Kitaifa
Bunge laazimia kufuta kigezo JKT kuwa kigezo cha ajira
Amesema JKT hawana uwezo wa kumchukua kila kijana anayetaka kwenda kwenye mafunzo hayo, hivyo wengi wanabaki.
“Wanaopata nafasi ni wachache na hao ndio wanapata nafasi ya kujiunga na vyombo hivi. Naomba kutoa hoja kigezo hiki kiondolewe. Lakini kwa sababu kwa sasa mchakato wa ajira unaendelea naomba mchakato huo usimamishwe,” amesema.
Mwanisongole amesema lengo ni vijana ambao hawakupata nafasi ya kuomba ajira hizo kwa sababu ya kigezo cha kutakiwa kwenda mafunzo ya JKT wapate fursa ya kuajiriwa.
Akichangia hoja hiyo, mbunge wa Viti Maalumu, Felister Njau amesema kigezo hicho kinapunguza wigo wa vijana wenye weledi na fani mbalimbali kuajirika kwenye vyombo hivyo.
“Vijana wote waende kwenye usaili na wale watakaopita, Serikali au taasisi ichukue jukumu la kuwapeleka kwenye mafunzo ya JKT. Tukiacha hivi ilivyo tatizo linakuwa kubwa kwa sababu huko mtaani kuna minong’ono, lakini hatuwatendei haki (vijana) kwa sababu wao hawana makosa,” amesema.
Rashid Shangazi (Mlalo), amesema jambo hilo ni baya kwa sababu linakiuka Katiba inayokataa ubaguzi.
“Serikali ya awamu ya kwanza na ya pili haikuwa na mapato makubwa, lakini bado iliweza kupeleka vijana wote waliomaliza kidato cha sita kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Ameshauri Serikali kuangalia kupunguza muda wa mafunzo kwa mujibu wa sheria kutoka miezi mitatu hadi mmoja, ili vijana wote waweze kuenda kama tatizo liko kwenye gharama.
Shangazi ameshauri Wizara ya Fedha kutoa fedha kwa JKT ili vijana wote wanaomaliza kidato cha sita waende kupata mafunzo muhimu yanayosaidia kutambua na kuelewa uzalendo kwa Taifa lao.
Wabunge wengine waliochangia ni Tabasamu Hamisi (Sengerema), Luhaga Mpina (Kisesa), Husna Saiboko, Dk Christian Mzava na Agness Marwa.
Mchango wa mawaziri
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini amesema Tume ya Haki Jinai eneo hilo imeelekeza mfumo wa ajira wa vyombo hivyo uboreshwe.
“Kwa vile taarifa hii ina maeneo mengi ya kufanyiwa kazi, tunaomba maelekezo yako yaende sambamba na kutekeleza maelekezo ya Tume ya Haki Jinai, ili kwa pamoja tuwe tumelikamilisha jambo hili kwa ukubwa wake,” amesema.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, amesema Serikali iko tayari kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Bunge.
Amesema vyombo vya ulinzi vina vigezo vya kutafuta vijana wanaohitajika kwenda kufanya kazi kwenye vyombo vyao ambavyo si kila Mtanzania anaweza kukidhi vigezo hivyo.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema kwa sababu hoja hiyo inafanyiwa kazi kupitia maoni yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai, baadaye mwongozo wa namna nzuri ya kutekeleza jambo hilo utatolewa.
“Niliombe Bunge likubali Serikali tulipokee jambo hili liunganishwe katika maoni yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai yafanyiwe kazi kwa pamoja, ili jibu litakapotoka liwe linajumuisha maoni ya watu wote,” amesema.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi ameomba jambo hilo walirudishe serikalini, ili wakalifanyie kazi.
“Tunaomba lirudishwe serikalini ili baadaye tuweze kuendelea na utaratibu huo lakini tukiwa tumezingatia zaidi mwongozo wa Bunge lako wa kulichukulia kwa umakini,” amesema.
Akihitimisha hoja, Mwanisongole amesema Tume ya Haki Jinai ilikataa ajira katika vyombo hivyo kutolewa kwa kigezo cha kupitia mafunzo ya JKT na JKU kwa sababu limekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi.
Amesema kwa sababu mchakato wa ajira wa Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Magereza na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) bado ulikuwa haujafika mbali, utangazwe upya ili vijana waliokosa nafasi kutokana na kigezo hicho wapate nafasi.
Spika, Dk Tulia Ackson amesema Bunge haliwezi kufanya maamuzi ya kusitisha mchakato wa ajira kwa sababu kwa kufanya hivyo ni kama kutunga sheria ambayo inakwenda nyuma.
“Hivyo tukifanya maamuzi leo ni kwa ajili ya yale yanayokuja na si kwa yale yaliyokwisha kutangazwa,” amesema.
Amesema ajira zilizokwisha kutangazwa na vyombo hivyo hazitahusika na hoja hiyo, lakini ajira zinazofuata zisimuonee Mtanzania yoyote.
Dk Tulia amesema wakati mafunzo ya JKT yalipositishwa, vyombo hivyo vilikuwa vikiajiri vijana na baadaye kuwapeleka kwenye mafunzo hayo.
Azimio la Bunge
Bunge limeazimia vijana wote wapewe fursa sawa za ajira pale wanapokuwa wametimiza masharti mengine yote yanayohusika na nafasi ya ajira husika isipokuwa cheti cha JKT na JKU.
Dk Tulia amesema Serikali ifanye hivyo hadi pale itakapokuwa na uwezo wa kuwapokea na kuwapa mafunzo ya JKT na JKU vijana wote wanaohitimu kidato cha nne na cha sita.
Ametaja sababu tatu ambazo zimewafanya kufikia maamuzi hayo kuwa ni JKT na JKU kutokuwa na uwezo wa kuwapokea na kuwafundisha vijana wote wanaohitimu kidato cha nne na cha sita.
Sababu nyingine ni uwepo wa uwezekano wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwapeleka katika mafunzo hayo watakaokuwa wameajiriwa kwa kuzingatia masharti ya msingi ya ajira husika.
Ametaja sababu nyingine ni uwepo wa vijana wenye uwezo wa kutimiza masharti ya ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama isipokuwa sharti la kupitia mafunzo hayo.
Aprili, 2019 hayati Rais John Magufuli alitoa ajira kwa vijana wa JKT zaidi ya 2,000 walioshiriki ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali.
Vijana hao ni walioshiriki kwenye ujenzi wa nyumba za Serikali, ukuta wa Ikulu ya Chamwino Dodoma, nyumba za magereza na wanaofanya kazi kwenye kiwanda cha kuchakata mahindi cha JKT Mlale.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mji wa kiserikali wa Ihumwa, Dodoma Aprili 13, Rais Magufuli alieleza kufurahishwa na kazi kubwa iliyofanywa na vijana hao kwa muda mfupi, gharama nafuu na moyo wa kujitoa kwa ajili ya Taifa lao.
Alielekeza vijana hao waajiriwe katika maeneo mbalimbali ikiwamo jeshini, usalama wa taifa, Takukuru, uhamiaji na taasisi nyingine za Serikali.