Kitaifa

Sheria ya makampuni kufumuliwa kuvutia uwekezaji

Dar es Salaam. Serikali inakusudia kufanya maboresho kwenye Sheria ya Makampuni sura 212 na sura 213 ya Majina ya Kampuni, lengo kukuza na kuvutia uwekezaji zaidi nchini na kuendana na hali sasa ya mabadiliko ya teknolojia.

Marekebisho ya sheria hiyo yanafuatia maoni ya wadau waliyoyawasilisha kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), wakidai sheria hiyo haiendani na mazingira ya sasa ya biashara nchini.

Baada ya kupokea maoni hayo Brela na kuyafanyia utafiti, ilibaini dosari kwenye sheria hiyo yakiwemo masharti kuwa ili upate jina ya biashara lazima kampuni iwe na watu 20 na iwe na majukumu tofauti manne; wadau wakipendekeza kampuni iwe na kazi moja na idadi ya watu ipunguzwe kutoka 20.

Maoni hayo Brela iliyawasilisha kwa Tume ya Marekebisho ya Sheria Tanzania, ambayo pia inayapitia na kutoa mapendekezo kwa ajili ya maboresho ya sheria hiyo.

Akichangia mjadala wa mabadiliko ya sheria hiyo leo Machi 12, 2024 jijini Dar es Salaam, Balozi Mwanaidi Maajar amependekeza Sheria ya Makampuni namba 400A iondolewe.

Amesema Sheria hiyo inampa mamlaka makubwa msajili wa makampuni kuifuta kampuni yoyote bila kujiridhisha, inapotuhumiwa kwa masuala ya uhalifu.

“Msajili hawezi kujua kwenye kampuni fulani umetendeka uhalifu bila uchunguzi wa vyombo vya usalama, hakuna utaratibu unaofuatwa, bali kampuni kufutwa, sasa kama sheria hii mliweka muwatishe wahalifu, basi mmefukuza watu wazuri, tunataka kuwe na sheria ya kuwalinda wafanyabiashara dhidi ya tatizo lolote linapotokea, hatua zichukuliwe kwa kosa lisilotiliwa shaka,” amesema.

 Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Nathaniel Mandepo amesema maboresho yatakayofanyika ni katika kutengeneza mazingira ya uwekezaji nchini.

“Hatua hizi za awali za kukusanya maoni ya wataalamu itafuatana na utafiti wa mapungufu kwenye sheria, sera na mfumo unaotumia sheria husika, kupata taarifa muhimu zitakazosaidia maboresho,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Usajili Makampuni na Majina ya Biashara Brela, Isdor Nkindi amesema baada ya maboresho ya sheria wafanyabiashara na wanajamii watajiona ni wadau wanaotegemeana.

 “Kampuni zinazorudisha mchango kwa jamii (CSR) zimekuwa zikiona  zinachokifanya ni hisani, hivyo sheria itakwenda kutambua CSR kama takwa la kisheria. Kwa mataifa mengine CSR ni jambo la lazima,” amesema.

Akifungua kikao hicho, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda ambaye ni Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), William Erio amesema maboresho ya sheria yanalenga kuwapa fursa wafanyabiashara nchini kuchangamkia masoko ndani na nje ya nchi.

Alisisitiza Serikali inahamasisha uwekezaji na kuvutia wawekezaji nchini na maboresho hayo yakifanyika uwekezaji utaongezeka zaidi nchini.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi