Kitaifa
Utafiti watajwa mwarobaini saratani zinazoathiri wanawake
Dar es Salaam. Serikali imetakiwa kuwekeza kwenye utafiti na mazingira wezeshi katika kupambana na saratani zinazowaathiri wanawake, ikiwemo kuwafuata walioko maeneo ya pembezoni.
Maoni hayo yametolewa wakati takwimu zikionyesha saratani ya shingo ya kizazi na matiti zinazowaathiri wanawake, zikichukua asilimia 45 ya saratani zote.
Akizungumza kuhusu saratani katika maadhimisho ya siku ya wanawake yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa),mtaalamu wa magonjwa ya saratani kwa wanawake na watoto, Profesa Rashmiin Aiyushman kutoka Hospitali ya Ramaiah ya nchini India, amesema ni muhimu kuzungumzia masuala wanayowahusu wanawake ili kuokoa watoto wanaobaki yatima kutokana na vifo vya mapema vya wanawake vinavyosababishwa na saratani.
“Changamoto kubwa wanawake hawana elimu, hawapati huduma za vipimo na kinga dhidi ya saratani. Ni muhimu kwa wao kujua hali zao mapema kupitia vipimo na matibabu. Kuna haja kuweka mifumo itakayowezesha namna ya kuwapima na kuwabaini mapema pia katika ngazi ya kijamii wapewe elimu,” amesema.
Amesema katika Bara la Asia, tafiti mbalimbali zinazofanyika zinaonyesha wanawake wanaathirika zaidi na saratani ikilinganishwa na wanaume na hivyo wamewekeza zaidi kwenye tafiti ili kupata suluhisho la changamoto hiyo.
“Tafiti zina umuhimu na sera zinazotungwa serikalini zizingatie kundi la wanawake, kuwekeza kwao kielimu na kupima. Huduma zipewe kipaumbele na katika ngazi za maamuzi ziangalie wanawake wenye miaka 20 na 30, lakini pia lazima ionekane nafasi ya kinababa katika kuangalia wanawake wenye changamoto hii kwani baadhi yao huwatelekeza,” amesema.
Akizungumzia ombwe lililopo katika uchechemuzi wa taarifa za saratani kwa wanawake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk Rose Reuben, amesema saratani zinawapata wanawake zaidi ya wanaume na takwimu mbalimbali zinaonyesha hilo.
Amesema nchini India ambako takwimu zilionyesha saratani kuwapata wanaume zaidi, hivi karibuni baada ya kufanya utafiti, wamebaini idadi ya wanawake wenye saratani inaongezeka zaidi na wametafuta taratibu mbalimbali za kuondoa hilo ombwe.
“Wenzetu wanawafuata wanawake waliko kwa kutumia magari ambayo yanakuwa na madaktari kwa kuwafuata vituoni na hivyo kupata wanawake wenye changamoto hiyo mapema na kuwapa matibabu,” amesema.
Hali ilivyo nchini
Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya 42,000 kila mwaka na kati yao 4,300 ni wenye saratani ya matiti, lakini wanaofika kwenye vituo vya huduma za afya ni 15,900 pekee.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2017, vifo vitokanavyo na saratani ya matiti vinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2030, huku idadi ya wagonjwa wapya ikitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 82.
Saratani ya matiti ni aina ya saratani ya kawaida ambapo wanawake milioni 2.3 waligunduliwa na wanawake 685,000 walipoteza maisha yao mwaka 2020, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).