Kimataifa

Marekani yang’ata, kupuliza vita vya Israel na Palestina

Dar es Salaam. Tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Palestina huko Gaza Oktoba 7, 2023, Marekani imekuwa mshirika wa karibu wa Israel kwa kutangaza msimamo wa kuiunga mkono.

Marekani iliahidi uungaji mkono  kwa Israel na msaada wa kijeshi. Katika majibu yake ya kwanza kwa shambulio la Hamas dhidi ya Israel, Rais wa Marekani, Joe Biden aliweka wazi, kuwa nchi yake inaiunga mkono Tel Aviv.

“Kwa yeyote anayefikiria kutumia fursa ya mgogoro huu, nina neno moja; usifanye kitu,” aliongeza.

Onyo hili liliilenga waziwazi Iran na nchi nyingine za Kiarabu zilizodhaniwa zinaiunga mkono Palestina.

Katika wiki ya pili tangu kuanza kwa vita hivyo, Marekani ilipeleka msaada wa silaha Israel sambamba na maofisa kadhaa wa kuishauri Israel katika masuala ya vita.

Hata hivyo, licha ya uungaji mkono huo wa Marekani kwa Israel, hivi karibuni imeshuhudiwa Marekani ikipeleka misaada ya kiutu kwa wananchi huko Gaza.

Haikushia hapo, kupitia makamu wake wa Rais, Kamala Harris Marekani imetoa wito wa kuyataka mataifa mengine kupeleka misaada huko Gaza na kutaka usitishwaji wa mapigano.

“lazima kuwe na usitishaji mapigano mara moja kwa angalau wiki sita zijazo na kusaidia kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel,” alisema Kamala katika hafla moja mjini Alabama jana Jumapili.

Hamas iliambia BBC kwamba haikuweza kufanya hivyo kwa sababu ya mashambulizi ya Israel.

Shinikizo la kusitishwa kwa mapigano liliongezeka baada ya tukio la Alhamisi nje ya Mji wa Gaza Kaskazini ambapo takriban watu 112 waliuawa wakati umati wa watu ulipokuwa ukigombea misaada na wanajeshi wa Israel wakafyatua risasi.

Wengi wanashindwa kuelewa msimamo halisi wa Marekani wanaona kitendo cha kuisaidia Isreal silaha za kivita huku ikipileka misaada Gaza kwa waathirika wa vita hivyo kinaleta mkanganyiko.

Mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia, Innocent Shoo amesema misaada ya Marekani huko Gaza ni kutaka kurejesha imani yake duniani huku ikifahamika kuwa imechangia kwa kiasi kikubwa mauaji ya raia kwa kuiunga mkono Israel kupitia misaada yake ya silaha.

Shoo amesema uchaguzi mkuu nchini Marekani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu ni moja ya sababu za Marekani kupeleka misaada na kutaka mapigano yasitishwe walau kwa wiki sita, lengo likiwa ni kurejesha imani kwa taifa hilo.

Ameongeza kuwa kitendo cha Israel kukataa mazungumzo ya usitishaji wa vita huko Misri siku za hivi karibuni kunatokana na wasiwasi kwamba huenda wakikubali kusitisha mapigano kundi la Hamas linaweza kujipanga upya kuendelea na vita huku lengo la Israel likiwa ni kuifuta Hamas.

“Ni ngumu kusitisha mapigano kwa sababu masharti wanayowekeana ni magumu kutekelezeka. Israel inataka iendelee kubakisha jeshi lake Gaza wakati Palestina inataka jeshi la Israel liondoke Gaza, ni ngumu,”amesema Shoo.

Amesema mauaji ya raia wengi wa Gaza yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na wanamgambo wa Hamas kujichanganya kwa raia bila kuvaa sare za jeshi, jambo lililosababisha majeshi ya Israel kupiga raia pale linapohisi kuna maadui katikati yao.

Zaidi ya watu 30,000, wameuawa tangu kuanza kwa vita hivyo huku idadi ya waliojeruhiwa ikifikia zaidi ya 71,000.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi