Kitaifa

Barabara za mitaa zitakazojengwa na DMDP

Dar es Salaam. Baada ya Serikali kusaini mkopo wa takriban Sh1 trilioni kutoka Benki ya Dunia (WB) unaolenga kutekelezaji Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu Dar es Salaam wa awamu ya pili (DMDP 2), hizi ndizo barabara zitakazoboreshwa ambazo pia zinatarajiwa kubadili mandhari na muonekano wa baadhi ya maeneo.

Mradi huo unalenga kuboresha barabara zenye urefu wa kilomita 250 katika manispaa zote tano— Kinondoni, Ilala, Kigamboni, Ubungo na Temeke, ikilinganishwa na kilomita 207 katika awamu ya kwanza ya mradi huo ambazo iligusa wilaya tatu pekee.

Februari 20, mwaka huu, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Mwakilishi Mkazi wa WB nchini, Nathan Belete walisaini mkopo huo katika ofisi ndogo za Hazina, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mkataba huo unaotarajiwa kuanza utekelezaji wake wa miaka sita katika mwaka wa fedha 2024/25, asilimia 78 ya fedha hizo zitaelekezwa katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara na masoko.

Kwa mujibu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) Mkoa wa Dar es Salaam, barabara za awali zitakazoanza kujengwa kwenye awamu ya kwanza ya utekelezaji na zimeshafanyiwa usanifu zitakuwa zina urefu wa kilomita 150.74.

Kwa wilaya ya Ubungo, jumla ya kilomita 36.11 zitajengwa kwenye maeneo zaidi ya 20 kwa umbali tofauti.

Katika maeneo yote barabara ndefu zaidi ni kilomita 9.83 ya Msumi, na Goba Wakorea kilomita 7.76, huku barabara fupi ni ile ya kilomita 0.28 ya Tiptop na barabara ya Shule.

Nyingine ni Hondogo Shija (4.16), Makoka (4.04), Posta Matembe (0.82), Sheikh Bofu (1.13), Msikitini (0.37), Sinza KKKT (0.27), Segesera (0.77), Lion (0.84), Juma Ikangaa (0.97), Mbegani (0.28), Namnani (0.66), Chimwaga (0.34) na Mikindani (0.45)

Zimo barabara za Ubungo NHC (0.6), Midizini (0.99) na Binti Kayenga (1.27). Jumla ni kilomita 36.11.

Manispaa ya Kinondoni

Kilomita 20.34 zitajengwa katika manispaa hii. Zipo barabara za Nakalekwa -Bwawani (7.32), Umoja (3.86), Mivumoni (4.79), Tegeta Polisi – Silver- Binti Matola (0.77), na Amiri/Leni Tatu (Dawasa) kilomita 0.68.

Nyingine ni Togo (0.36), Togo 2 (0.36) na Togo 3 (0.2).

Jiji la Dar es Salaam

Jumla ya kilomita 29.8 zitajengwa zikijumuisha barabara ya Banana Kitunda- Kivule -Msongola kilomita (16.31), Barakuda- Changombe -Majichumvi (3.27), Majumba Sita – Segerea (3.31), Migombani (1.57), Tabata Mawenzi – Kisiwani 2.12 na Bombom Market (0.12).

Barabara nyingine ni Community Park 2 (0.38), Community Park 2 Road 2 (0.56), Community Park 2 Road 3 (0.11), Community Park 2 Road 4 (0.11), Community Park 1 (0.35), Community Park 2 (0.11), Kigilagila Market 2 (0.28), Kigilagila Market (0.76), Kigilagila Market 3 (0.44).

Temeke

Kilomita 32.09 zitajengwa zikigusa barabara ya Ndunguru (1.64), Masaki (3.91) Masuliza (4.04) Kipati (0.72), Agape (1.07), Kilimahewa -Toangoma (6.17), Msikitini (0.45), Mwembeni (Nyika) (0.44), Malawi (0.28), Songambele (0.32), Mwakalinga Road 1.07.

Nyingine ni Markas (0.48), Majimaji (0.32), Keko Machungwa (0.57), Magorofani (0.31), Igome (Yemen) kilomita 0.85, Diwani (0.67), Basri (0.9), Konisaga 1 (0.29), Konisaga (3 0.4), Kurasini (1.12), Taningira (0.42), Uhasibu (0.44), Kizota (0.91) na Lushoto (0.3).

Pia zimo barabara za Pendamoyo (0.56), Pendamoyo 1 (0.2), Mandera (0.85), Mkumba – Miburani (0.39).

Kigamboni

Kwa upande wa Manispaa ya Kigamboni, zitaboreshwa barabara za kilomita 32.4.

Hizi zitajumuisha MC Full Shangwe (1.38), Gofingo – Shangwe (1.77), Kibada Plot (2.91), Lingia – Nyakwale (3.75), Gezaulole (Mivumoni) (7.05), Geza Juu – Eddah Avenue (2.92), Muongozo P/S (2.85), Pengo Simba (2.47), Dege Mbutu (1.6) na Atani Dege (1.76).

Nyingine ni Machava Njama (0.7), Mtaa wa Maji – Posta (1.28), Orasa (0.89), Mzee Msomi (0.65) na Polisi Pikori.

Meneja Tarura

Meneja wa Tarura Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga aliliambia gazeti hili kuwa wiki ijayo watatangaza zabuni, ili kuwapata wakandarasi watakaotekeleza jukumu hilo.

“Tunatarajia kuwa na wakandarasi zaidi ya watano katika ujenzi wa barabara hizi, kilomita 100 zilizobaki zinaendelea kufanyiwa usanifu na upembuzi yanikinifu na tutakuwa tunatoa mrejesho wa kila hatua tutakayoifikia,” alisema Mkinga.

Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile alisema wilaya hiyo ina mtandao wa barabara za Tarura takribani kilomita 1,000, lakini zenye lami hazizidi kilomita 10, hivyo ujio wa DMDP awamu ya pili umekuwa na manufaa makubwa.

“Itabadilisha taswira ya Manispaa ya Kigamboni, sambamba na kurahisisha usafiri kwa wananchi kutoka eneo moja kwenda lingine, ili kuleta tija ya kiuchumi,” alisema Dk Ndugulile, ambaye ni mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto alisema mradi wa DMDP una faida kubwa kwa wananchi wa jiji hilo, ikiwamo kurahisisha usafiri na shughuli za kiuchumi.

“Mtu anayekaa Kivule atakuwa na uwezo wa kufuata huduma Kariakoo na kurudi haraka, pia mradi huu umeenda kwa wananchi wa kawaida mitaani ambako kuna huduma za vituo vya afya.

“Kuna maeneo gari la wagonjwa kumfuata mtu ni shida, ujenzi wa barabara hizi utakuwa mwarobaini wa kuondokana na changamoto hizo,” alisema Kumbilamoto, ambaye ni diwani wa Vingunguti.

Mkazi wa Ilala, Asha Khamis alisema: “Ujenzi wa barabara hizi utatufanya tujihisi tunaishi mjini, tunasikia tu Masaki na Upanga kuna lami hadi milangoni, lakini kwetu Kitunda kuna vumbi, kiangazi na masika ni tabu,” alisema na kuongeza;

“Tunaishukuru Serikali inatukumbuka na kutujali, isiishie hivi iangalie na maeneo mengine yenye uhitaji, ili kuboresha miundombinu ya barabara,” alisema Khamis.

Mkazi wa Mabibo – Makuburi, Julius Mapo alisema ujenzi wa barabara ya Migombani inayoungisha hadi Segerea itakuwa mkombozi kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam wanaotumia njia hiyo.

“Ni njia ya mkato kama unataka kwenda Segerea au Gongo la Mboto, lakini kwa namna ilivyo sasa ni changamoto, hasa mvua ikinyesha, tunashukuru Serikali na viongozi kuiona na kuipa kipaumbele kwenye ujenzi,” alisema Mapo.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi