Kitaifa
Sababu matukio ya ukatili kuongezeka Zanzibar
Dar es Salaam. Malezi duni ya watoto yanayofanywa na wazazi, kukosa elimu ya kujitambua na umasikini vinatajwa na wadau kuwa sababu ya kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji, visiwani Zanzibar.
Matukio hayo yameongezeka kwa asilimia 5.06 kutoka 162 yaliyoripotiwa Desemba, 2023 hadi kufikia 171 Januari mwaka huu.
Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) iliyochapishwa katika tovuti yao hivi karibuni, ambayo pia inaonyesha katika matukio yaliyoripotiwa ubakaji unaongoza kwa matukio 89.
Hata hivyo, katika ripoti ya mwaka hadi mwaka inaeleza, matukio yaliyokuwapo Januari mwaka huu yamepungua kwa asilimia 1.2 ikilinganishwa na 173 yaliyoripotiwa Januari, 2023.
Asilimia 87.7 matukio hayo ya unyanyasaji wa kijinsia na udhalilishaji yaliyoripotiwa Januari yalifanywa dhidi ya watoto, asilimia 8.2 yalikuwa dhidi ya wanawake na wanaume asilimia 4.1.
Miongoni mwa watoto 150 waathirika wa ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, wasichana waliobakwa walikuwa 84, wavulana waliolawitiwa 12 na wasichana saba waliingiliwa kinyume na maumbile.
Kutorosha walikuwa wasichana 8, shambulio la aibu walikuwa wasichana 16 na shambulio walikuwa 23 kati yao wasichana walikuwa 11. Wasichana walioathiriwa walikuwa 126 sawa na asilimia 84 na wavulana walikuwa 24 ambayo ni sawa na asilimia 16.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya OCGS, katika matukio 150 yaliyofanywa dhidi ya watoto, 72 yalifanywa kwa walio katika umri wa miaka 15 hadi 17 ambao ni waathirika wakubwa.
Kundi hilo lilifuatiwa na wenye umri wa miaka 11 hadi 14 kupitia matukio 42 yaliripotiwa dhidi yao, huku walio na umri wa kati ya miaka 6 hadi 10 wakiripoti matukio 24.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa watoto walio na umri sifuri hadi miaka mitano ni miongoni mwa waathirika kwani matukio 12 yaliripotiwa dhidi yao.
Matukio yanayoongoza
Kubaka ni tukio linaloongoza kwa kuripotiwa vipindi vyote na Januari pekee kwenye kesi 89 zilitajwa waathirika 84 walikuwa wasichana na 5 walikuwa wanawake.
Matukio ya kulawiti kwa mwezi huo yalikuwa 12 ambapo waathirika wote walikuwa wavulana huku matukio ya kuingilia kinyume na maumbile yakiwa 7 ambapo waathirika wote walikuwa wasichana.
Pia miongoni mwa matukio yaliyoripotiwa yalikua ni kutorosha yaliyokuwa 9 ambapo 8 kati yake walikuwa wasichana na mmoja (1) mwanamke.
Shambulio la aibu au kukashifu yalikuwa 16 ambapo wote walikuwa wasichana. Matukio ya shambulio yalikuwa 38 ambapo waathirika 11 walikuwa wasichana 12 walikuwa wavulana, Wanawake walikua nane na wanaume saba.
Maeneo yanayoongoza
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wilaya ya Magharibi B inatajwa kusajili matukio mengi yaliyokuwa 47 sawa na asilimia 27.5 ya matukio yote.
Wilaya ya Mjini ilisajili matukio 43, wilaya ya Magharibi A (33), Chakecheka (20), Kaskazini B (7), Micheweni (6), Kaskazini A (5), Kati (5), Wete 3 huku wilaya za Kusini na Mkoani zikiripotiwa kuwa na idadi ya tukio moja kwa kila wilaya.
Akitaja siri ya tukio moja pekee kuripotiwa katika mkoa wake, Hatibu Juma Njaja ambaye ni mkuu wa wilaya ya Mkoani anasema, “tunapambana pamoja, hizi ni miongoni mwa kesi ambazo hazivumiliki hata Rais Dk Hussein Mwinyi amekuwa akisisitiza hilo,” anasema.
Anasema endapo mtuhumiwa atabainika wamekuwa wakimchukulia hatua za kisheria haraka, kuondoa mwanya wa mapatano, pia kutoa elimu katika shehia kujua wanapaswa kufanya nini matukio hayo yakitokea.
