Kitaifa
Biteko: Hatuwezi kusema tatizo la umeme litakwisha lini
Dk Biteko amesema kuwa mbali na kuwekeza kwenye nishati ya jotoardhi, kuna maeneo ya Mkoa wa Shinyanga na Makambako mkoani Njombe kuna uwezekano mkubwa wa kupata umeme wa upepo na jua megawati 600, lakini changamoto ni uwekezaji wa miundombinu.
“Hatuwezi kutegemea chanzo kimoja cha nishati ya umeme, sasa tunakuja na maboresho ya upatikanaji wa nishati ambayo itaondoa changamoto ya kukatika kwa umeme wakati tukisubiri muda wa kuwashwa kwa mashine moja kwenye mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere kuingizwa kwenye gridi ya Taifa,” amesema.
Amesema Serikali imeamua kwa dhati kuendeleza miradi ya umeme wa jotoardhi kwa tayari wamedhamiria na Rais Samia kuanza na uzalishaji wa megawati 10 kati ya 60 kupitia mradi wa kampuni tanzu ya Shirika la Umeme ya TGDC kuharakisha kunatenga fedha haraka iwezekanavyo.
Dk Biteko amesema kuwa nchi ina vyanzo vingi vya umeme ambavyo havijapewa nguvu, sasa umefika wakati wa kuondokana nayo kwa kuongeza nguvu huku akibainisha kuwepo kwa mahitaji makubwa kutokana na ongezeko la watu na viwanda.
“Nimewaambia Tanesco kuhakikisha miradi ya jotoardhi inaanza kuboresha kwa kutengewa fedha, ili kuhama kwenye utegemezi wa chanzo kimoja cha kuzalisha nishati ya umeme,” amesema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya TGDC, Mathew Mwangomba amesema kwa sasa wako katika hatua nzuri huku akieleza zaidi ya dola milioni 75 za Marekani (Sh187.87 bilioni) zinahitajika kuhakikisha wanazalisha megawati 10 huku matarajio yakiwa ni megawati 60.
“Nikuhakikishie Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, mradi huu baada ya kupata fedha utatekelezwa kwa wakati na bado kuna kazi ya kuchoronga mita 1,500 mpaka 1, 900 ardhini ambako kuna nishati ya kiwango kikubwa,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema watahakikisha wanasimamia mradi huo kwa lengo na kuhakikisha Watanzania wanatoka kwenye hadha ya mgawo wa umeme.
Naye Mbunge wa Busokelo, Atupele Mwakibete amemwomba Waziri Biteko kuharakisha kukamilisha mradi huo, kwani una mahitaji makubwa kwa wananchi.
“Kuna changamoto kubwa za umeme katika Jimbo langu, nilijua ujio wako umeme matumaini sambamba na kuwepo kwa vyanzo vingine vya umeme ambavyo Serikali ikiwekeza taifa litakuwa na nishati ya kutosha,” amesema.