Connect with us

Kitaifa

Maajabu shule yaandikisha wanafunzi watatu Rombo

Rombo. Inawezekana yakawa ni moja ya maajabu duniani yanayofaa kuingia katika kitabu cha maajabu cha Guiness, baada ya Shule ya Msingi Mlembea iliyopo wilayani Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro kuandikisha wanafunzi watatu pekee wa darasa la kwanza mwaka 2024.

Shule hiyo ambayo ni miongoni mwa 162 za msingi zilizopo wilayani Rombo, ina jumla ya wanafunzi 90.

Wakati shule hiyo ikiwa na hali hiyo, kuna shule nyingine za msingi katika baadhi ya mikoa zikiwa zimeandikisha zaidi ya wanafunzi 800 hadi 3,000.

Shule hiyo imekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii kuanzia wiki iliyopita baada ya taarifa kusambaa kuwa imeandikisha wanafunzi watatu tu wa darasa la kwanza na watoto sita wa darasa la awali, hivyo kufanya shule kuwa na wanafunzi wapya tisa.

Inaelezwa idadi ya wanafunzi imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka shuleni hapo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uwepo wa mzunguko wa shule zaidi ya nne katika eneo hilo pamoja na baadhi ya wazazi kupeleka watoto katika shule za binafsi.

Pamoja na maelezo ya watendaji wa Serikali wa wilaya hiyo akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rombo, Godwin Chacha kueleza kiini, kiu ya Watanzania ni kutaka kujua inaendeshwaje na wanafunzi hao wachache.

Baadhi wanahoji mitandaoni shule hiyo kuendelea ikiwa hivyo na walimu watano, ni matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali, huku wakipendekeza ama shule hiyo iunganishwe na shule jirani zinazoizunguka au kuibadili matumizi yake.

Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1975, ipo Kata ya Olele, Tarafa ya Mashati na kimazingira, haina uzio na wanafunzi wanaosoma hapo wanatoka katika vitongoji viwili na kuna wakati hutoroka kwenda nyumbani kula na kurudi shuleni.

Upatikanaji wa taarifa za shule hiyo baada ya kusambaa mitandaoni umekuwa mgumu kiasi kwamba mwandishi anayetaka kuitembelea hukataliwa na mwalimu mkuu ambaye hakutaka kutaja jina lake, akitaka lazima kuwe na kibali cha Mkurugenzi.

Iliwawia vigumu waandishi wetu hata kupata picha za mazingira ya shule hiyo kutokana na uongozi wa shule kutowaruhusu na kuwataka waende na kibali na hata walipotoka, walisindikizwa mpaka getini.

Hii yote ilikuwa ni kuhakikisha kuwa hawachukui picha bila kibali cha mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo na jitihada za kupata kibali ilikuwa jambo gumu kuwezekana.

Kwa mwonekano wa majengo, baadhi ni machakavu yanayohitaji ukarabati mkubwa na pia shule ipo karibu na makazi ya watu, hivyo inakuwa rahisi kuwepo mwingiliano kati ya wananchi na watoto na walimu wanaofundisha hapo.

Alichokisema DED, DC Rombo

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Godwin Chacha amesema shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 90, imepanga kuandikisha wanafunzi wasiozidi 11 wa darasa la kwanza mwaka huu.

Akielezea sababu za shule hiyo kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi, mkurugenzi huyo amesema ni kutokana na eneo hilo kuwa na mzunguko wa shule nyingi pamoja na baadhi ya wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi.

“Pale kuna mzunguko wa shule za msingi nne, hivyo wananyang’anyana wanafunzi, lakini pia watu wengine wamepeleka watoto wao kwenye shule binafsi, lakini jumla ya wanafunzi katika shule hii ni kama 90.

“Hivyo huwezi kutarajia kupata wanafunzi wengi wakati hata hao wa madarasa ya juu ni wachache,” amesema mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi huyo amesema wamejiwekea mipango mbalimbali ikiwemo kugeuza baadhi ya shule kuwa za mchepuo wa Kiingereza, ili kuvutia wazazi kutoka maeneo mbalimbali ya Rombo na nje ya Rombo kupeleka watoto wao katika shule hizo.

“Pia tumependekeza baadhi ya shule kuziunganisha kuwa moja kiutawala, maana kuna shule zipo katika eneo moja, lakini nyingine unakuta ina wanafunzi 100 na nyingine 200, hivyo zikiunganishwa itasaidia rasilimali kutumika vizuri,” amesema.

Hii ni pamoja na walimu kutumika kwa umoja na kuboresha upatikanaji wa elimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala hakutaka kuingia kwa undani kuhusu uchache huo wa wanafunzi, amesema mpaka sasa wilaya wameandikisha wanafunzi 4,639 wa awali na 4,454 wa darasa la kwanza.

“Tuliweka malengo ya kuandikisha wanafunzi 5,175 wa darasa la awali na tayari tumeandikisha 4,639 sawa na asilimia 90 na kwa darasa la kwanza tumelenga kuandikisha wanafunzi 4,932 na tumeshaandikisha 4,454.

“Hii ni sawa na asilimia 90 na taarifa hii ni mpaka Alhamisi ya Januari 11, 2024,” amesema na kuongeza;

“Wanafunzi wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha darasa la kwanza na awali, zipo shule zimevuka malengo ikiwemo Shule ya Msingi Ubaha ambayo maoteo kwa darasa la awali ilikuwa ni wanafunzi 22.”

Hata hivyo, amesema shule hiyo hadi sasa imeandikisha wanafunzi 60, lakini darasa la kwanza wanafunzi waliopaswa kuandikishwa ni 30 na tayari wameandikishwa 40.

“Zipo shule ambazo maoteo yake ni idadi ndogo kutokana mazingira, lakini kwa ujumla uandikishaji wa wanafunzi hawa unakwenda vizuri na tumejipanga kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapelekwa,” amesema.

Mkuu huyo wa wilya amesema tayari wameanza msako wa nyumba kwa nyumba na hata kwenye magulio na masoko, ili kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanakwenda na kutimiza haki zao za kimsingi za kupata elimu.

Wananchi washauri

Rust Tarimo, mkazi wa Olele amesema uchache wa wanafunzi shuleni unatokana na uamuzi wa mzazi ni wapi ampeleke mtoto kwa kuwa kila mzazi anatamani kuona mwanaye akisoma katika mazingira mazuri na kufikia malengo ya ufaulu.

“Mlembea ni shule yetu na watoto wangu wote wamesoma katika shule hii,”amesema mwananchi huyo anayeishi jirani na shule hiyo.

“Lakini kwa sasa wanafunzi ni wachache sana na hii ni kutokana na kwamba sisi huku temezeeka na watoto wetu wametawanyika wanafanya kazi maeneo mbalimbali, hivyo hawawezi kuleta watoto wao kusoma huku,” amesema Tarimo.

“Pia eneo hili lina shule mbalimbali za msingi, kila mzazi anaamua ampeleke mtoto wake wapi kulingana na taaluma za shule, nishauri Serikali iliangalie hili kama wanafunzi watazidi kuwa wachache, wanafunzi wahamishwe shule jirani.”

“Miundombinu hii ya shule inaweza kuboreshwa na kujengwa hata ufundi au kutumika kwa matumizi mengine, maana huwezi kulazimisha mzazi alete mtoto Mlembea wakati si malengo yake,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Yuda Gervas amesema pamoja na sababu zilizotajwa kusababisha uchache wa wanafunzi, Serikali inapaswa kulitazama hilo na kuhakikisha inaboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia shuleni hapo.

“Serikali itazame shule hii kama inapaswa kuendelea au wanafunzi wahamishiwe shule jirani, kwani kama unavyoiona wanafunzi wanaosoma hapa wanatoka jirani na shule na wakati mwingine mchana wanatoroka kwenda nyumbani kula na kurudi, kwani anaweza kuona kila kinachoendelea shule akiwa nyumbani,” amesema Gervas.

Katika matokeo ya kitaifa ya upimaji  wa darasa la nne mwaka huu yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 13 na wanafunzi sita wamepata daraja C, wanne daraja D, huku watatu wakitakiwa kurudia darasa. Hii ndio shule ya msingi Mlembea.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi