Kitaifa
Mzozo waibuka ununuzi wa mabehewa, vichwa vya treni
Dar es Salaam. Vita vya ununuzi wa injini na mabehewa ya mtumba kwa ajili ya reli ya kisasa (SGR) vimeibuka kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Kampuni ya Eurowagon Demiryolu Ticaret ve Limited ya Uturuki.
Mvutano huo umejikita kwenye upatikanaji wa injini mbili za mabehewa 30 kwa ajili ya majaribio na matumizi ya mradi wa SGR wa Tanzania.
Nyaraka ambazo gazeti dada la The Citizen limeziona zimefichua mzozo uliopo kati ya pande hizo mbili, huku kila upande ukiulalamikia mwingine na kutoa vitisho.
Katika barua yake, Wakili wa Eurowagon Demiryolu Ticaret ve Limited ameonya kuchukua hatua ikiwa makubaliano ya mteja wake hayatatekelezwa kufikia Januari ya mwaka huu.
“Tutalazimika kufanya tathimini ya zabuni nyingine kuhusu mabehewa ya treni kama makubaliano hayatawezekana kukamilishwa,” imesema barua hiyo.
Mgogoro huo unahusisha mkataba uliosainiwa Oktoba 1, 2020 kati ya TRC na Eurowagon Demiryolu Ticaret ve Limited kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa 30 ya abiria na vichwa viwili vya treni vya umeme kwa jumla ya Euro 26.6 milioni.
Pamoja na malipo ya awali yaliyotolewa na TRC, mambo yalibadilika ilipofika Februari 2022, baada ya shirika hilo kuvunja mkataba baada ya vichwa na mabehewa yakiwa yamenunuliwa na mipango ya usafirishaji ikiwa imekamilishwa.
Barua ya Eurowagon Demiryolu Ticaret ve Limited inadai kuwa, walikuwa wameshakamilisha asilimia 50 ya kazi kwa mujibu wa mkataba ndani ya mwaka mmoja, licha ya changamoto za maambukizi ya Uviko- 19.
Barua hiyo inadai kuwa uamuzi wa TRC kuvunja mkataba Februari 2022 umevuruga makubaliano yaliyokuwa yakiendelea pamoja na kusababisha hasara kwa Eurowagon Demiryolu Ticaret ve Limited.
Barua hiyo inaeleza, “hakuna matokeo ya maana yaliyofikiwa na hasara iliyosababishwa kwa mteja wangu na TRC inaendelea siku hadi siku.”
Imeendelea kuonya kwamba, ikiwa makubaliano hayatafikiwa hadi Januari 2024, Eurowagon Demiryolu Ticaret ve Limited haitakuwa na jinsi isipokuwa kufanyia tathimini zabuni nyingine kwa ajili ya mabehewa.
Waraka huo umefafanua kuwa, uamuzi wa Eurowagon Demiryolu Ticaret ve Limited kukarabati na kuyaunda upya mabehewa na mchakato wa kusafirisha mabehewa hayo, utabaki Ujerumani kama makubaliano hayatafikiwa na kuafikiana kulipa fidia.
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo jana, Kaimu mkurugenzi mkuu wa TRC, Amina Lumuli alikiri kupokea barua ya wazi (LC) na kueleza kutotekelezeka matakwa ya barua hiyo ambayo ni mkataba wa benki anayotumia mnunuzi kulipa endapo meli itafikisha mzigo uliokusudiwa.
Barua ya TRC iliyokuwa ikijibu kampuni hiyo ilisema, shirika hilo limebaini madai pamoja na masharti mengine katika barua ya wazi.
Lumuli, ambaye pia ni mtia saini wa TRC alifafanua kuwa, “haikuwezekana katika hatua hiyo ya majadiliano kwa TRC kufanikisha matakwa ya mdai ambayo ni kiini cha majadiliano na bado pande za majadiliano hazijaafikiana.
Hata hivyo, TRC imeiomba Eurowagon Demiryolu Ticaret ve Limited, kurejea mawasiliano na Deutsche Bhan (DB) ya kuachilia mabehewa 17 yaliyo chini yake.
TRC imependekeza kuachiliwa kwa mabehewa ili kufanikisha ukarabati wakati majadiliano yakiendelea.
“Gharama za kuegesha mabehewa zitakuwepo kwa DB zitajadiliwa pembeni, tunaomba mkubali na kuheshimu ombi letu,” inaeleza barua ya TRC.
Nyaraka hizo pia zimefichua kuwa, pande mbili zimefanya mikutano Novemba 12, 2023 kujadili mambo yaliyobaki yaliyoibuka wenye mkataba, lengo likiwa ni kuendeleza uhusiano mwema na masilahi kati ya Uturuki (mkandarasi wa SGR) na Tanzania.