Connect with us

Kitaifa

JKCI, UDSM kushirikiana mafunzo ya matibabu ya moyo, figo

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wameingia ushirikiano wa kutoa mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa  wa moyo na figo ili kuboresha sekta ya afya.

Mafunzo hayo yanalenga kuzalisha wataalamu watakaokuwa na uwezo wa kutoa huduma bora kwa wagonjwa na uangalizi wa juu, jinsi ya kuokoa maisha na kuwahudumia wagonjwa mahututi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Machi 4, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema kuna uhitaji wa wataalamu, hivyo ushirikiano huo utawezesha kuleta tija.

Amesema zitaanzishwa programu za mafunzo ya shahada na chini ya shahada katika programu zitakazoanzishwa za upasuaji wa moyo na udaktari bingwa wa matibabu ya tundu dogo la moyo.

“Nchini tuna madaktari bingwa wa moyo wasiozidi 50 na Watanzania tuko zaidi ya milioni 60, hivyo uhitaji ni mkubwa ndio maana tukaona tuongeze watumishi kupitia kuwafundisha katika eneo hili watoe huduma,” amesema Dk Kisenge.

Dk Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, amesema Tanzania imepiga hatua katika kuwekeza kwenye vifaatiba na majengo.

Amesema kutokana na uwekezaji huo, wameamua kuzalisha wataalamu hao ili wakafanye kazi ya kutoa huduma.

“Hapa nchini kuna idara za uangalizi, idara za dharura, mitambo ya tundu dogo la moyo katika hospitali za umma na binafsi, yenye gharama ya karibu Sh7 bilioni kwa mtambo mmoja na ili kuendeshwa, mitambo hii inahitaji wataalamu wa hali ya juu,” amebainisha.

Kufuatia mpango huo,  amesema wauguzi na wanafunzi wanatakiwa wakasome wapate utaalamu zaidi ili waweze kuhudumia wagonjwa ipasavyo.

“Tutakuwa tunatumia vifaa vya kisasa, pamoja na teknolojia ya hali ya juu katika kufundisha wanafunzi wetu tukiwatumia madaktari kutoka India, Italia, Israel na Marekani, ” amebainisha.

Akieleza faida zake, amesema mafunzo hayo yataboresha tiba utalii ambayo imeanza kuongezeka.

Alisema kwa mwaka jana JKCI imehudumia wagonjwa zaidi ya 500 kutoka nchi za Congo DRC, Zimbabwe, Msumbiji, Malawi, Comoro  na wageni kutoka Ujerumani, Poland,  Marekani na China.

Naibu Makamu Mkuu wa UDSM anayeshughulikia taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa amesema sababu ya kushirikiana na JKCI ni kutoa mafunzo ya darasani na wodini ili wauguzi wawe na uwezo wa kutenda.

“Tumeamua kuingia ushirikiano na JKCI ili kutoa mafunzo ya tiba na sayansi shirikishi kutokana na uhaba wa wataalamu katika eneo hili. Sababu ya pili ya ushirikiano huu tunataka kutoa mafunzo ya vitendo ili kuwa na wataalamu wabobezi,” amebainisha.

Taasisi zote mbili zimepata ridhaa za mamlaka zake za usimamizi ili kuanza kushirikiano na kuwa wataanza na programu fupi za mafunzo.

“Tutakuwa tunatoa mafunzo ya shahada na chini ya shahada kwa kuwafundisha wanafunzi ambao watahitimu kwa jina la UDSM ila kwa sasa tunaandaa mitalaa,” amesema Profesa Rutinwa.

Awali, Daktari Bingwa wa kuzibua mishipa ya moyo, Dk Khuzeima Khanbhai amesema programu hizo za mafunzo zitakuwa za kwanza nchini, Afrika Mashariki na Kati.

“Yatakuwa mafunzo ya kwanza ambapo tutafundisha kuzibua mishipa ya mtu akipata shambulio la moyo ili kuongeza wataalamu nchini,” amebainisha Dk Khanbhai.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi