Kitaifa

Serikali ya Rais Samia yapongezwa kwa kusimamia demokrasia

Dar es Salaam. Ikiwa zimesalia siku kadhaa kabla ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kufikisha miaka mitatu madarakani, Shirika la Mfuko wa Asasi za Kiraia (FCS) limesema uongozi huo umefanya kazi kubwa katika kuheshimu na kusimamia misingi ya demokrasia.

Mkurugenzi Mtendaji wa FCS anayemaliza muda wake, Francis Kiwanga amesema katika kipindi cha miaka mitatu Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha kwa vitendo kuheshimu misingi ya demokrasia.

Akizungumza leo Machi 5, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi ofisi kwa mkurugenzi mtendaji mpya, Justice Rutenge, Kiwanga amesema katika kipindi hicho cha uongozi, FCS imezidi kuwa daraja kati ya watu na Serikali.

“Tunajivunia uongozi wa Rais Samia unaoheshimu misingi ya demokrasia na uhuru wa watu,” amesema.

Hata hivyo,  amebainisha kuwa FCS itaendelea kuwa daraja kati ya watu na Serikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya jamii na Taifa kwa jumla.

“Kwetu tunaiona ni taasisi inayopigania misingi ya utawala bora, tunahitaji kuendeleza juhudi za kupambania maendeleo ya watu, na hili ni suala la kujikumbusha kila siku,” amesema Kiwanga.

Mwenyekiti wa Bodi ya FCS, Dk Ally Laay, amempongeza mkurugenzi mtendaji anayemaliza muda wake kwa kuwa mchapakazi, mwadilifu na kusimamia majukumu yake kwa weledi na kuiheshimisha taasisi hiyo.

Laay amesema ana imani kubwa na Rutenge anayetarajiwa kuanza rasmi majukumu yake Mei mosi, 2024 akichukua nafasi ya Kiwanga aliyehudumu kwenye shirika hilo kwa miaka nane.

“Rutenge ameshinda kwa kishido kikubwa licha ya kuwepo ushindani mkubwa katika mchakato mzima wa kumpata mkurugenzi mtendaji mpya, bodi imemwamini kuwa atafanya kazi vizuri na kuendelea aliposhia kiwanga kutokana na sifa alizo nazo na ni kijana,” amesema Laay.

Kwa upande wake Rutenge ameahidi kufanya kazi kwa weledi kulingana na taaluma na ujuzi alio nao kwa masilahi mapana ya jamii na Serikali kwa jumla.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi