Connect with us

Kitaifa

Mbunge ataka picha ya Rais Samia iwekwe kwenye fedha

Dodoma. Mbunge wa viti maalumu, Ng’wasi Kamani ameihoji Serikali kuwa, haioni haja ya yakuweka kumbukumbu ya kudumu ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye fedha za Tanzania.

Kamani amehoji hayo leo Alhamisi Februari 8, 2023 katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri wa Mkuu Kassim Majaliwa bungeni.

Mbunge huyo amesema mwaka 2006 Bunge lilipitisha Sheria ya Benki ya Tanzania ambayo chini ya kifungu cha 27 (1b), inaipa mamlaka benki hiyo kutengeneza (ku-design) fedha kwa kuweka nembo na mambo mbalimbali.

Amesema mwaka 2021 Tanzania imepata Rais wake wa kwanza mwanamke anayefanya kazi nzuri na anatambulika duniani kama madhubuti na wa mfano.

Kamani  amesema anatambua kuwa Bunge la Marekani liko katika utaratibu wa kupitisha sheria itakayowezesha Harriet Tubman ambaye ni mwanamama na mwanaharakati aliyefanya kazi kubwa katika vita ya utumwa kumweka kwenye Dola 20 kama kumbukumbu.

“Na natambua katika bara letu la Afrika nchi kama Nigeria, Malawi na Tunisia zimekwisha fanya hatua hizi na zimetambuliwa na Benki ya Dunia na IMF (Shirika la Fedha Duniani) kama hatua ya uelekeo unaofaa.

“Je Serikali haioni haja ya kuweka kumbukumbu ya kudumu kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka picha yake katika fedha za nchi hii?” amehoji Kamani.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema awali suala la uwekaji wa picha za viongozi mbalimbali katika fedha lilikuwa ni uamuzi uliofanyika kwa lengo la kukumbuka mchango wa viongozi hao nchini hasa zinazotumika sasa za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume.

“Ni kutambua mchangao wao walioutoa katika Taifa hili, kwa hiyo picha zao zilitumika kama sehemu ya kumbukumbu na tunazo aina ya fedha za noti na sarafu tunazotumia kuweka alama za wanyama wetu, hii ilikuwa ni kuenzi tunu ya Taifa lakini pia kuboresha hamasa kwenye utalii,” amesema Majaliwa.

Amesema mara nyingi uamuzi wa kuweka picha  hufanywa na kiongozi mwenyewe kwa kushirikiana na Benki Kuu (BoT),  kwa sababu mbunge huyo ameleta hoja hiyo na wao  wanatambua mchango mkubwa uliotolewa na Rais Samia, wameupokea ushauri huo.

“Niseme kuwa tumeupokea ushauri wako na litaingia serikalini na litajadiliwa, watafanya maamuzi kwa kushauriana na Benki Kuu taarifa hizi zitatolewa rasmi,” amesema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi