Connect with us

Kitaifa

BoT yatangaza ukomo wa riba mikopo yake kwa benki

Dar es Salaam. Benki kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza ukomo wa riba ya asilimia 5.5 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 kati yake na benki za biashara nchini kuanzia jana.

BoT imeanzisha utaratibu huo ili kuongeza uwezo wa kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Benki Kuu imeanza kupanga riba kwa mara ya kwanza na itakuwa ikibadilika kila baada ya miezi mitatu baada ya Kamati ya Sera ya Fedha kukutana na kufanya tathmini ya mwenendo wa uchumi na mwelekeo wake.

Hata hivyo, kupangwa kwa riba hizi, bado kutaendelea kuweka wigo kwa benki za biashara kuweka viwango tofauti vya riba kulingana na huduma wanazotoa na hali ya soko.

Akizungumza leo Januari 19 baada ya kuzindua mfumo mpya wa Sera ya Fedha unaotumia riba ya BoT, Gavana wa benki hiyo, Emmanuel Tutuba alisema upangaji wake unategemea sana uwazi ili kufikia malengo yake ya kukabiliana na mfumuko wa bei na kuchangia ukuaji wa uchumi.

“Ni matumaini yangu kuwa riba hii itatoa mwelekeo kwa taasisi za fedha katika utekelezaji wa shughuli zake, ikiwemo ukokotoaji wa riba za huduma na hivyo kuongeza ufanisi wa sera ya fedha katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha shughuli za kiuchumi,” amesema Tutuba.

Amesema kiwango cha asilimia 5.5 kilichowekwa kati ya BoT na benki za biashara kinaendana na malengo ya kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabakia ndani ya lengo la asilimia 5 na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia lengo la asilimia 5.5 au zaidi kwa mwaka 2024.

Amesema riba hiyo pia imezingatia lengo la kuhakikisha thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni inaendelea kuwa imara.

Amesema ili kuwezesha kufikiwa kwa malengo hayo BoT itatumia nyenzo mbalimbali za sera za fedha kuhakikisha riba katika soko la fedha baina ya benki hapa nchini inakuwa tulivu.

“Hivyo, Benki Kuu itakuwa inafuatilia mwenendo wa riba ya mikopo ya siku 7 katika soko hilo na kuchukua hatua kuhakikisha mabadiliko ya riba hiyo yanakuwa ndani ya wigo usiozidi asilimia 2 chini au juu ya Riba ya Benki Kuu,” amesema Tutuba.

Pia mabadiliko haya yanafanyika ili kutekeleza itifaki ya kuanzisha Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuelekea kuwa na sarafu moja na Benki Kuu moja ya Afrika Mashariki.

Akizungumza kwa niaba ya wengine, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Benki nchini (TBA), Geofrey Mchangila amesema sera hii inaanza kutumiwa rasmi baada ya kusemwa kwa miaka mingi bila kufanyika kwa utekelezaji.

“Hiki kilichofanyika ni mafanikio makubwa na tuna kila sababu ya kupongeza, wakati tunaondoka katika mfumo unaotumia ujazi wa fedha na kuja katika mfumo wa kutumia riba tuna kila sababu ya kujivunia.”

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi