Makala

Chumvi, kitunguu saumu hatari kutibu ‘red eyes’

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya na madaktari bingwa wa macho wamesema wanapokea idadi kubwa ya wagonjwa wakiwa katika hali ya ugonjwa mkali, kutokana na matumizi ya njia mbadala kutibu macho, ikiwamo matumizi ya mkojo na chumvi.

Hali hiyo imebainika siku 15 tangu kutangazwa kuibuka ugonjwa huo ujulikanao viral keratoconjunctivitis (red eyes) Januari 13, 2024 mkoani Dar es Salaam.

Wataalamu waliozungumza na Mwananchi Digital leo Januari 28, 2024 wameeleza wagonjwa wanaotumia chumvi, mkojo, chai ya rangi na kitunguu saumu kama tiba, macho yao huvimba na kuuma zaidi pamoja na kupatwa homa. Athari hasi zaidi zinazotajwa ni kusababisha vidonda kwenye kioo cha jicho.

Tiba hizo mbadala zinaelezwa zinaweza kusababisha kovu kwenye jicho litakalomfanya mgonjwa apate uoni hafifu au kupoteze uwezo wa kuona kabisa.

Daktari bingwa na mkuu wa kitengo cha macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Sarah Mrema ameisema idadi ya wagonjwa wanaohudhuria hospitalini hapo kutibiwa macho imekuwa ikiongezeka na kupungua.

Amesema wamekuwa wakipokea wagonjwa wakiwa tayari walianza kutumia tiba za majani ya chai, vitunguu saumu na chai ya rangi.

“Si kwamba wanapona wakitumia tiba mbadala, maumivu yanazidi, wakija hapa wanakuwa na maumivu makali. Ukihoji anakwambia alitumia mkojo, chumvi na njia nyingine nyingi. Unampa dawa anatumia, kisha anapona,” amesema Dk Sarah.

Kwa mujibu wa Dk Sarah, takwimu za hospitali hiyo zinaonyesha tangu Desemba 22, 2023 wagonjwa 105 walifika kutibiwa na kuna siku orodha ya wagonjwa inapanda na siku nyingine inapungua.

Daktari bingwa wa macho katika Hospitali ya Muhimbili-Upanga, Neema Moshi amesema unapotumia vitu vikali kutibu macho, ni rahisi kuharibu kioo cha mbele cha jicho na maumivu yanayotokea huwa makali.

Amesema wakati mwingine unaweza kupoteza uoni kwa sababu ya kuharibu kioo hicho.

“Tunapokea wagonjwa wengine wana hali mbaya, lakini hawezi kuwa mkweli, unajua mgonjwa hawezi kuja kusema alitumia kitu fulani, mara nyingi wanafichaficha labda tatizo liwe kubwa zaidi ndipo wanasema ukweli,” amesema.

Dk Neema amesema kama mgonjwa ametumia vitu hivyo na hajapata athari hawezi kupata athari baadaye.

“Si kwamba athari hizo zinakuwa za taratibu, kama amepona na haikuonekana kupata shida yoyote haiwezi kutokea tena baadaye,” amesema.

Meneja Mpango wa Taifa wa huduma za macho kutoka Wizara ya Afya, Dk Bernadetha Shilio amesema wapo wagonjwa wanaopata athari, lakini hawana takwimu, akisisitiza ni muhimu wagonjwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu.

“Taarifa hizi zinatolewa na wataalamu wa afya, yaani madaktari kwenye vituo husika, labda mimi kuna mtu amekuja amefanya hivi na vile lakini kutoa hali ilivyo kwa sasa wangapi wamethirika kwa sasa bado.

“Hata leo nimepewa taarifa kuna mtu anatumia sijui vitu gani, lakini pia kuna taarifa za uvumi kuna mtu katoka huko anashauri wagonjwa wanywe Azuma inatibu, huo ni uongo,” amesema.

Dk Shilio amewataka wagonjwa waepuke kutibu macho kwa kutumia kitunguu saumu kwa kuwa kunaweza kusababisha michubuko kwenye ngozi ya jicho na kioo cha mbele ya jicho, hivyo kuathiri uwezo wa jicho kuona.

“Maji ya chumvi yanaweza kusababisha michubuko au kidonda kwenye kioo cha mbele cha jicho, hivyo kutengeneza kovu litakalopunguza uwezo wa jicho kuona au ulemavu wa kutoona wa kudumu,” amesema.

“Matumizi ya chai ya rangi katika kutibu macho yanaweza kusababisha vidonda kwenye kioo cha jicho na kusababisha kovu kwenye jicho litakalokufanya upate uoni hafifu au upoteze uwezo wa kuona kabisa,” amesema.

Dk Shilio amewataka wagonjwa pia kuepuka kutibu macho kwa mkojo, kwani ni hatari kwa usalama wa macho kwa kuwa mkojo hubeba uchafu na vijidudu vinavyoweza kusababisha maambukizi mengine na kupoteza uwezo wa kuona kabisa.

Amewataka kuzingatia kunawa mikono mara kwa mara na wapatapo ugonjwa huo kuwahi kituo cha afya kwa uchunguzi na matibabu sahihi na kwa wakati.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi