Kitaifa

Force Account bado ni changamoto

Dodoma.Tasisisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imebaini mianya minane katika matumizi ya mfumo wa Force account (mradi unaotekeleza bila zabuni) kwenye utekelezaji wa miradi ikiwamo kutokuwepo mfumo thabiti wa weledi na taaluma.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni  amesema hayo jana wakati wa kukabidhi taarifa yake ya mwaka 2022/23 kwa Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.

Amesema walifanya tathimini ya matumizi ya force account katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi iliyofanyika kutokana  na uwepo wa changamoto ya utekelezaji wa miradi kwa njia ya Force account.

Amezitaja changamoto hizo ni baadhi ya miradi iliyotekelezwa chini ya mfumo huo kuwa chini ya viwango, gharama kubwa na kutozingatia taratibu za ununuzi.

Hamduni amesema kwa jumla uchambuzi huo ulibaini mianya mbalimbali ikiwamo baadhi ya watendaji waliokuwa wakisimamia force account kutokuwa na uelewa au kuwa na uelewa mdogo kuhusu taratibu za ununuzi.

Mengine waliyobaini ni ukiukwaji wa sheria na miongozo wakati wa kuunda kamati za usimamizi, ukiukwaji wa sheria wakati wa usimamizi wa miradi, kutokuwepo kwa mfumo thabiti wa weledi na taaluma katika utekelezaji wa miradi inayotekelezwa bila zabuni.

“Uchambuzi ulibaini upungufu wa wataalamu, ukosefu wa fedha za usimamizi, ufinyu wa muda wa utekelezaji wa miradi na kutokuwepo kwa ukomo wa matumizi ya njia ya force account,”amesema.

Amesema ili kuondokana na changamoto hizo, Takukuru ilikabidhi mapendekezo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Hamduni amesema mapendekezo mengine waliyoyakabidhi ni kutoa elimu ya mara kwa mara ya matumizi ya mfumo huo, kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya matumizi ya njia ya mfumo huo.

Amesema pia walishauri kuwekwa kwa ukomo wa gharama za miradi inayotekelezwa bila zabuni, makisio ya miradi kuendana na sifa za kijiografia za eneo husika ili kuimarisha usimamizi pamoja na wataalam kutumika katika maeneo hayo.

Amesema baadhi ya maeneo yaliyowasilishwa kwa PPRA yamezingatiwa katika Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma yaliyofanyika hivi karibuni.

 

LAAC nayo yaona changamoto

Katika mkutano wa 14 wa Bunge la 12, uliomalizika Februari mwaka huu, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilianisha uwepo wa changamoto katika utekelezaji wa miradi inayotekelezwa bila kufuata mfumo wa zabuni.

Changamoto hizo ni ukiukwaji wa mwongozo wa matumizi ya Force account na kamati za usimamizi wa miradi kutoundwa au kutofanya kazi kikamilifu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Halima Mdee amesema walibaini pia viashiria vya miradi iliyotekelezwa kwa njia ya Force account kutoishi kwa kipindi cha muda mrefu na mingine kushindwa kukamilika kwa wakati uliopangwa.

“Bunge linaazimia kwamba, Serikali ichukue hatua stahiki kwa watendaji wote waliokiuka Mwongozo wa utekelezaji wa miradi isiyofuata mfumo wa zabuni,”amesema Mdee.

Alipendekeza Serikali ifanye tathimini ya miradi iliyotekelezwa kwa kutumia mfumo huo  na kukokotoa gharama za uchakavu wa miradi hiyo na kuchukua hatua kwa watendaji wote watakaobainika kutekeleza miradi chini ya viwango.

Haya yataongeza ufanisi

Akizungumza na Mwananchi Digital  Ijumaa Machi 29,2024, Mhadhiri katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) jijini Dar es Salaam, Dk Nasibu Mramba ameshauri Serikali kufanyia kazi changamoto zilizoonekana wakati wa utekelezaji wa mfumo huo.

“Ni watu wanaosimamia wasiwe na uroho (wa fedha) zinafanikiwa sisi tuna kampasi ya Mbeya majengo yake yako vizuri sana yamejengwa kwa Force Account. Watu wanaofika pale wanasema yamejengwa kwa Sh5 bilioni lakini yamejengwa kwa Sh1.6 bilioni kwa sababu kulikuwa na usimamizi,”amesema.

Amesema ili kutekeleza kwa ufanisi miradi ya aina hiyo kunahitajika vitu viwili ambavyo ni aina ya mkandarasi na usimamizi mzuri wa mradi ambao utahusisha wataalam.

“Force account inafanya kazi nzuri sana lakini uwe na wasimamizi wazuri na mafundi wazuri, je wanapatikana kila mahali? Kwa hiyo mimi nafikiria kuwa isiondolewe kila mahali bali inatakiwa ifanyiwe ukomo,”amesema.

Amesema kutokana na changamoto zilizoonekana Serikali itengeneze mwongozo ambao utaufanya mfumo huo ufanye kazi vizuri zaidi na uwepo wa orodha maalumu ambayo atakayetimiza ndiye atakayeruhusiwa kwenda kwenye mfumo huo.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi