifakara iko mstari wa mbele
Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) imekuwa sehemu muhimu katika tathmini ya kitabibu ya chanjo ya R21/Matrix-M™. Ushiriki wa taasisi hiyo ni muhimu katika utekelezaji na uendeshaji wa majaribio, ambayo yanazingatia viwango vya kitabibu vya kimataifa huku yakizingatia maudhui ya ndani.
Dk Olotu aliongoza timu ya wataalamu kupitia majaribio ya awamu ya tatu ya chanjo hiyo, akishirikiana na taasisi kama vile Imperial College London na washirika wengine katika mabara kadhaa. Ushirikiano huu umekuwa muhimu katika kutathmini utendaji kazi wa chanjo katika mazingira tofauti ya magonjwa na kutoa maarifa muhimu ambayo yanagusa mikakati ya afya ya kimataifa.
Majaribio ya kitabibu na matokeo yake kwa jamii ya Kitanzania
Majaribio ya kitabibu yaliyofanywa katika vijiji vya Kiwangwa na Miono katika Mkoa wa Pwani na Taasisi ya Afya Ifakara, yamekuwa muhimu. Maeneo haya yaliyochaguliwa kwa viwango vyao vya maambukizi ya Malaria, yametoa taswira ya ufanisi wa chanjo katika mazingira tofauti. Zaidi ya watoto 600 wenye umri wa miezi 6-36 walishiriki, ikionyesha idadi ya watu walio katika hatari zaidi.
Dk Honorati Masanja, Mkurugenzi Mkuu wa IHI anabainisha kuwa, “Hili ni tukio la kihistoria kwa Ifakara, Tanzania na jamii ya kimataifa. Jukumu la taasisi yetu katika majaribio haya linasisitiza dhamira yetu ya kupambana na malaria kupitia utafiti na uvumbuzi wa msingi.”
Safari ya kutokomeza Malaria
Kutolewa kwa mafanikio kwa chanjo ya R21 kunaashiria wakati wa mabadiliko katika afya ya umma Tanzania na nchi kama Ghana ambapo Malaria inasalia kuwa changamoto kubwa ya kiafya. Muingiliano wa chanjo hii katika programu zilizopo za kudhibiti Malaria kunaweza kongeza juhudi za kuboresha afya ya umma, uwezekano wa kuzuia mamilioni ya visa vya Malaria na kupunguza mzigo mkubwa ambao ugonjwa huu unaweka kwa jamii.
Msimamo wa Ghana wa kuwa nchi ya kwanza kuidhinisha chanjo ya R21 unatoa funzo kwa mataifa mengine. Maendeleo haya muhimu yanaangazia umuhimu wa mamlaka za afya za kitaifa katika kupitisha suluhu bunifu za kupambana na kutokomeza ugonjwa huu hatari.
Njia ya kusonga mbele inahusisha sio tu kuendelea kwa usambazaji wa chanjo lakini pia ujumuishaji wa zana hizi mpya katika mikakati mipana ya kudhibiti Malaria. Kwa kushughulikia changamoto za kiufundi, kuimarisha imani ya jamii na kuhakikisha utafiti na ufuatiliaji endelevu, jamii ya afya duniani inaweza kupiga hatua kubwa kuelekea kutokomeza mojawapo ya magonjwa hatari zaidi duniani.
Kuhusu Taasisi ya Afya Ifakara (IHI)
Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) au kwa kifupi Ifakara, ni shirika linaloongoza la utafiti wa afya barani Afrika lenye rekodi nzuri ya kuendeleza, kupima na kuthibitisha ubunifu wa afya.
Taasisi hii inaendeshwa na maeneo ya kimkakati ya utafiti, mafunzo na huduma. Ifakara inajumuisha taaluma mbalimbali za kisayansi, kuanzia sayansi ya msingi ya matibabu na ikolojia hadi majaribio ya kimatibabu, utafiti wa mifumo ya afya, tafsiri ya sera na utekelezaji wa programu za afya.
Mwelekeo wa kimkakati wa Ifakara
Ifakara inatazamia kuwa na watu wenye afya njema na waliowezeshwa kupata huduma za afya na masuluhisho yanayothibitika. Taasisi hii inajidhatiti kufikia dira ya kuwa kituo cha umahiri katika utoaji wa huduma bora za afya kwa ushirikiano kupitia utafiti, uvumbuzi, uimarishaji wa uwezo na utekelezaji wa programu.
Kazi za Ifakara katika mkakati wake wa miaka mitano (2023-2028) zinalenga katika kutoa masuluhisho ya msingi kwa ajili ya kushughulikia mahitaji na changamoto za jamii, tafsiri ya sera na maarifa ili kuziba pengo kati ya utafiti na sera, uwezeshaji wa jamii ili kuwezesha ushirikiano, kufanya maamuzi ya pamoja na kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taasisi ili kuinua ubora katika utafiti na utekelezaji wa programu kwa madhumuni ya kubadilisha maisha ya watu.
Zaidi ya miaka 60 ya kuboresha afya ya jamii
Ziara ya Ifakara ya mtaalamu wa wanyama wa Uswizi Prof. Rudolf Geigy mwaka wa 1949 iliashiria mwanzo wa historia ya zaidi ya miaka 60 ya Ifakara. Geigy [1920-1995] alitafuta eneo kwa ajili ya kutafiti magonjwa ya kitropiki. Miaka minane baadaye, alifungua Maabara ya Taasisi ya Tropiki ya Uswizi (STIFL).
Jina “Ifakara” linamaanisha “mahali unapoenda kufa”, kielelezo cha mzigo mkubwa wa kihistoria wa magonjwa katika eneo hilo kabla ya juhudi kubwa za kudhibiti kuanza. Katika miaka ya baada ya uhuru, STIFL ilitekeleza jukumu la kutoa mafunzo kwa maafisa wa matibabu ambao wangeweza kutumikia nchi baada ya Uhuru. Serikali ya Tanzania iliiagiza STIFL kutekeleza jukumu hilo.
Mwaka 1996, Ifakara ilibadilishwa jina na kuitwa ‘Ifakara Health Research and Development Center (IHRDC). Jina hili lilidumu hadi mwaka 2008 ambapo lilibadilishwa tena na kuwa Taasisi ya Afya ya Ifakara. Uongozi imara wa wakurugenzi wa sayansi wa Tanzania tangu 1993, kama vile Dk. Andrew Kitua na warithi wake, uliifanya IHI kusifiwa kimataifa.
Upanuzi uliendelea kwa kufunguliwa kwa tawi jipya la Bagamoyo mwaka 2005 na maendeleo makubwa ya miundombinu yaliyofanyika mwaka 2012 kwa kuanzishwa kwa Kituo cha Mafunzo na Kituo cha Majaribio ya Kliniki. Dk. Honorati Masanja, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa sasa, aliteuliwa mwaka 2016.