Kitaifa
Mbunge ataka nyongeza ya mafao kwa wastaafu
Dodoma. Mbunge wa Segerea Bonnah Kamoli ameihoji Serikali ni lini itaongeza malipo ya pensheni kwa wastaafu ya kila mwezi kama ilivyofanyika kwa Zanzibar.
Kamoli ameuliza swali hilo la nyongeza bungeni leo Februari 5, 2023 ambapo amesema pia bado kuna baadhi ya wastaafu wanalalamika hawapati malipo ya kila mwezi.
“Wastaafu wa Zanzibar wameshaongezewa (kiwango) je, Serikali ina mpango gani kwa hapa kwetu Tanzania ili waweze kuongezewa hayo malipo,”amehoji Bonnah.
Akijibu swali Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema changamoto hiyo ya ucheleweshaji wa malipo kwa wastaafu iliisha baada ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.
Kuhusu kuongezwa kwa mafao kwa upande wa Zanzibar, Katambi amesema suala la mifuko ya jamii si la Muungano na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutangulia kuongeza viwango vya mafao.
“Lakini na sisi tuko tayari kwenye hatua nzuri ya kufanya tathimini ya uhimilivu ambayo itaangalia taarifa ya ustamilivu wa mifuko, kuangalia kiwango cha upatikanaji wa mafao kama kimepanda. Miaka mitatu ya kufanya tathimini ya uhimilivu tayari imetimia na tayari tuko katika hatua hiyo,”amesema.
Katika swali la msingi Bonnah amehoji ni lini kanuni mpya za malipo ya pensheni ya kila mwezi kutoka asilimia 50 hadi 67 itaanza kutumika.
Akijibu swali hilo, Katambi amesema amesema kiwango cha malipo hayo kilianza kutumika Julai mwaka 2022.
“Kanuni ziliandaliwa kwa kushirikisha wadau wote kwa lengo la kufanya maboresho ili kuwainisha mafao ya wanachama na kufanya mfuko kuwa endelevu,”amesema Katambi.