Sababu za kuongezeka
Wakati matukio haya yakiongezeka, hali duni za maisha za familia zinatajwa kuwa moja ya sababu inayochochea watoto kufanyiwa ukatili.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude kukosekana kwa huduma muhimu, huchochea watoto kujiingiza katika njia hatarishi za kujitafutia mahitaji ambazo hutumiwa na wenye nia ovu kuwafanyia ukatili.
“Ukiangalia kama wale watoto waliopo mtaani, wanatafuta hela, hawana malezi, akitokea mtu akawaambia njoo nitakupa hela anaenda, hivyo baadhi huweza kutumia uhitaji wao kuwafanyia vitendo viovu,” anasema Mkude.
Anasema familia ikiwa haina kipato cha uhakika hata kuiongoza inakuwa ngumu, tofauti na ile yenye kipato kinachoweza kukidhi mahitaji.
Hiyo ni kwa sababu wazazi hushindwa kupanga mipango mizuri kwa ajili ya watoto wao kuanzia umri mdogo mpaka wanapokuwa watu wazima.
Anasema ni muhimu umasikini ukadhibitiwa kwani mzunguko wake hubeba vitu vingi na wakati mwingine kuwa chanzo cha mimba za utotoni.
Akiunga mkono suala hilo, Jesca Mzurikwao anasema matukio mengi yanayotokea mtaani dhidi ya watoto, chanzo chake huwa ni kudanganyiwa fedha na zawadi ndogondogo.
“Vitu anavyopewa mara nyingi ni vile ambavyo mzazi hampatii mara kwa mara ndiyo maana ni ngumu kusikia mtoto kutoka familia yenye kipato cha kati karubuniwa kwa vitu kama hivyo, ukiachana na wale wanaokutana na ukatili shuleni au kwenye nyumba za ibada,” anasema Jesca.
Akiwa kama mama pia anaonya tabia ya baadhi ya wazazi kuwaamini majirani hususani wanaume.
“Mtoto akiona mama amemzoea mjomba ambaye anakaa chumba cha jirani, anampa uhuru wa kumpa zawadi zote, anakuwa hana wasiwasi na kuhisi yuko mikono salama bila kujua watu wamebadilika,” anasema.
Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa anasema malezi duni ya wazazi ni moja ya sababu ya kuendelea kuwapo kwa matukio haya.
Anasema katika baadhi ya maeneo kawaida kukuta wazazi wanamuacha binti wa miaka 5 hadi 6 nyumbani akiwa mwenyewe, wakati wao wanaenda katika shughuli za kujiingizia kipato jambo ambalo linahatarisha usalama wake.
“Binti anayepaswa kuachwa nyumbani mwenyewe walau ni kuanzia miaka 15 ambaye yupo katika umri wa kujitambua akiwa mdogo chini ya hapo hutoa mwanya kwa wenye nia ovu kuwafanyia ukatili,” anasema Olengurumwa.
Akilizungumzia hilo, Mkuu wa Divisheni ya Watoto, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Zanzibar, Mohammed Jabir anasema kuwapo kwa ongezeko hilo huenda ikabebwa na picha mbili ikiwamo kuwapo mwamko wa watu kuripoti matukio hayo.
Anasema mbili huenda imechangiwa tukio lililokuwapo katika mwezi husika unaoweza kuwa kama kichochea kilichoongeza matukio hayo.
Mara kadhaa Rais Mwinyi amekuwa akikemea uwepo wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji akieleza kuwa suala hilo halivumiliki.
Katika hatua ya kupambana na matukio hayo, Dk Mwinyi aliunda na kuzindua kamati ya kupinga udhalilishaji wa kijinsia.
Nini kifanyike?
Katika hilo, Olengurumwa anasema ili kumaliza tatizo hilo juhudi mbalimbali zinahitajika ikiwemo kutoa elimu ya haki za binadamu kwa watu wote ikiwemo watoto tangu wakiwa wadogo. “Watoto wenyewe hawajui haki zao tangu wakiwa wadogo, baadhi wanafanyiwa vitendo vingine na kuona ni sawa, inaweza isiwe na matunda ya hapo lakini kwa miaka 10 ijayo tukaona faida yake,” anasema Olengurumwa.
Anasema hali hiyo itawafanya wao kujilinda na hata baadaye wanapokuwa wazazi inakuwa ni rahisi kuwalinda watoto wao.
Anasema njia nyingine inayoweza kukomesha suala hilo ni kutoa elimu kwa jamii na kuileza namna malezi bora yanavyoweza kumuepusha mtoto kupitia katika vitendo vya ukatili wa kijinsia.