Kitaifa
Demokrasia yashuka duniani, sababu ya Tanzania kuimarika
Hali ya ukuaji wa demokrasia duniani imekuwa ikipitia changamoto nyingi, ambapo baadhi ya mataifa yanafanya vizuri kwenye eneo hilo, mengine yakitawaliwa kiimla na mengine yakiwa ni utawala mseto wa demokrasia.
Mataifa ya Afrika ambayo bado demokrasia yake inakua, yameangukia kwenye utawala wa kiimla huku mengine yakiwa na utawala mseto, ikiwemo Tanzania ambayo uchaguzi wake wa mwaka 2020 ulilalamikiwa na wadau kila kona.
Ripoti ya hali ya demokrasia duniani iliyoandaliwa na Economist Intelligence Unit (EIU) kupitia ripoti yake ya “Democracy Index 2023” imeangazia hali ya demokrasia katika nchi 165 na nchi mbili zisizo na utawala kamili.
Vigezo vilivyotumika kupima hali ya demokrasia katika mataifa hayo vimezingatia mambo kadhaa, ikiwemo mchakato wa uchaguzi na mfumo wa vyama vingi, utendaji kazi wa Serikali, ushiriki wa kisiasa, utamaduni wa kisiasa na uhuru wa wananchi.
Kwa kuzingatia vigezo hivyo, kila nchi inawekwa kwenye kundi lake kati ya makundi manne ya utawala ambayo ni demokrasia kamili, demokrasia yenye upungufu, utawala mseto na utawala wa kiimla. Habari njema ni kwamba nchi mbili zilizotambuliwa kama za kidemokrasia ziliongezeka na kufanya idadi kufikia 74 mwaka 2023. Hata hivyo, kwa kuzingatia vigezo vingine, mwaka 2023 haukuwa mzuri kidemokrasia.
Kati ya mwaka 2022 na 2023, wastani wa alama za utawala wa kiimla zilishuka kwa pointi 0.12 na utawala mseto kwa pointi 0.07.
Wastani wa alama za demokrasia kamili na demokrasia yenye upungufu kila mwaka ulishuka kwa pointi 0.01 na 0.03 kila moja.
Hii inaonyesha kwamba tawala zisizo za kidemokrasia haziko tayari kubadilika wakati tawala mseto zikijitahidi kupambana kuwa za kidemokrasia.
Kwa mujibu wa vipimo vilivyotumika kwenye utafiti huo, takribani nusu ya ulimwengu unaishi katika demokrasia ya aina fulani (asilimia 45). Ni asilimia 7.8 pekee ndiyo wanaishi kwenye demokrasia kamili, ikiwa imeshuka kutoka asilimia 8.9 mwaka 2015.
Kiwango hicho cha asilimia kiliporomoka baada ya Marekani kuondolewa katika kundi la nchi zenye demokrasia kamili na kuwa nchi yenye demokrasia yenye upungufu mwaka 2016, na sasa bado iko kwenye kundi hilo.
Theluthi moja ya watu duniani wanaishi katika tawala za kiimla (asilimia 39.4), kiwango ambacho kimekuwa kikiongezeka miaka ya hivi karibuni.
Idadi ya nchi zenye demokrasia kamili (zilizopata alama zaidi ya 8 kati ya 10) ziliendelea kuwa 24 mwaka 2023, sawa na mwaka uliotangulia. Idadi ya nchi zenye demokrasia zenye upungufu ziliongezeka kutoka 48 mwaka 2022 hadi 50 mwaka 2023.
Kati ya nchi 95 zilizosalia kwenye utafiti huo, 34 zimeainishwa kama nchi zenye tawala za mseto, zinazochanganya vipengele vya demokrasia kamili tawala za kiimla, na 59 zimeainishwa kama nchi zenye tawala za kiimla.
Katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, Mauritus ndiyo nchi pekee iliyotambuliwa kuwa na demokrasia kamili ikishika nafasi ya 20 duniani.
Kwa Afrika Mashariki, Tanzania, Kenya na Uganda zimeorodheshwa kama nchi zenye tawala mseto wakati Rwanda, Burundi na Jamhuri ya DR Congo zikiwekwa kundi la nchi zenye utawala wa kiimla.
Kwa upande wa alama, Tanzania inaongoza katika nchi za Afrika Mashariki ikishika nafasi ya 12 kikanda na kidunia nafasi ya 86, ikifuatiwa na Kenya nafasi ya 14 kikanda na 92 kidunia wakati Uganda inashika nafasi ya 16 kikanda na 99 kidunia.
Tatizo la michakato ya uchaguzi na raia kutokuwa na uhuru kutokana na migogoro ya kisiasa limeuandama ukanda wa Afrika Magharibi kiasi cha kuangukia kwenye kundi la nchi zenye utawala wa kidikiteta, nchi hizo ni pamoja na Equetorial Guinea, Libya, Sudan, Chad, Burkina Faso, Djibout, Mali, Cameroon, Togo na Niger.
Nchi zinazoongoza duniani kwa kuwa na demokrasia kamili ni Norway, New Zealand, Iceland, Sweden, Finland, Denmark, Ireland, Switzerland, Uholanzi na Taiwan. Nchi nyingine ni Ujerumani, Luxembourg, Canada, Australia, Uruguay na Japan.
Baadhi ya nchi zilizo kwenye utawala wa kiimla duniani ni Afghanistan, Myanmar, Korea Kaskazini, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Syria, Turkmenstan, Chad, DRC, Sudan, Libya, Equitorial Guinea, Tajikistan, Yemen, Iran, Eritrea na Belarus.
Maoni ya wadau
Mchambuzi wa siasa za kimataifa, Ibrahim Rabbi anasema kushuka kwa demokrasia duniani huenda kulisababishwa na waliotambulisha na kuleta dhana hiyo kwa sababu waliwaaminisha watu njia bora ya kuishi ni kufuata demokrasia. “Kwa miaka ya hivi karibuni waliotuaminisha wao wenyewe demokrasia imewashinda na sheria walizotuaminisha kama misingi bora, ikiwemo mifumo ya haki wameigeuza kuingiza maslahi yao,” anasema.
Rabbi anasema hata mapinduzi mengi Afrika kuanzia mwaka 2020 viongozi walikuwa wanasema demokrasia ya Magharibi na Afrika hailingani.
Anasema Afrika demokrasia iliporomoka kuanzia mwaka 2017, kipindi ambacho Marekani ilipata Rais mhafidhina Donald Trump aliyeenda tofauti na msimamo wao wa kusimamia demokrasia duniani.
“Kipindi kile Trump alikuja na sera ya Make America Greet Again kwa kuitazama Marekani zaidi na ikajitenga na Afrika na kujiondoa kwenye mifumo mingi duniani, ikiwemo kwenye mikataba ya mabadiliko ya hali ya hewa.”
Kwa upande wake, mwanazuoni wa sayansi ya siasa na sheria kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), Profesa Ambrose Kessy anasema nafasi ya Tanzania kwenye ripoti hiyo si jambo la kushangaza kwa sasa kutokana na Rais aliyepo madarakani (Samia Suluhu Hassan).
“Serikali ya sasa imebadilika, imetoa uhuru mkubwa kwa watu kujieleza bila kuvunja sheria na nafikiri imejitathimini na kuona kila mtu anayo nafasi ya kufanya mapinduzi katika taifa iwapo atapewa nafasi,” anasema.
Anasema kupitia ripoti ya utafiti huo Serikali kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), wanapaswa kuichukua na kuifanyia kazi kwa undani kwa kuwa hazidanganyi kwa kuangalia na maeneo mengine yanayokuza demokrasia.
“Rais Samia amejitahidi kufanya mengi na yote hayo yanaonekana ni katika kuionesha dunia tunakua kutoka chini ambako watu walikuwa wanalalamika kutokuwa na uhuru hasa vyama vya upinzani,” anasema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisuilie anasema 4R imechangia kwa kiwango kikubwa katika kipindi hiki na imesaidia kuleta mapinduzi ya siasa za Tanzania, huku akitolea mfano wakati Chadema wanafanya maandamano yao Mbeya waligoma kumpisha Naibu Waziri Mkuu Dk Doto Biteko.
“Ingekuwa miaka ya nyuma hali ingekuwa tofauti na si ajabu wangesambaratishwa, kwa hiyo ndani ya kipindi hiki ustahimilivu umeshamiri kwa kiwango kikubwa kwa viongozi wa kiserikali,” anasema.
Anasema pamoja na kwamba kumekuwa na mjadala wa Watanzania na vyama vya siasa kuhitaji Katiba mpya, kitendo cha kuacha uhuru wa watu kupumua kusema ya kwao imeleta ufanisi mkubwa.
“Pia hata Rais mwenyewe anaonesha utashi mkubwa wa kisiasa, anastahimili vya kutosha kwa kuamini nchi inapaswa kujengwa na wote kwa kuruhusu kila mmoja kutoa mawazo yake,” anasema.
Anasema ndani ya kipindi cha miaka miwili nyuma Serikali imekuwa ikifanya maridhiano na vyama vya siasa na utulivu unazidi kuongezeka na ni eneo ambalo hata Kenya wamezidiwa.