Kitaifa

Kadogosa: Mgawo sio kikwazo utendaji SGR

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wananchi wakitilia shaka namna treni ya umeme inavyoweza kufanya kazi kutokana na kukosekana uhakika wa upatikanaji wa nishati hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amefafanua itakavyofanya kazi.

Alisema treni hiyo itakuwa na njia yake maalumu ya kusafirishia umeme, hivyo kutoathirika na kukatika kwa umeme kunakoendelea.

Hivi sasa kuna vilio kutoka kwa wananchi kutokana na kukosekana umeme wa uhakika nchini jambo linaloathiri shughuli za kiuchumi na kijamii.

Baadhi ya maeneo wamekuwa na hisia kuwa wanakatiwa umeme zaidi ya mengine jambo linalowaumiza.

Kadogosa alitoa kauli hiyo alipohudhuria jukwaa lililolenga kuzungumzia umuhimu wa kuwapo kwa upatikanaji wa fedha endelevu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuwekeza kwenye mikakati ya kukabiliana nayo.

Jukwaa hilo liliandaliwa na Benki ya Standard Chartered ya jijini hapa na kushirikisha wadau mbalimbali.

Akizungumza katika jukwaa hilo Ijumaa iliyopita, Kadogosa alisema TRC haina tatizo wala hofu kwa kuwa wanayo njia maalumu ya usafirishaji umeme kwa ajili ya treni ambayo haifungamani na njia yoyote.

Alisema hiyo inawafanya kuwa na uhakika wa nishati na njia pekee inayoweza kufanya wakose umeme wa kuendeshea treni ni pale nchi nzima itakapokuwa gizani.

“Hata hivyo, sisi si watumiaji wakubwa wa umeme, watu wanadhani labda treni itatumia megawati 2,000 hapana, tuna imani kuwa umeme unaozalishwa na Tanesco na wanaotarajia kuingiza katika gridi utatosheleza sisi kuendesha treni,” alisema Kadogosa.

Alisema ikiwa umeme utakosekana nchi nzima na treni kushindwa kufanya kazi, katika maeneo yao ya maunganisho ya treni (shunting) kuna vichwa vya treni vinavyotumia dizeli ambavyo vinaweza kutumika kama mbadala.

“Baadaye tutakuwa na ‘hybrid’ ambazo tutaagiza hizi zitakuwa zikitumia umeme ikitokea dharura unaweza kubadili na kutumia mafuta,” alisema Kadogosa.

Alisema vichwa vya treni vya ‘hybrid’ pia vipo vya aina tofauti ikiwemo vilivyowekwa betri ambayo ina uwezo wa kujichaji kadri treni inavyofanya kazi na baadaye nishati hiyo inaweza kutumika kwa dharura pindi kunapokuwa na tatizo.

Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) katika kongamano hilo ulichaguliwa kuwa wa mfano, kutokana na namna utekelezaji wake ulivyoepuka uharibifu wa mazingira.

Wakati Kadogosa akisema hayo, wananchi wamekuwa wakiendelea kusubiri ufumbuzi wa tatizo la upungufu wa umeme unaosababisha mgawo, ambao Serikali imetoa ahadi mpya ikisema utaisha Machi mwaka huu.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Lupembe, Edwini Swalle bungeni wiki iliyopita alisema mgawo utaisha Machi baada majaribio ya mtambo namba tisa wa uzalishaji wa umeme kwenye Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) kufanikiwa juzi.

Awali, Februari Mosi, mwaka huu, akijibu maswali ya wabunge, Kapinga aliwataka wananchi wavumilie hadi Februari 16, akisema zitapatikana megawati 215 zitakazomaliza tatizo hilo.

“Naomba nilifahamishe Bunge lako tukufu kwamba, jana (juzi) tumefanikiwa kufanya majaribio kwa ukamilifu kwa mtambo kwa uwezo wake wa mwisho, yaani megawati 235,” alisema bungeni na kuongeza:

“Kama ambavyo tulisema ratiba ya awali itakamilika Februari 16, kwa siku ya jana tumefanikisha majaribio hayo kwa kiasi kikubwa. Hivi sasa wataalamu wetu wanaendelea na ‘fine tuning’ (marekebisho madogo) na kuweka ulinzi wa mitambo kwa ajili ya kwenda kwenye uzalishaji.”

Spika, Dk Tulia Ackson naye alihoji mgawo wa umeme utaisha lini?

Akijibu Kapinga alisema mgawo wa umeme unategemeana na matumizi ya kila siku ya nishati hiyo nchini na kuongeza:

“Kwa kweli mgawo utakuwa umepungua kwa kiasi kikubwa, lakini kwa sababu mtambo namba tisa utazalisha megawati 235 na namba nane utakaoanza uzalishaji Machi utazalisha megawati 235, jumla zitakuwa megawati 470. Uhakika ni kwamba kufikia Machi, mgawo wote utakuwa umeisha,” alisema.

Kero kwa wananchi

Mgawo wa umeme umekuwa kero kwa wananchi, huku baadhi ya wakazi wa maeneo tofauti jijini Dar es Salaam wakilalamikia ratiba ya mgawo kutofuatwa, huku wengine wakieleza maeneo yao yamekuwa yakiathiriwa zaidi.

“Eneo kama Tabata, hakuna ratiba maalumu ni kukatika umeme tu hujui ufanye nini, na ukikatika haijulikani utarudi saa ngapi ni hasara kwetu kama wafanyabiashara wadogo unaweza kupoteza mtaji wote kwa ajili ya umeme,” alisema Jenista Msangi, mfanyabiashara wa keki.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Besta Msasanuri, aliyetaka ratiba maalumu ya mgawo wa umeme kutolewa ili ikiwezekana watu wachelewe kufungua ofisi.

“Wengine kazi zetu ni umeme asilimia 100 bila umeme hakuna kazi sasa badala ya kuja kukaa hapa kupiga ramli bora tucheza na familia,” alisema Besta.

Kauli ya Tanesco

Msemaji wa Tanesco, Kenneth Boymanda alisema malalamiko ya watu yaliongezeka siku za karibu baada ya upungufu wa uzalishaji umeme kuongezeka kutokana na hitilafu zilizotokea katika baadhi ya mashine, zikiwamo zinazotumia gesi na maji.

Hali hiyo ilifanya hata baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa katika mgawo awali kukosa umeme kwani makadirio na ratiba inapopangwa inatumia makisio ya mashine zilizopo na mahitaji.

“Mashine zikiharibika zinaongeza upungufu lakini matengenezo yanaendelea na muda wowote kuanzia sasa zitarejea katika hali yake ya kawaida,” alisema Boymanda.

Pia alisema wakati mwingine majaribio ya mtambo namba tisa katika Bwawa la Julius Nyerere yamekuwa yakisababisha kukatika kwa umeme kwani umekuwa ukiingia na kutoka.

“Watu watuvumilie wakati tunamalizia majaribio ya mwisho ili tuiingize umeme katika gridi na kupunguza makali haya, hadi Machi tutakuwa katika hali nzuri,” alisema Boymanda.

SGR na nauli kwa abiria

Wakati Kadogosa akitoa hakiisho hilo kuhusu utendaji wa SGR, Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) inakamilisha, upangaji wa viwango vya nauli ya treni za mwendo wa haraka vitakavyotumika baada ya huduma kuanza rasmi kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Shirika la Reli Tanzania TRC lilipendekeza viwango mbalimbali vya nauli za abiria kwa treni ya SGR, huku Latra ikiitisha maoni ya wadau ikiwa ni utekelezaji wa kifungu Na 21 cha Sheria Na 3 ya Latra ya mwaka 2019.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi