Connect with us

Kitaifa

Majaliwa, naibu waziri mkuu China wagusia masuala ya kiuchumi

Dar es Slaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Liu Guozhong aliyewasili nchini jana Jumatatu Januari 22, 2024 kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Mazungumzo ya viongozi hao wawili yamefanyika leo Januari 23, 2024 katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam, kuhudhuriwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko na viongozi wa Serikali kutoka Jamhuri ya Watu wa China na Tanzania.

Majaliwa amesema ujio wa kiongozi huyo unatokana na mahusiano mazuri yaliyopo tangu enzi za waasisi wa nchi hizo mbili ambapo mahusiano hayo yameendelea kunufaisha wananchi wa Tanzania na China, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa.

“Mazungumzo yetu leo yamegusa masuala ya kiuchumi tukizingatia programu ya sasa ya nchi ya Tanzania ya kukuza uchumi, pia tumezungumzia masuala ya biashara na uwekezaji ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile viwanja vya ndege, barabara na uboreshaji wa nishati ya umeme,” amesema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amesema China imekuwa ikifanya uwekezaji nchini, huku akitolea mfano ujenzi wa reli ya kati, na kwamba China imetoa mkopo nafuu.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema kuwa wamegusia pia kuhusu uimarishaji wa mipango mikakati ya nchi ya China kwa nchi za Afrika (FOCAC), ambao imedhamiria kusimamia maendeleo ya Afrika katika afya, elimu, miundombinu na nishati na kwamba Tanzania tayari imewasilisha miradi nane.

Ameongeza kuwa Tanzania imeieleza China kuhusu nia yake ya kuukuza uchumi wa buluu, kwani kuna fursa za kutosha na uwekezaji bado unahitajika, hivyo imealika kampuni kubwa kutoka China kuwekeza kwenye eneo hilo kufanya uvuvi wa kisasa hivyo Tanzania iwe wazalishaji wakuu wa samaki.

Pia amesema mazungumzo yao yaligusa sekta ya afya huku maboresho ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) yakitajwa, ili itoe huduma bora zaidi na kwamba Serikali ya China inafadhili suala hilo, ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa madaktari na mafunzo nchini China.

Pia, wamezunguzia kuhusu uboreshwaji wa sekta ya kilimo na Naibu Waziri Mkuu wa China ameahidi kuwakutanisha mawaziri wa kilimo wa nchi hizo wajadiliane na waone maeneo ya ushirikiano na teknolojia inayohitajika kuboresha sekta hiyo hasa kwenye eneo la umwagiliaji ambapo kunahitajika mitambo mikubwa kuboresha suala la umwagiliaji.

Kwa mujibu wa Majaliwa, China imekubali soko la nchi hiyo litumike kama soko la bidhaa za Tanzania kwa kuwa nchi hiyo ina mahitaji kubwa ya nafaka kama vile maharage ya soya, korosho na mazao mengine, hivyo amewasihi Watanzania wachangamkie  fursa hizo.

Amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na China, ili kuweza kufanya biashara, kushirikiana katika siasa na masuala ya kijamii kwa ujumla wake.

 Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu Liu amesema China itaendelea kuifanya Tanzania nchi ya kimkakati katika mashirikiano kwenye sekta za biashara, uwekezaji na kilimo ikiwemo kuwa soko la mazao ya parachichi, maharage pamoja na korosho.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi