Kitaifa
TTCL yatajwa ya mwisho ubora wa huduma
Katika ripoti ya robo ya nne ya mwaka 2023 iliyotolewa mwanzoni mwa wiki, kampuni ya TTCL ilifaulu kwa asilimia 67.02 katika matukio zaidi ya 280 yaliyotumika kupima ufanisi wa mitandao yote sita.
Ripoti hiyo ambayo hutolewa kila baada ya miezi mitatu, inaonyesha kuwa TTCL ilipimwa kwa matukio 285, Tigo ilipimwa kwa matukio 283 na kupata ufaulu wa asilimia 98.59, ikifuatiwa na Zantel iliyopimwa kwa matukio 280 na kupata asilimia 98.57.
Mtandao wa tatu kwa ubora wa huduma katika ripoti hiyo ni Vodacom Tanzania iliyopimwa kwa matukio 287 na kupata ufaulu wa asilimia 96.86, wa nne ni Airtel iliyopimwa kwa matukio 286 na kufaulu kwa asilimia 95.10, na Halotel nafasi ya tano uliopimwa kwa matukio 285 na kupata ufaulu wa asilimia 90.18.
Miongoni mwa vitu ambavyo mitandao ilipimwa navyo ni uharaka wa kukamata mtandao baada ya simu kuwashwa, muda inaochukua simu kuunganishwa pindi mtu anapopiga, kasi ya huduma ya mtandao, hali ya usikivu na utulivu wa mtandao mtu anapokuwa katika mwendo.
Vingine ni mtandao unapatikana katika eneo la ukubwa gani, hali na ubora wa mtandao unapopatikana pindi mtu anapotaka kutumia na usambazaji wa mtandao wa 2G, 3G na 4G na mengineyo.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari alisema ikiwa mtoa huduma ya mawasiliano atashindwa kufikia kiwango ubora wa huduma walichowekewa huchukuliwa hatua za kiudhibiti.
“Tunachukua hatua za kiudhibiti, ndiyo maana tunawafuatilia, tunaangalia nini wanafanya, changamoto ziko wapi ili kuboresha huduma,” alisema Dk Jabir, alipoulizwa iwapo TCRA inachukua hatua yoyote kwa wenye ufaulu mdogo.
Juhudi za Mwananchi kuwapata TTCL kuzungumzia kilichoelezwa na ripoti hiyo juu ya ubora wa huduma hazikufanikiwa.
Ofisa Mkuu wa Teknolojia na Ufundi wa Tigo, Emmanuel Mallya alisema ubora wa huduma ni matokeo ya uboreshaji walioufanya ndani ya takribani miaka miwili iliyopita.
“Kutokana na utekelezaji wa mpango wa uwekezaji, tumepandisha hadhi minara yetu mingi nchini, mwaka jana tulipata tuzo ya mtandao wenye kasi zaidi Tanzania kutoka taasisi ya Ookla,” alisema Mallya na kuongeza kuwa majiji makubwa yote yamewekewa mawasiliano ya 5G.
Alisema mpaka mwishoni mwa Februari mwaka huu watakuwa wamekamilisha kusambaza mtandao wa 4G katika eneo kubwa la nchi na lengo ni kuendelea kutoa huduma muhimu na zenye ubora wa hali ya juu kwa wateja.
Akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi tuzo yao Tigo, Mkuu wa Ookla Mashariki ya Kati na Afrika, Tristan Muhader alisema ubora wa mtandao wa Tigo si tu unasaidia kuboresha huduma kwa wateja, bali unainua kiwango cha Tanzania katika upimaji duniani.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC), Mary Msuya alisema wao kama watetezi wa watumiaji wa huduma wamekuwa wakiwasiliana na wadau, ikiwemo TCRA au mtoa huduma ikiwa watapokea malalamiko ya kusuasua kwa huduma katika baadhi ya maeneo.
“Tukishawasiliana nao, wao wanaenda kuangalia ubora wa huduma, kama haitafikia kipimo TCRA itawasiliana na mtoa huduma, haya yote yanafanyika ili kuhakikisha mtu anayepewa huduma anafurahia kile anachokilipia,” alisema. Alisema hilo pia huweza kufanywa kwa mashauriano ya pamoja kati yao wadau, TCRA na watoa huduma kwa kuangalia kwa pamoja changamoto ambazo zinaathiri utoaji wa huduma.
Ushauri kwa TTCL
Mhadhiri msaidizi wa benki na fedha katika Chuo kikuu Ardhi (ARU), Aziz Rashid, alishauri TTCL kufanya mageuzi ya kibiashara ili kuwa na mawazo na muundo wa kiuendeshaji sawa na washindani wake katika biashara ya huduma za simu.
“Wafanye mageuzi na kukumbatia usasa katika uendeshaji wa shughuli zao sawa au zaidi ya washindani wao au kuangalia maeneo ambayo ni ya kimkakati kwao,” alisema Rashid.
Alisema TTCL wanaweza kuamua kuwekeza zaidi kwenye mifumo inayotoa suluhu ya huduma za fedha kidijitali au kuwekeza katika mkongo wa Taifa na teknolojia zinazoendana na hizo.
Machi mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2021/2022, alisema wazi kuwa TTCL imeshindwa kwenye biashara ya mawasiliano ya simu na hivyo akapendekeza ibaki kusimamia kampuni za mawasiliano ya simu na mkongo wa Taifa wa mawasiliano.
“TTCL na biashara ya simu frankly speaking (nikiongea ukweli) limewashinda, waendeshe lile linalowezekana, washike mkongo ili wa monitor (wasimamie) wenzao, wao wakiingia kwenye simu na mkongo ni wa kwao kunakuwa hamna ushindani ulio sawa,” alisema Rais Samia.
Alisema kuna haja ya tafakari ya kina kuona iwapo kuna haja ya shirika hilo kuendelea na biashara ya simu au kuendelea na maeneo mengine, ambayo alisema yapo mengi yanayoweza kufanyiwa kazi kwa ufanisi.