Kitaifa
RC Chalamila aeleza sababu vyombo vya dola kutoshiriki usafi
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema sababu za vyombo vya ulinzi na usalama kutoshiriki kufanya usafi leo kama aliyoeleza awali, imetokana na Jeshi la Polisi kutoa kibali cha maandamano kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Chalamila amesema vyombo hivyo vitashiriki kikamilifu usafi huo Jumamosi ya Januari 27, 2024.
Awali, Januari 13, 2024 Chalamila alitangaza kuwa Januari 23 na 24 mwaka huu ni siku ya usafi ambayo vyombo vya dola vingeshiriki.
Hata hivyo, jana na leo vyombo hivyo havijaonekana vikishiriki usafi huo, huku Chalamila na wasaidizi wake wakionekana kuwaongoza wananchi kufanya usafi leo Stendi ya Malamba Mawili wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam.Akizungumzia kutokuwepo kwa vyombo vya ulinzi na usalama, Chalamila amesema waliona vyombo hivyo kushiriki sio sawa kwa sababu Mkuu wa Jeshi la Polisi alikuwa tayari ametoa ruhusa ya kufanyika maandamano hayo.
“Tumeona vyombo hivyo vikishiriki, Chadema wasije wakasema maandamano yao yamevurugwa na vyombo vya dola. Hivyo, tumewaacha wayafanye kwanza ili wasije wakasema demokrasia yao ya maandamano ilizuiwa.
“Kwa nini tumefanya hivyo, kwenye sheria kuna vifungu vinasema unapompa kwa mkono huu halafu unamnyang’anya kwa mkono huu sio sawa. Hivyo tuliona kama maandamano yameruhusiwa polisi huwezi tena kuwapeleka barabarani,” amesema Chalamila.
Kuhusu ugawaji wa vifaa vya usafi, kama alivyoahidi amesema amevigawa tangu Januari 22, 2024 na aliona afanye tukio hilo kimyakimya ili kuepusha kuleta taharuki.
“Ugawaji wa vifaa, nilifanya kama nilivyoahidi kufanya Januari 22, sema hatukutaka ku-draw attention,” amesema Chalamila.
Mwakilishi wa Chadema Wilaya ya Ubungo, James Salao ameishukuru Serikali kwa kuruhusu maandamano, akisema miaka ya nyuma yalipigwa marufuku.
Akizungumzia suala hilo, mkazi wa Malamba Mawili, Emily Nkya amesema Serikali imefanya jambo la kiungwana kuacha maandamano yaendelee, kwa kuwa awali matukio hayo yalileta hofu ya kutokea vurugu.
Mkazi mwingine Evod James, amesema kilichofanywa na Serikali ni kuonyesha ukomavu wa demokrasia, huku akiitaka Chadema ifanye maandamano ya amani kama ilivyoahidi.