Connect with us

Kitaifa

Bunge laishukia Serikali kwa kero ya umeme

Dodoma. Wakati upungufu wa umeme ukiwa ni dhahiri na Serikali ikisema umefikia megawati 193 kutoka 400, Bunge limeitaka ihakikishe mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) unakamilika haraka na kuanza uzalishaji kuanzia mwezi huu Februari 2024 kama ilivyoahidi.

Mbali na hilo, Bunge hilo limeazimiakuwa Serikali iongeze idadi na mtandao wa vituo vya kujaza gesi kwenye magari nchini, ikianza na maeneo ambayo taratibu za awali za ujenzi zilikuwa zimeanza.

Hata hivyo, licha ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kulieleza Bunge kuwa kwa sasa upungufu wa umeme umebaki megawati 193, hali ya upatikanaji wa nishati hiyo katika maeneo mbalimbali nchini bado ni changamoro, kukatika kwake mara kwa mara kumeendelea kuonekana maeneo mengi.

Mgao huo ulianza Septemba mwaka 2023 kutokana na upungufu wa uzalishaji wa umeme katika vyanzo vikiwemo vya maji uliosababishwa na mabwawa yakiwemo Kihansi, Mtera na Kidatu kupungua uwezo wa uzalishaji, huku ikielezwa pia kulikuwa na metengenezo ya mitambo na njia za kuusafirisha.

Kutokana na kadhia hiyo, Septemba 25, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alimpa miezi sita bosi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Gissima Nyamo-Hanga, kuhakikisha umeme wa uhakiki unapatikana nchini.

Alimtaka Nyamo-Hanga aliyechukua nafasi ya Maharage Chande aliyehamishiwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na baadaye Shirika la Posta, kulifanya jambo hilo kama kazi yake ya kwanza ndani ya Tanesco.

Miezi hiyo sita itatamatika Machi 25, mwaka huu huku hali ya mgao ikiwa bado inaendelea.

Mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, Mariam Abdallah akizungumza na gazeti hili leo Februari 6, 2024 amesema, “mgao bado unaendelea, hakuna nafuu yoyote kwani hali ni ileile.”

Anachokieleza Mariam ndicho kiko kwenye maeneo mbalimbali nchini huku wafanyabiashara wanaotegemea umeme kutekeleza majukumu yao, wakikutana na changamoto kwenye biashara zao.

Mapema leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk Mathayo David amewasilisha taarifa ya shughuli za kamati yake kwa mwaka 2023 na kutoa mapendekezo ya kutaka Serikali kukamilisha mradi huo Februari mwaka huu, hoja ambayo imeridhiwa na Bunge.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Dk Mathayo amesema taarifa iliyowasilishwa kwenye kamati Januari, mwaka 2024 ilionyesha mradi huo umefikia asilimia 95.83 na kuwa tayari malipo ya Sh5.85 trilioni sawa na asilimia 89.24 yalikuwa yamefanyika.

Amesema hali ya usambazaji na upatikanaji wa umeme nchini si ya kuridhisha kutokana na ukame, uhaba wa gesi, uchakavu wa miundombinu na uchache wa vituo vya kupoza umeme.

Amesema hali hiyo inaathiri uzalishaji wa bidhaa na huduma nchini na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi na kuchangia ongezeko la mfumuko wa bei.

“Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali ihakikishe mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP) unakamilika haraka na kuanza uzalishaji kuanzia Februari, 2024 kama ilivyoahidi,” amesema, Dk Mathayo.

Baadaye Naibu Spika, Mussa Zungu amelihoji Bunge, likapitisha azimio hilo kwa sauti moja. Kwa maana hiyo zimesalia siku 22 na ukamilishaji mradi huo na kuanza kutumika.

Januari 13 mwaka huu, Tanesco ilitoa taarifa kwa umma ikieleza awamu ya pili ya kuunganisha kituo kipya cha kupoza umeme cha kilovoti 400 cha Chalinze na njia ya msongo wa kilovoti 220 inayoanzia Luguruni hadi Morogoro.

Taarifa hiyo ilieleza, kazi hiyo itakapokamilika itaongeza uwezo wa kituo cha kilovoti 440 Chalinze kupokea umeme utakaozalishwa kutoka kwenye mitambo ya JNHPP na kuingia kwenye Gridi ya Taifa. Shughuli ilikuwa ihitimishwe Januari 21, mwaka huu kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Mtera yampa wasiwasi mbunge

Akichangia taarifa hiyo, Mbunge wa Kuteuliwa, Riziki Lulida alisema mvua zilipokuwa zinanyesha kwa wingi mkoani Mbeya, kamati hiyo ilipita Bwawa la Mtera na hakukuwa na maji, lakini pembeni ambako kuna wavuvi, maji yalikuwa ni mengi.

“Mimi nikajiuliza maswali, hiki nini ninachokiona? Hii hali sio ya kuiachia Naibu Spika. Hii ni hatari kubwa kwa nchi. Tukitegemea michezo hiyo, hii nchi itaingia katika giza ambalo tutategemea kununua majenereta na vitu ambavyo vitamuathiri Mtanzania,” alisema.

Amesema unapozungumzia mabadiliko ya tabianchi na watu wanacheza na mifumo ya maji kwenye mabwawa ya uzalishaji wa umeme, inamaanisha hata bwawa la JNHPP halitafanya kazi na itakuwa historia.

Amesema wapo watu walisema bwawa hilo halitafanya kazi na hivyo akawataka Watanzania kuchukua hatua ya kuhakikisha JNHPP linafanya kazi.

Gesi kwenye magari nayo shida

Katika taarifa hiyo ya kamati, Dk Mathayo amesema magari yanayotumia gesi asilia yaliongezeka nchini kutoka takribani 1,139 mwaka 2020/2021 hadi kufikia takribani 3,000 mwaka 2022/2023.

Hali hiyo, amesema ilisababishwa na unafuu wa gesi wa takribani asilimia 40 ikilinganishwa na mafuta hususan katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Mtwara.

Ongezeko hilo limesababisha foleni kwenye vituo vitano vya kujaza gesi vilivyopo nchini na hivyo wenye magari kulazimika kutumia muda mwingi katika kujaza gesi, ameeleza Dk Mathayo.

Katika hoja hiyo Bunge pia limeazimia kwamba Serikali iongeze idadi na mtandao wa vituo vya kujaza gesi kwenye magari nchini kwa kuanza na maeneo ambayo taratibu za awali za ujenzi zimeanza kama Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na vituo vya GPSA.

Akifafanua tatizo jingine, Dk Mathayo amesema baadhi ya wamiliki wa magari wanashindwa kuweka mfumo wa kutumia gesi asilia kwenye magari kutokana na gharama kuwa kubwa ya Sh2 milioni kwa gari, uchache wa wakaguzi wa mfumo nchini ambao wako 10 na uchache wa karakana.

Bunge vilevile limeitaka Serikali ichukue hatua zitakazowezesha kupunguza gharama za kufunga mfumo wa kutumia gesi kwenye magari na kuongeza idadi ya wakaguzi.

Akichangia taarifa hiyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda amesema kama matumizi ya gesi katika magari ni nafuu kuliko mafuta, kwa nini Serikali isiweke msisitizo katika kuongeza vituo vya ujazaji wa gesi na magari yanayotumia nishati hiyo?

Ametoa mfano wa gari dogo kuwa likiwekwa gesi ya Sh16,000 linaweza kusafiri umbali wa kilometa 200 lakini hilohilo likitaka kusafiri kwa umbali huo kwa kutumia mafuta, litalazimika kutumia si chini ya Sh60,000.

Ng’enda ameitaka Serikali ambayo ni mdau mkubwa wa matumizi ya mafuta, iwe mfano na kwamba wanatarajia mwaka ujao wa fedha itaahiza magari ya kutumia gesi badala ya mafuta ili iwe mdau wa kwanza wa matumizi ya nishati hiyo.

Mbunge wa Bunda Mwita Getere ametaka Serikali kuweka ruzuku kwa kampuni zinazozalisha gesi asilia ili wananchi waweze kupata huduma hiyo kwa urahisi.

Juhudi zinafanyika

Akifafanua baadhi ya hoja za wabunge, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema sababu za kukatika kwa umeme ni upungufu wa umeme na miundombinu ya kusafirisha umeme huo.

Amesema Serikali imefanya juhudi kubwa kwa kuangalia mawanda mapana ya vyanzo vya kuzalisha umeme vina hali gani.

“Utaona hatua ya kwanza tutakayozungumza tutalitaja Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere kama suluhu ya kwanza ya muda mrefu kwa ajili ya kutusaidia tatizo la upungufu wa umeme,” amesema.

Amesema hadi jana hali ya umeme iliyopo nchini baada ya mvua kunyesha, ukarabati wa mitambo na kuongeza mgandamizo wa gesi, upungufu umepungua hadi kufikia megawati 193 kutoka megawati 400.

Dk Biteko amesema maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme yalikuwa yamepungua sana lakini hivi sasa yameongezeka.

“Mtera kwa mfano ambayo ilishuka mpaka ikafika mita 689, kwa taarifa ya leo (jana), tumefika mita 695, bado mita tatu tufike kwenye kiwango cha juu kabisa cha uzalishaji wa umeme,” amesema.

Kwa upande wa changamoto ya miundombinu, Dk Biteko amesema ni ukweli kwamba kunahitajika muda kuwekeza na kusimamia hiyo miundombinu na kutoa mfano wa kujenga njia moja ya kusafirisha umeme mwingi kwa muda si chini ya miezi 12.

“Nchi hii tuna vituo vya kupoza umeme pungufu ya mahitaji, tunahitaji kwa nchi nzima zaidi ya vituo 231 lakini vipo 171, tuna njia ndefu, hivyo kukitokea hitilafu mahali fulani hata kama ni tawi lakianguka litawatoa wananchi wengi kwenye gridi,” amesema.

Aidha, Dk Biteko amesema wakati mwingine changamoto za kukatika kwa umeme huwa zinatokana na wizi wa vifaa na kutoa mfano katika kipindi kifupi mikoa ya Pwani na Dar es Salaam iliibiwa transfoma zaidi ya 87

“Ikiibiwa (transfoma) itawatoa wananchi wengi sana kwenye umeme lakini wananchi watakachokiona ni kwamba ni tatizo la Tanesco.

Onyo kwa wezi

“Nataka niwahakikishie kwamba wale wote wanaodhani kwamba wataendelea na mchezo wa kuiba transfoma, kuhujumu transfoma siku zao zinahesabika na wakitaka kujua hilo awaangalie wale ambao tumewakamata, hatua gani zimechukuliwa.”

Kuhusu gesi, Dk Biteko amesema ni kweli gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme inahitajika lakini mgandamizo wake umepungua.

Hata hivyo, amesema ipo miradi mbalimbali ya ujenzi wa mabomba ya gesi inaendelea nchini ili ipatikane gesi ya kutosha na kwamba hawajaacha miradi mingine itakayowezesha uzalishaji wa umeme.

Pia Dk Biteko amesema uzembe ndani ya Tanesco hauvumiliki na kwamba wameendelee kuchukua hatua kwa wanaobainika, ingawa hazisemwi hadharani.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi