Makala

Mabibo, mabaki viwanda vya sukari kuzalisha umeme na ethano

Dar es Salaam. Zaidi ya Sh2 bilioni zinatarajiwa kutumika katika uzalishaji wa mafuta ya ethano yanayotumika kama nishati safi ya kupikia kupitia mabaki yanayotokana na uzalishaji wa sukari, mabibo, mihogo na katani.

Fedha hizo pia zitatumika kuongeza uzalishaji wa umeme utakaoletwa katika gridi ya Taifa kupitia baadhi ya viwanda vya sukari vilivyopo nchini na kuweka ruzuku katika majiko yanayotumia ethano.

Fedha hizo zimetolewa na Shirika la kimataifa la maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kupitia Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), huku baadhi ya wanufaika ikiwa ni kiwanda cha sukari TPC, Bagamoyo, Mayara, Zanzibar sugar na kampuni ya Consumer Multichoice.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi kwa wanufaika, leo Jumanne, Februari 13, 2024 Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo wa TIB, Joseph Chilambo amesema kwa kushirikiana na UNIDO wamekuja na mpango mpya wa matumizi ya nishati ya ethano inayotengenezwa kutokana na mabaki ya mazao ikiwemo katika uzalishaji wa sukari, mabibo.

“Mabaki katika utengenezaji wa sukari, mabibo ya korosho yanatumika kutegeneza ethano ambayo ni nishati mbadala inayotumika katika kupikia isiyotoa moshi na miti haikatwi, jambo ambalo linaacha mazingira salama na watu kuwa salama,” anasema Chilambo.

Amesema kutolewa kwa fedha hizo kunalenga kupunguza hewa ukaa na uharibifu wa mazingira katika kukata kuni na kuchoma mkaa.

Pia ni fursa kwa viwanda, kwani baadhi ya wafanyabiashara watakwenda kuanzisha viwanda kwa ajili ya kutengeneza ethano itakayokuwa ikitumiwa na Watanzania katika kupikia.

Mratibu wa miradi ya nishati na mazingira kutoka UNIDO, Victor Akim amesema miradi hiyo inalenga kulinda na kuboresha mazingira kwa kutumia taka katika uzalishaji wa nishati ya kupikia na umeme.

“Mradi mwingine unasaidia viwanda vya kilimo ambavyo vinazalisha umeme kutokana na taka wanazozalisha katika viwanda vyao, pia watazalisha ethano ambayo inatokana na mabaki katika uzalishaji sukari,” amesema Akim.

Ofisa Mtendaji wa Utawala wa kampuni ya sukari TPC, Jafari Ally amesema wamekuwa wakitumia mabaki ya miwa katika kuzalisha ueme megawati 17.5 ambapo megawatt 13 wamekuwa wakitumia wao na kinachobakia wanapeleka katika gridi ya Taifa.

“Kupitia fedha tulizopewa, tutakwenda kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha umeme, kwani tunakwenda kuwekeza mitambo mingine na kuweka kiwanda kingine cha ethano,” amesema Ally.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Consumer Choice’s, Frida Mlingi ambayo imepewa ruzuku kwa ajili kusambaza majiko yanayotumia ethano katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Dodoma na Mwanza, amesema wanaamini ndani ya miezi 17 waliyopewa watapunguza matumizi ya kuni na mkaa.

“Tuna dhamana ya kusambaza majiko 6,000 ndani ya miezi 17 kuanzia Agosti mwaka jana, tunaendelea vizuri hasa kwa jiji la Dar es Salaam na majiko zaidi ya 300 yameshasambazwa, pia tuna mradi mwingine wa kusambaza majiko 20,000 kwa miezi 36 jijini hapa kuanzia sasa,” amesema Frida.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi