Connect with us

Kitaifa

Akili bandia yaibua mjadala bungeni

Dodoma. Matumizi ya akili bandia (AI) yamewaibua wabunge, huku Mbunge wa  Kawe, Josephat Gwajima alihoji Serikali itawapeleka wapi wataalamu wanaowasomesha itakapofika kila kazi inafanywa na roboti.

Maswali kuhusu akili bandia yameulizwa leo Ijumaa Februari 9, 2024 na wabunge wengine wa viti maalumu, Esther Matiko na Neema Lugangira.

Gwajima, ambaye pia ni Askofu amesema Serikali matumizi ya roboti yanalenga kutatua tatizo la upungufu wa watu duniani kwa nchi za Magharibi ambazo idadi ya watu ni wachache.

“Huku kwetu Tanzania bado kuna watu wengi sana, sasa itakuwaje tutakapofika wakati mwalimu roboti, daktari roboti, tutawapeleka wapi watu ambao tumewafundisha leo. Je, Serikali imejiandaaje baada ya roboti kuwa imechukua ukanda wa ajira zote?” amehoji.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kazi ya wizara ni kuandaa sheria, taratibu, taasisi na uwekezaji ili Tanzania ipate faida katika matumizi ya akili bandia badala ya kupata hasara.

Amesema Bunge lina wajibu wa kuhakikisha sheria zinatungwa, taratibu zinawekwa ili wale watakaopoteza ajira kuwe na namna ambayo watashughulikiwa.

“Ila tuliandae Taifa letu kwamba haya mabadiliko yana fursa ndani yake na ndiyo maana tunawafundisha watoto wetu na kuandaa vyuo kwa sababu haya mapinduzi hayakwepeki, lazima tujiandae kuenda mbele,” amesema Nape.

Neema amesema zipo athari kubwa katika uchaguzi, shuleni na maeneo mengine ambayo watatumia akili bandia kuandaa tafiti.

“Je, waziri husika yuko tayari kuandaa kanuni ambazo zitawalinda Watanzania juu ya matumizi hasi ya akili bandia,” amehoji.

Nape katika majibu ya swali hilo amesema suala la hasara na faida za akili bandia haliwezi kushughulikiwa kwa sheria moja na kwamba, Serikali iko tayari kutengeneza kanuni wakati ikisubiri mabadiliko makubwa ili jamii iendelee kuwa salama, lakini ifaidike na matumizi ya akili bandia.

Kwa upande wake, Esther amehoji Serikali imejipangaje kimkakati kupeleka wataalamu wa akili bandia katika maeneo kama vile mahakama na polisi kukabiliana na madhara hasi ya akili bandia.

Waziri Nape amesema wanafundisha wataalamu na kwa mwaka huu itafundisha watumishi wa Serikali kutoka maeneo 500.

Amesema wataalamu hao watajifunza ndani na nje ya nchi na pia wanaanzisha vyuo vya Tehama katika mikoa ya Dodoma na Kigoma.

Amesema pia kutawekwa vituo vinane nchini ambako watu wataweza kupata mafunzo ya akili bandia.

“Wito wangu tusifikirie mabaya na changamoto pekee kwenye matumizi ya akili bandia, badala yake tuangalie faida zitakazopatikana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na uchumi wetu,” amesema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi