Connect with us

Kitaifa

Biteko akatiza mapumziko ya Pasaka ya vigogo kushughulikia umeme

Dar es Salaam. Wakati Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likitaja chanzo cha hitilafu kwenye Gridi ya Taifa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto  Biteko ameelekeza viongozi wote wa wizara, Tanesco na wafanyakazi wote waliopo kwenye mapumziko ya Pasaka warejee kazini haraka kushugulikia tatizo hilo.

Dk Biteko ambaye pia yupo njiani kuelekea kwenye Kituo cha Kidatu kuona jitihada zinazoendelea kufanywa ili kurudisha nishati hiyo katika hali ya kawaida, ameelekeza wafanyakazi hao kurudi kazini kuanzia muda wa tatizo lilipojitokeza, usiku wa kuamkia leo Aprili mosi, 2024, huku akisisitiza wahakikishe umeme unarejea kwenye maeneo yote nchini.

Agizo hilo limekuja wakati tanesco ikifafanua kuwa tatizo limetokana na hitilafu kwenye mfumo wa kudhibiti kiwango cha maji kwenye mitambo ya kufua umeme ya Kidatu.

 

Saa 8:22 usiku leo, Tanesco ilitoa taarifa kupi ikieleza kuwepo hitilafu kwenye gridi ya Taifa iliyosababisha maeneo mengi nchini kukosa umeme.

Baadaye saa 6 mchana shirika hilo limetoa taarifa ya pili likibainisha chanzo cha tatizo hilo kwenye mitambo ya Kidatu, hali iliyosababisha kushindwa kuzuia mtiririko mkubwa wa maji yanayoingia kwenye mitambo hiyo.

“Hitilafu hiyo ilisababisha mitambo kujizima kwa ghafla ili kujilinda. Kwa sasa (saa 6 mchana) mitambo ya kudhibiti uingizaji wa maji kwenye kituo cha Kidatu iliyopata hitilafu tayari imebadilishwa na kufungwa nyingine, na kazi ya kutoa maji yaliyoingia kwenye vyumba vya kuendesha mitambo inaendelea, pamoja na kuanza taratibu za kuwasha mitambo ya kufua umeme,” imeeleza taarifa hiyo.

Kufuatia hitilafu hiyo mikoa ikiwemo Iringa, Tanga, Pemba, Unguja na baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam na Pwani ilikosa umeme, na mchana huu inaelezwa imeanza kupokea umeme kupitia mitambo ya Pangani na Ubungo Namba Mbili huku taratibu za kimfumo za kurejesha umeme kwenye maeneo yote zikiendelea.

“Shirika linaendelea kuwaomba uvumilivu wateja wake wote katika kipindi hiki ambacho Nishati ya Umeme inakosekana,” imeeleza taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi