Kitaifa
Mamia wajitokeza tena kumuaga Lowassa Azania Front
Dar es Salaam. Mamia ya watu wameendelea kujitokeza kushiriki safari ya mwisho hapa duniani ya Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Lowassa (70) katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Azania Front, Dar es Salaam.
Umati huo ni sawa na ule uliojitokeza jana Jumanne, Februari 13, 2024 viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam ambapo mwili wa Lowassa uliagwa kitaifa na waombolezaji mbalimbali kushiriki wakiongozwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.
Leo Jumatano watu wamejitokeza kwa wingi kanisani hapo inapofanyika ibada ya kuaga mwili wa mwanasiasa huyo. Hapo ndipo alikuwa akisali enzi za uhai wake awapo jijini Dar es Salaam.
Saa 4:52 asubuhi, gari lililobeba jeneza la Lowassa limewasili kanisani hapo tayari kuanza kwa ibada hiyo.
Lowassa aliyefariki dunia Februari 10, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ndiye alitangaza kifo hicho kwa niaba ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Dk Mpango alisema, Lowassa alifariki baada ya kuugua magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.
Katika Kanisa la Azania Front na viunga vyake tayari kuna idadi kubwa ya watu waliojitokeza kushiriki ibada hiyo na kisha kumuaga, ikiwa ni fursa ya mwisho kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kabla ya kesho Alhamisi kusafirishwa kuelekea jijini Arusha.
Ibada hii ya mwisho kwa Lowassa jijini Dar es Salaam itaongozwa na Mkuu wa KKKT Askofu Alex Malasusa katika usharika huo.
Viongozi mbalimbali wa Serikali na wastaafu wamejitokeza katika ibada hiyo akiwemo Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba na Mkuu wa Majeshi mstaafu Jenerali Davis Mwamunyange.
Wengine ni aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Andrew Chenge na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.
Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa.
Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967. Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 – 1971, kabla ya kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka 1972–1973.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu na baadaye Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).
Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.
Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.
Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.
Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge wa Monduli mwaka 1990 na 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.
Katika uchaguzi mkuu 2005, Jakaya Kikwete aliibuka mshindi wa nafasi ya urais na alipounda Serikali, alimteua Edward Lowassa, Desemba mwaka huo kuwa Waziri Mkuu. Nafasi hiyo aliihudumu hadi Februari 7, 2008 alipotangaza kujiuzulu nafasi hiyo.
Hii ilitokana na tatizo kubwa la uhaba wa umeme na Serikali kulazimika kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo, zikiwamo zilizodaiwa kukiuka taratibu na sheria.
Baada ya kashfa hiyo kuchunguzwa na taarifa kutolewa bungeni, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alilazimika kujiuzulu baada ya kutakiwa ajipime kutokana na mazingira ya kashfa hiyo.
Wengine waliong’oka madarakani ni mawaziri wa nishati na madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.
Lowassa alikuwa mbunge wa Monduli hadi 2015. Mwaka huo alihamia Chadema na kuwania urais na kushika nafasi ya pili nyuma ya John Magufuli wa CCM aliyeibuka mshindi.
Mwaka 2019, Lowassa alitangaza kurejea tena CCM.