Connect with us

Kitaifa

Mambo sita yatajwa suluhu mgogoro wa NHIF, watoa huduma binafsi

Wadau wa afya wamependekeza mambo sita kumaliza mgogoro baina watoa huduma za afya binafsi na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ikiwemo Serikali kuondoa kodi kwa watoa huduma wa afya wa sekta binafsi.

Mambo mengine ni uwepo wa mamlaka itakayosimamia na kudhibiti masuala ya afya, NHIF kuboresha mifumo ya teknolijia ya habari na mawasiliano (Tehama), kudhibiti ulaghai unaofanywa na watoa huduma na kuwepo kwa adhabu kali kwa wanaokiuka utoaji huduma.

Hatua nyingine iliyopendekezwa ni mapitio ya gharama za huduma za afya kwa kutumia mifumo inayokubalika kimataifa na Serikali kuipa NHIF fedha za kujiendesha kwa miaka miwili.

Maoni hayo ya wadau yametolewa jana Jumatano, Machi 6, 2024 kupitia mjadala wa Mwananchi X Space iliyoandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ikiwa na mada isemayo ‘Nini kifanyike kupata suluhisho la kudumu baina ya NHIF na watoa huduma binafsi.’

Mjadala huo uliodumu kwa takribani saa mbili kuanzia saa 2:00 hadi saa 4:10 usiku, umeshirikisha wadau mbalimbali wa sekta binafsi, Wizara ya Afya pamoja na wataalamu kutoka NHIF.

Wadau hao wanatoa maoni ikiwa ni siku chache zimepita tangu Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya Tanzania (Aphfta) na Jumuiya ya Wamiliki wa Hospitali Binafsi Zanzibar (Zaphoa) kutangaza mgomo kwa kutokubaliana na matumizi ya kitita kipya cha mafao kilichoanza kutumika Machi mosi, 2024. Hata hivyo, mgomo huo umeisha baada ya wadau hao na Serikali kukubaliana kurudi katika meza ya mazungumzo.

Madai ya watoa huduma hao yalijikita katika hoja ya kwamba gharama zilizokokotolewa ndani ya kitita kipya kilichoboreshwa cha NHIF zinawaumiza na zitawafanya washindwe kutoa huduma na kuwasababishia hasara ya asilimia 30.

Mgomo wa watoa huduma hao kwa siku moja ulimfanya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyekuwa mkoani Lindi katika ziara kuitisha mkutano na waandishi wa habari akiwataka watoa huduma hao kusitisha mgomo na kurejea kwenye meza ya mazungumzo na Serikali hatua ambayo iridhiwa na watoa huduma.

“Kamati ya kitaalamu niliyoiunda iendelee kufanya majadiliano na watoa huduma wakati huduma zikiendelea kutolewa. Naomba kusisitiza kuwa, majadiliano yatafanyika wakati huduma zinaendelea kutolewa,” alisema Ummy, Machi mosi, 2024 akiwa Lindi.

Baadhi ya hospitali zilizokuwa zimesitisha kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF zilrejesha huduma kwa masharti wanakwenda kwenye meza ya mazungumzo kama alivyoeleza Waziri Ummy.

Nondo za wadau

Mtaalamu wa masuala ya bima, Anselmi Anselmi akichangia mjadala wa X-Space, amesema Aphfta na NHIF zimekuwa na matatizo ya kiutendaji, upande mmoja ukisema  NHIF inachelewesha madai na kumekuwa na utaratibu mgumu wa kuridhia matibabu, upande mwingine ukidai  wagonjwa wanapewa dawa ambazo hawahitaji au gharama tofauti na dawa iliyotumika na ulaghai.

“Ili kumaliza matatizo haya na mengine, ni lazima bei ziwe zinapitiwa mara kwa mara kwa kufuata mifumo inayokubalika kimataifa, pili kuwe na muongozo wa bei na kuzingatia utafiti kati ya sekta binafsi na umma,” amesema.

