Kitaifa

Mafundisho ya Profesa Janabi yamuibua Waziri Ummy

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesisitiza jamii kuyazingatia mafundisho ya masuala ya lishe yanayotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi.

Profesa Janabi kupitia vyombo vya habari amekuwa akitoa elimu kwa jamii kuhusu lishe bora.

Mafundisho hayo na mengine yamekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakipakia picha ya pilau mtandaoni akiambatanisha maelezo kuwa Profesa Janabi amekataza.Baadhi ya mafundisho yake ni idadi ya bia anayopaswa kunywa mtu kwa siku ambapo mwanaume anatakiwa kunywa mbili na mwanamke moja.

Pia Profesa Janabi amewahi kusisitiza jamii kuepuka ulaji wa wanga kwa wingi, matumizi ya sukari nyingi, chumvi ya mezani huku akisisitiza umuhimu wa kutokula vyakula vigumu usiku bali kutumia matunda.

Mbali na hayo aliwahi kueleza mwanaume si sahihi kuwa na unene mkubwa hadi kuvaa kiuno namba 40 ya suruali, na kiuno hakipaswi kufikia upanda wa mita 35.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya afya leo Jumatano, Januari 10, 2024 Waziri Ummy amesema japo mafundisho hayo hata yeye yanamtisha, lakini jamii isiyapuuze.

Kauli hiyo ya Ummy imemgusa Profesa Janabi wakati akieleza mkakati wa kudhibiti magonjwa nchini kwa mwaka 2024.

“Watu wanafanya mzaha na Profesa Janabi na mafundisho anayotoa japo wakati mwingine hata mimi ananitisha, mimi ni mwanafunzi wake na ameniharibu tangu Mei mwaka jana sinywi chai yenye sukari,” amesema.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi