Makala
Athari kwa wanaume kutobadilisha ‘boksa’ hii hapa
Kumekuwa na malalamiko katika kadamnasi au mikusanyiko mbalimbali, hususan kwenye daladala kuhusu baadhi ya wanaume kutofua nguo zao za ndani na hata kufikia hatua kuzionyesha mbele za watu zikiwa chafu hadi kufikia hatua ya kubadilika rangi.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ni hatari kutobadili nguo za ndani zinazofunikwa kwa muda mrefu bila kupata hewa, hivyo kuzalisha bakteria wanaotokana na unyevu wa jasho na kusababisha magonjwa ya ngozi pamoja na via vya uzazi.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wakazi wa Dar es Salaam wametoa maoni yao kuhusu hilo, akiwemo Pascal Zebedayo anayesema kurudia nguo za ndani bila kufua ni hulka ya mtu kutokana na yeye mwenyewe alivyozoea.
“Nairudia mpaka siku tatu ndiyo naona hapa imechafuka, kuna wakati naweza kukaa hata wiki kutokana na kazi ninazofanya, naamka alfajiri kuwahi mzigo narudi saa mbili usiku nikiwa nimechoka naoga nalala,” anasema.
Zebedayo, ambaye ni mfanyabiashara wa mitumba eneo la Karume, anasema wanaume wengi ambao wanaishi bila wake, suala la kutobadilisha nguo ya ndani akivaa kwa siku moja au mbili ni jambo la kawaida, tofauti na waliooa ambao husaidiwa na wake zao kufanya usafi.
Lodrick Mwale, mkazi wa Tandika anasema amenunua boksa tatu, zikichafuka hana muda wa kuzifua, hivyo huamua kuifanya kaptula kuwa nguo ya ndani mpaka atakapoona amepata muda wa kuzifua ndiyo atabadilisha. Anasema hata kaptula akiivaa huivaa kwa muda mpaka atakapohisi inatoa harufu ndipo ataifua.
“Tuna kimbizana na maisha, hatuna muda wa kufikiria kufua nguo za ndani, yaani za nje zitutese na za ndani pia, ukiona mtazamo wa sebule unapendeza unatosha, wa chumbani hautakusaidia chochote,” anasema Mwale.
Alizungumzia hilo, mkazi wa Mbezi, Frank Shirima anasema mara zote nguo zake hufuliwa na mke wake, hivyo haoni shida ya kubadilisha.
“Wakati nasoma chuo sikuwa na tabia ya kufua nguo zangu za ndani, mpenzi wangu akawa ananisema lakini sikubadilika kwa sababu ya uvivu na nilipomuoa kazi za kufua sasa anafanya mwenyewe na ndiye aliyenifanya niwe nabadili kila siku. Nisipofanya hivyo, ananisema sana,” anasema Shirima huku akiangua kicheko.
Wanawake nao hawakusita kulizungumzia hilo. Mkazi wa Segerea, Queen Kaloli anasema tatizo la kutofua nguo za ndani haliko kwa wanaume pekee, bali hata baadhi ya wanawake wanalo.
Anasema baadhi wakiingia kwenye hedhi kwa sababu tu hutumia taulo za hedhi akienda kuibadili na akakuta chupi haijachafuka, anirudia tena kuivaa siku ya pili.
“Wapo wanawake wa hivi, ukimuuliza anasema uchafu umezuiwa na taulo haujaifikia chupi,” anasema mwanadada huyo.
Hata hivyo, anasema kwa upande wake asipofua chupi anawashwa sehemu za maungio ya mwili, hivyo hulazimika kuibadili kila siku na ikibidi kila baada ya saa kadhaa kupita ndani ya siku.
Mkazi wa Gongo la Mboto, Jackline Materu anasema kwenye familia wana tabia ya kurundika chupi baada ya kuvaa na huzifua kila baada ya wiki.
“Lakini nilipoolewa, tuliweka utaratibu ambao mimi na mume wangu tunautumia, hata kama sipo kama tumezirundika, Jumamosi anazifua zote na kuzianika juani. Utartibu huu tumewaambukiza hadi watoto wetu na wao wanafanya hivyo,” anasema Jackline.
Zainabu Ali, mkazi wa Kigogo anasema hapendi kuvaa chupi kwa sababu zinamuwasha na wakati mwingine anavaa anapokwenda matembezini na anaporudi anairudisha kabatini bila kuifua.
Kauli za wataalamu
Daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi, Dk Ramadhan Mohamed anasema kuna madhara yatokanayo na kutobadilishwa kwa chupi kwa jinsia zote mbili.
Anataja madhara hayo kuwa ni pamoja na kupata maambukizo ya kwenye njia ya mkojo (UTI) na fangasi.
“Kuna watu wanapata UTI kwa njia nyingine, lakini wapo wanaopata ugonjwa huu kwa sababu ya kutokubadilisha chupi zaidi ya siku mbili, joto huzalisha bakteria wanaopendelea kuishi kwenye unyevunyevu,” anasema.
Anasema baadhi ya wenza hulaumiana pindi mmoja akiugua ugonjwa huo akidhani ameupata baada ya kuchepuka, lakini anasema chanzo kimojawapo cha UTI ni uvaaji wa chupi au boksa kwa muda mrefu bila kuifua.
Akizungumzia maambukizo ya fangasi sehemu za siri, Dk Ramadhan anasema husababishwa pia na kuvaa chupi kwa muda.
Anasema wengine hutumia maji wakati wa kutawaza na hajifuti, ile hali ya unyevunyevu inaenda kutengeneza fangasi kutokana na uvundo wa nguo ya ndani.
Mtaalamu huyo anasema nguo hizo pia husababisha muwasho, vipele na wengie huota ukurutu na kusababisha kutoka vidonda au kutengeneza michubuko sehemu za siri. “Mimi huwa nawatibu watu magonjwa ya ngozi, nikimpatia dawa akizitumia kwa usahihi, hupona lakini huwa nashangaa anarudi tena baada ya wiki mbili hali ikiwa imemrudia, nikimuuliza utaratibu wa uvaaji wa nguo za ndani, majibu yake ananiambia huwa akiivaa zaidi ya siku tatu bila kuibadili,” anasema daktari huyo.
Anasema kwa wanawake, wanatakiwa kuvaa chupi kila baada ya saa nane ili kuepuka athari zilizotajwa.