Suluhu nyingine aliyoitaja ni Serikali kutoa msamaha wa kodi kwa sekta binafsi, kwani sekta hiyo ni muhimu akisistiza kama msamaha imeondolewa kwenye kilimo inawezekana kwenye afya.

Mbali na hayo, Dk Anselmi ameshauri NHIF iboreshe mifumo yake ya Tehama ambayo itapunguza ulaghai na kurahisisha ulipaji wa madai huku akisisitiza adhabu kwa wanaofanya ulaghai.

Naye mshauri na mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amesema sekta binafsi imekubali kutoa huduma za afya baada ya mgomo, lakini hoja yao ni kupata hasara kutokana na ukokotozi wa ulipaji gharama ulivyofanyika.

“Walisema wanakwenda kupata hasara na tuliona kamati iliyoundwa waliwawekea faida ya asilimia 10 hadi 20, ukiangalia kwenye uendeshaji wa hospitali kwa uhalisia faida hiyo kwa taasisi inayolipa kodi nyingi na mishahara mikubwa nilidhani hiyo faida ni kwa wanaouza duka na si sehemu kama hospitali,” amesema.

Dk Osati amesema kutokana na ukokotozi huo, wagonjwa na wanachama wa NHIF wanakwenda kupata huduma isiyo bora, jambo ambalo linakwenda kurudisha nyuma kasi ya uongezaji huduma za afya na kuinua tiba utalii nchini.

Amesema ni lazima Serikali kupitia Wizara ya Fedha ifanye uamuzi wa makusdi wa kuweka fedha kwenye mfuko wa NHIF walau kwa miaka hii miwili, kabla ya kwenda kwenye bima ya afya kwa wote.

Amesisitiza kama hilo halitazingatiwa matatizo yatakwenda kuwa makubwa akisisitiza suala la upotevu wa fedha NHIF linapaswa kuimarisha mifumo yake.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deusdedit Ndilanha ameshauri mabadiliko yanayofanyika NHIF lazima yaguse watoa huduma wote kwa jicho la kipekee.

Dk Ndlahna amesema mfuko umekuwa na taratibu wa kufanya maboresho kila baada ya muda na mara nyingi kumekuwa na sintofahamu na katika hilo madaktari wamekuwa wakitoa ajenda zao ambazo ni za kudumu.

“Ajenda yetu ya kwanza ambayo tuliipeleka kwenye menejimenti ya NHIF, ni kuwa ibaki kuwa mtoa huduma na kiwepo chombo huru kitakachoisimamia katika vitu inavyovifanya kwa mwongozo, kitu kama hiki kitapunguza kelele kama sio kuondoa kabisa.

“Ajenda ya pili ilikuwa ni eneo la ada ya usajili na kumuona daktari. Katika mapendekezo waliyokuja nayo kuna maeneo waliyapunguza na kuongeza, madaktari walihoji inakuaje ada ya kumuona daktari iwe tofauti,” amesema Dk Ndlahna.

Akitoa ushauri juu ya nini kifanyike kutokana na mivutano hiyo, amesema kiwepo chombo cha mwongozo kitakachoisimamia NHIF.

“Kingine katika mabadiliko yoyote tutakayoyafanya, lazima tuwazingatie na madaktari ambao ndio watoa huduma,” amesema

Akitoa tathmini yake, Mhariri wa takwimu gazeti la Mwananchi, Halili Letea amesema huduma za NHIF zinategemewa na kunufaisha watu huku akisema jambo hili lililojitokeza limewagusa watu wengi.

“Kulingana na takwimu kuna asilimia nane ya watanzania wote hivyo ni watu wengi wanaotegemea huduma hiyo. Hadi Machi mwaka 2023 vituo vya afya vilivyoguswa na NHIF vilikuwa 8965 maanyake imegusa maeneo mengi huku vinatarajiwa kuongezeka zaidi.

NHIF imebeba mzigo huu

Akieleza uhalisia uliopo, Meneja wa Uchakataji Madai wa NHIF, Dk Raphael Mallaba amesema uwepo wa ongezeko magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, shinikizo la damu, figo yamekuwa na athari kubwa kwa mfuko kwa sasa.

“Katika mwaka wa fedha wa 2016/17 mfuko ulilipa madai kwenye magonjwa hayo Sh36 bilioni lakini katika mwaka 2022/23 NHIF imelipa Sh137 bilioni ambapo ongezeko hilo ni athari moja kwa moja kwa mfuko.

Aidha akifafanua zaidi, amesema NHIF inatoa huduma kwa watu zaidi ya milioni 4.9 ambapo kuna takribani asilimia 92 ya watu wapo nje ya mfumo wa bima.

Amesema pamoja na kuwa watu milioni 4.9 wanufaika wa mfuko, asilimia 80 ya mapato ya watoa huduma yanatoka NHIF hivyo watoa huduma wana utegemezi mkubwa wa mapato kwenye mfuko huo.

“Mfuko umesajili vituo vingi vya umma ambavyo ni asilimia 72 na mapato yao yanategemea kutoka kwenye mfuko wa taifa wa bima ya afya, kwa malipo ya mwaka wa fedha 2022/23 mfuko ulilipa Sh751 bilioni , vituo vya umma vililipwa asilimia 34 sawa na Sh252 bilioni pia vituo binafsi vililipwa Sh284 bilioni sawa na asilimia 38,”amesema

Suluhu ya sintofahamu iliyopo sasa, Dk Mallaba amesema tayari Serikali imepitisha sheria ya bima kwa wote ambayo wakati wa utekelezaji wa sharia hiyo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) itakwenda kusimamia shughuli zote.

“Kwa kuwa tunakwenda kuwa na TIRA tunakwenda kuwa na suluhu ya kudumu kwa sababu bei zitakazokwenda kutoka zitatumiwa na wote pia tunakwenda kuwa na wigo mpana wa NHIF, hivyo ni fursa zaidi kwa watoa huduma kuwahudumia watu wengi Zaidi,” amesema.

Akitoa suluhisho la kudumu kutokana na mtifuano huo kati ya NHIF na watoa huduma binafsi, Kamishna wa Tira, Dk Baghayo Saqware akizungumzia kwa upande wa huduma za dawa amesema kinachotakiwa ni uwepo wa muongozo wa bei.

“Wakati wa kamati ya kitita kipya nikiwa kama mwenyekiti wa kamati hiyo tuliongea na NHIF watoa huduma na wadau wengine, tukapata mapendekezo yao tukagundua kuna mambo yanachanganywa mfano tunasahau kuwa masuala ya NHIF na watoa huduma ni masuala ya kimkataba.

“Kwenye suala la bei lazima kuwe na mfumo wa mapendekezo ili mfuko ulipe. Kama kamati tukakubaliana na tukaona suluhisho la kudumu katka kitita hichi ni kuwa na bei elekezi ya ununuzi, uwiano wa faida na gharama za usimamizi ambazo ni vigezo vya kisayansi na kibiashara,” amesema.

Tatizo lilipoanzia

Februari 28, 2024, NHIF ilitangaza kuanza kutumika kwa kitita kipya Machi mosi, 2024 kitendo ambacho kilipingwa na APHFTA kwa madai ukokotozi wa gharama zilizowekwa kwenye kitita hicho kitawafanya kushindwa kutoa huduma kwa wanachama.

Watoa huduma hao walisema hasara watakayopata kama watatumia kitita kipya cha mafao ya gharama za huduma kilichofanyiwa maboresho na NHIF watakumbana na hasara ya hadi asilimia 30 kutokana na huduma nyingi kushushwa bei.

Kufutia msimamo wa Aphfta, hospitali mbalimbali ikiwemo Aga Khan, TMJ, Regency, Kairuki na Hospitali ya Upendo wilayani Babati mkoani Manyara, ziliitoa taarifa kwa umma za kutowapokea wanachama wa NHIF.

Mgogoro huo wa NHIF na watoa huduma za afya uliwaibua wadai mbalimbali waliotaka Serikali kuchukua hatua za haraka kuumaliza, kwani maumivu yalikuwa kwa wananchi.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi