Kitaifa
NHIF yawapa mbinu mpya wanachama wake
Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umewataka wanachama wake kutumia vituo mbadala kupata huduma ya matibabu ili kuepuka usumbufu wanaoweza kukutana nao katika hospitali binafsi.
Kauli hiyo imekuja baada ya Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya nchini Tanzanja (Aphfta) kutangaza kusitisha huduma kwa wanachama wa NHIF wakidai kuwahudumia ni kitengeneza hasara.
Uamuzi huo wa Aphfta unatokana na kuanza kwa bei ya kitita kipya kilichoboreshwa cha NHIF leo Ijumaa, Machi 1, 2024 ambacho watoa huduma hao binafsi wanakipinga.
Jana usiku, baadhi ya hospitali mathalani za Kairuki, Hospitali ya Regency na Hospitali ya TMJ za jijini Dar es Salaam zilitoa matangazo yaliyosambaa kwa kasi mitandaoni zikieleza kutowapokea wagonjwa wenye kadi za NHIF.
Kutokana na hilo, NHIF nayo imetoa taarifa kwa umma iliyosainiwa na Meneja Uhusiano wake, Angela Mzirary ikiwataka wanachama wake kutumia vituo mbadala kupata huduma.
NHIF imesema wanachokifanya watoa huduma hao binafsi ni kinyume cha mkataba unaowaka kutoa notisi ya siku 90 kama wanataka kusitisha kutoa huduma.
“Ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza, mfuko unawatangazia wanachama wake kutumia vituo mbadala kupata huduma,” imeeleza taarifa hiyo.
“Maofisa wa NHIF watakuwa katika vituo kuhakikisha wanachama wenye changamoto wanasaidiwa kupata huduma katika vituo vingine.”
Taarifa hiyo iliendelea kueleza, mfuko umeshaanza kuwasiliana na wanachama wenye matibabu yanayohitaji mwendelezo wa huduma ikiwamo huduma za kuchuja damu (dialysis) ili kuwaelekeza vituo mbadala kwa ajili ya upatikanaji wa huduma hizo.
Pia, NHIF imesema inaendelea kufanya usajili wa vituo vingine binafsi ili kuongeza wigo wa watoa huduma na kusogeza huduma kwa wanachama.
Mmoja wa wachangiaji wa taarifa hiyo kutoka mitandao ya kijamii, rmsonge2022 amesema tunahitaji maridhiano kati yenu na watoa huduma hao maana kwa sisi wahusika tumezoea kupata huduma kutoka kwao.”
NHIF imemjibu ikisema, “mfuko una vituo zaidi ya 9,200 ambavyo imevisajili, hivyo hakuna mwanachama atakayekosa huduma.”
Katikati ya mvutano huo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu jana akiwa katika Kituo cha Afya cha Mnazi Mmoja Mkoa wa Lindi akiendelea na ziara mkoani humo aliulizwa swali na waandishi juu ya hicho kinachoendelea na kueleza leo Ijumaa atalitolea ufafanuzi wa kina.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deus Ndlanha ametoa wito kwa madaktari kuzingatia weledi katika shughuli hiyo.
“Madaktari tuna kiapo chetu, mgonjwa anapokuja anahitaji huduma lazima umpatie, kisha mambo mengine yatafuata baadaye.
“Ikitokea kuna mambo kama hayo madaktari waendelee kutoa huduma wao wapo katikati kwa mujibu wa viapo vyetu, mgonjwa aendelee kupata huduma mpaka itakapoamliwa vinginevyo,” amesema Dk Deus.
Amesisitiza wajibu huo utekelezwe bila kutazama kama ni mnufaika au si mnufaika wa huduma, atalipa au atalipaje baada ya huduma hayo yatajulikana baadaye.