Uncategorized
Suala la malipo wastaafu iliyokuwa Jumuiya Afrika Mashariki laibuka upya
Dodoma. Wakati kukiwa na kauli tofauti za Serikali kuhusu madai ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwamba hawaidai Serikali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kama wapo wanaodai wawasilishe madai kwa mwajiri wao.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi ya Mei 2, 2024 na Majaliwa alipojibu maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
Kauli hiyo imefuatia swali la Hawa Mwaifunga, mbunge wa viti maalumu, aliyeuliza swali akitaka kujua Serikali inatoa kauli gani juu ya malipo ya wastaafu hao ili waweze kupata haki zao kama zipo.
Mwaifunga ameuliza swali hilo kwa mara ya pili katika Bunge hili, mara ya kwanza aliuliza vivyo hivyo, kwamba Serikali ina mpango gani wa kuwalipa wastaafu wa jumuiya hiyo.
Majibu ya Serikali yalitolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe na kumfanya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kutoa kauli kuwa ni vyema Serikali ikatoa taarifa rasmi kwa wastaafu hao, kuwa walishalipwa fedha na hakuna malipo mengine.
Hata hivyo, leo Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuna Watanzania walifanya kazi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Baada ya kuvunjika kwa jumuiya hiyo wako ambao walikuwa wanadai haki zao za utumishi. Ofisi yangu na ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje tumekuwa tukipokea malalamiko haya na tumekuwa tukiyafanyia kazi kwa kuwaelekeza waende kwa mwajiri wao,” amesema.
“Kumbukumbu tulizonazo wapo waliowasilisha madai na nyaraka wameshalipwa. Sasa kwa kuwa mbunge (Mwaifunga) anahitaji kujua hao wanaohangaika, ambao bado hawajapewa haki zao na kwa kuwa Serikali yetu inasimamia haki ya kila aliyetenda kazi yake, basi kama wapo wawasilishe madai kwa mwajiri wao ili tathmini iweze kufanywa na kama haki ipo watapewa haki zao,” amesema.
Agizo la Spika
Agizo la Spika kuitaka Serikali kutoa tamko, lilitokana na majibu ya Kigahe kuwa, madai ya wastaafu hao yalishafanyiwa kazi kuanzia Julai 2006 hadi Novemba 2013 walipoyafunga rasmi.
Spika Tulia alisema kama hivyo ndivyo, ni vyema wastaafu hao wakapewa taarifa rasmi kwani wengine hawajui hilo, hivyo wanaendela kuhangaika kwa kufuatilia madai hayo na wapo maeneo mbalimbali nchini.
Alisema taarifa wanaweza kupatiwa hadi ngazi ya wilaya ili kuwafanya wasiendelee kufuatilia, wakiamini watalipwa.
Swali kama hilo pia liliwahi kuulizwa bungeni na mbunge wa Viti Maalumu, Susan Mgonokulimaaliyetaka kujua kama Serikali imeshalipa stahiki za wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika Juni 1977.
Waziri wa Fedha na Mipango (kwa wakati huo), Dk Philip Mpango alisema Serikali ilishalipa stahiki za wastaafu.
Dk Mpango alisema kati ya mwaka 2005 na 2010, Serikali iliwalipa wastaafu 31,519 kati ya 31,831 ambao walilipwa jumla ya Sh115.3 bilioni.
Alisema waliolipwa ni wale waliojitokeza na kuthibitishwa na waliokuwa waajiri wao.
“Katika kipindi cha 2011 – 2013 Serikali iliendelea kuwalipa wale ambao walikuwa hawajalipwa ambapo wastaafu 269 walilipwa Sh1.58 bilioni na kufanya jumla ya waliolipwa kufikia 31,788, hivyo kiasi kilicholipwa kufikia Sh116.88 bilioni,” alisema Dk Mpango ambaye sasa ni makamu wa Rais.
Alisema upokeaji madai mapya ulisitishwa Desemba 31, 2013 kwa mujibu wa makubaliano kati ya wawakilishi wa wastaafu na wanasheria wao kwa upande mmoja na Serikali kwa upande wa pili.
Baada ya majibu hayo, Faida Bakari katika swali la nyongeza, alisema si kweli kwamba wazee walilipwa wote na ana ushahidi, hivyo akahoji kwa nini Serikali ifunge suala hilo, ndipo Mwanasheria Mkuu wa Serikali akajibu kwamba suala hilo limekwisha na hawana popote pa kwenda.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju (kwa wakati huo) alisema wastaafu hao hawawezi kupata chochote na hawawezi kwenda mahakama yoyote.
Masaju alisema Mahakama ya Rufaa ilishamaliza kazi yake, hivyo hakuna tena mlango wa wastaafu hao kupitia.
Alisema wakati Serikali ikimaliza kulipa madeni kwa wastaafu hao, wapo wengine ambao walifungua kesi namba 73/2015 kwenye Mahakama ya Rufaa, maombi ambayo yalitupiliwa mbali, hivyo hawana mahali pengine pa kukimbilia.
Desemba 20, 2019 taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Fedha na Mipango, ilitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya wastaafu hao iliyoandikwa kwenye gazeti moja (si Mwananchi).
Taarifa hiyo ilisema Wizara ya Fedha na Mipango inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyoandikwa kwenye gazeti yenye kichwa cha habari “Wastaafu EAC waibuka na mafao yao” taarifa hiyo ilieleza wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki hawajalipwa mafao yao kwa miaka 40 iliyopita.
“Wizara ya Fedha na Mipango inapenda kuufahamisha umma kuwa imekwishawalipa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mujibu wa “Hati ya Makubaliano” (Deed of Settlement) iliyosajiliwa Mahakama Kuu Septemba 21, 2005, kati ya Serikali na watumishi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hati ya Makubaliano ilibainisha wazi mambo yafuatayo:
“Wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walikubali kufuta madai yao yote yaliyokuwa katika Kesi Na. 95 ya mwaka 2003, waliyoifungua Mahakama Kuu ya Tanzania;
“Serikali ilikubali kuwalipa wadai wote waliokuwa wamefungua kesi mahakamani na wengine wote waliofanya kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla ya Juni 30, 1977, na baada ya malipo hayo kufanyika, Serikali isingedaiwa tena;
Serikali ilikubali kuwalipa wastaafu 31,831 jumla ya Sh117 bilioni kwa misingi ya stahili ya kila mmoja kulingana na taarifa ya kila mmoja wao kwenye jalada au nyaraka nyingine zilizothibitishwa. Serikali ilikubali kuchukua gharama za mawakili wa wadai ili malipo wanayolipwa wastaafu hao yasikatwe chochote.
Ulipaji mafao kwa ujumla ulikamilishwa mwaka 2009/2010 na Serikali iliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuendelea kushughulikia madai halali yatakayojitokeza, hususan yale yanayohusu mirathi kwa wahusika katika zoezi hili kwa kutumia sheria na taratibu zilizotumika katika shughuli husika.
Hadi Desemba 2013 jumla ya wastaafu 31,788 kati ya 31,831, walikwishalipwa kiasi cha Sh116.880 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 99.9 ya fedha zote zilizokubalika kulipwa.
Kwa maelezo haya Serikali kwa mara nyingine tena inarejea kusisitiza kuwa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamelipwa haki zao zote kwa mujibu wa sheria na inatoa wito kwa wastaafu wote wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kukubali kuwa malipo yaliyolipwa baada ya uhakiki ni halali kwa mujibu wa sheria.
Serikali inawasihi sana wazee wetu hawa kujiepusha na upotoshaji na udanganyifu kutoka kwa wajanja wachache wanaotaka kujinufaisha kupitia migongo yao kwa kuendelea kujidai kwamba wao wana uwezo wa kusimamia madai yao ambayo hayapo.