Kitaifa
Kero za Muungano sasa zasalia tatu
Dodoma. Serikali imesema tangu mwaka 2006, hoja 22 kati 25 zilizopokewa na Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja na Muungano.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo, leo Ijumaa Februari 9, 2024 amesema hayo alipojibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalumu, Najma Murtaza Giga.
iga amehoji kuna mikakati gani kuhakikisha changamoto za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi hazileti madhara nchini na lini zitapatiwa ufumbuzi.
Akijibu swali hilo, Jafo amesema tangu kuanzishwa kwa Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya kushughulikia kero za Muungano mwaka 2006, hoja 25 zimepokewa na kujadiliwa kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.
Amesema kati ya hoja hizo, 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja na Muungano.
“Hoja zilizobakia zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi na kwa kuwa Serikali zetu zote mbili SJMT na SMZ zina nia na dhamira ya dhati ya kuhakikisha mambo yote yanayoleta changamoto katika utekelezaji wa masuala ya Muungano yanapatiwa ufumbuzi, tunaamini hoja hizo zitapatiwa ufumbuzi hivi karibuni,” amesema.
Amesema Muungano umeendelea kuimarika na mwaka huu wanaadhimisha miaka 60 tangu kuasisiwa kwake mwaka 1964, na huo ni ushahidi kwamba Serikali zimefanya kazi kubwa na ya kutukuka.